


.jpg)
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limekiri kwamba lmichuano mipya ya Ligi ya Super8 haikuwa kwenye kalenda lakini linazishauri klabu za Simba na Yanga kushiriki ili kuwasaidia wachezaji wao kupata mechi nyingi za maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Bara ambayo itafanyika kuanzia Septemba Mosi.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema kwamba ligi hiyo imeanzishwa baada ya kutofanyika kwa mashindano ya Kombe la Taifa yaliyokuwa yakitoa nafasi kwa wachezaji kuwa na mechi nyingi zaidi na vile vile kutoa nafasui ya kuvumbua vipaji vipya.
Osiah alisema kuwa hawaamini kwamba endapo Simba na Yanga zitashiriki ligi hiyo zitavuruga programu za mazoezi za makocha wao na badala yake, wachezaji watapata nafasi ya kujiandaa vizuri na msimu ujao wa ligi.
"Hatukuyaweka kwenye kalenda, tulikuwa njia panda katika kuikubali ligi hii na Taifa Cup (Kombe la Taifa) ambalo wadhamini wake (Kampuni ya Bia-TBL) sasa wameelekeza nguvu zao katika kuidhamini Taifa Stars," alisema Osiah.
Hata hivyo, Osiah aliongeza kwamba endapo Simba na Yanga zitashindwa kushiriki, watateua timu nyingine ambazo zilifanya vizuri kwenye msimu uliopita wa ligi na kuanzia mwakani wataweka kanuni maalumu ili kuwepo na heshima na thamani ya michuano hiyo.
Aliongeza kuwa jana, TFF ilitarajiwa kukutana na Simba kujadili mapendekezo yao huku ikisema kwamba haijapokea barua yoyote kutoka Yanga ili kuthibtisha kuwa itashiriki au vinginevyo.
Osiah alisema vilevile kuwa leo TFF itakuwa na kikao cha maandalizi na wadhamini hao ambao wamesaini mkataba wa miaka mitatu kuidhamini ligi hiyo mpya itakayochezwa kwenye vituo vinne tofauti.
Ligi hiyo ya Super8 inatarajiwa kushirikisha timu nane kutoka Tanzania Bara na Visiwani na kudhaminiwa na benki ya ABC.
Tayari timu mbili za Bara, Azam na Polisi Morogoro iliyopanda daraja msimu huu zimethibitisha ushiriki wake.
Simba ambao ndio mabingwa wa Ligi Kuu ya Bara, hivi sasa wanafanya mazoezi ya viungo bila ya kuwa na kocha wao Milovan Cirkovic wakati Yanga wako kwenye mapumziko na wataanza kujifua tena kuanzia keshokutwa.