Sunday May 1, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Wazee Yanga kumburuza Nchunga Takukuru

23rd May 2012
Print
Comments
Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Lloyd Nchunga.

Hali ndani ya Yanga bado si shwari na jana wanachama wa klabu hiyo wanaoongozwa na Baraza la Wazee wametangaza kumpeleka mwenyekiti wa klabu hiyo, Lloyd Nchunga, katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) kwa madai kwamba ametumia vibaya fedha za klabu hiyo.

Hata hivyo, Nchunga juzi aliliambia gazeti hili kwamba yeye bado ataendelea kuwa mwenyekiti wa Yanga mpaka maamuzi mengine yatakapotolewa kwenye mkutano mkuu na si nje ya hapo huku jana akishindwa kupatikana kwenye simu yake ya mkononi kuelezea maamuzi hayo ya kupelekwa TAKUKURU.

Akizungumza kwa niaba ya wanachama wenzake, Katibu wa Baraza la Wazee, Ibrahim Akilimali, alisema kuwa wameamua kufikia maamuzi hayo baada ya kufahamu Yanga inakusanya zaidi ya Sh. milioni 100 kila mwezi lakini wanashangaa kuona wachezaji na watendaji wengine wa klabu yao hawajalipwa mishahara tangu mwezi Februari.

Akilimali alitaja baadhi ya wanaoipatia Yanga fedha kila mwezi ni mdhamini wao, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) inayotoa Sh. milioni 25, Push Mobile (Sh. milioni 3) na mmoja wa wanachama wao ambaye alitoa Sh. milioni 75 ili kusaidia mishahara ya wachezaji.

"Tumefikia kwenda huko kwa Hosea ili kukomesha ufisadi ndani ya Yanga, tunaona hujuma zinatokea ndani ya Yanga," alisema Akilimali.

Alisema pia wao walikutana ili kupata idadi ya wanachama ambao wanaweza kuomba Mkutano Mkuu wa dharura na wanaifahamu katiba yao tofauti na kauli ya Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah, aliyoitoa kuhusiana na mkutano wao uliofanyika Jumapili.

Alieleza kwamba wanachama wamefikia maamuzi ya kumtaka Nchunga aondoke madarakani baada ya kushindwa kutekeleza na kusimamia kazi zake kwa ufanisi na kufikia malengo kama ilivyobainishwa katika Ibara ya 33 ya katiba yao iliyopitishwa mwaka 2010.

Vile vile Akilimali alisema kuwa kutokana na klabu kutokuwa na Makamu Mwenyekiti (Davis Mosha - alijiuzulu nafasi hiyo) imewalazimu kumtaka kiongozi huyo wa juu kuachia ngazi na hatimaye kuitisha uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi.

"Sisi tuna mgogoro mkubwa, TFF walipaswa kutukutanisha ili kumaliza tatizo hili na si kukaa upande mmoja, Yanga ndio tutakaoumia kwa sababu tutashindwa kusajili wachezaji wazuri na tulionao watatukimbia kwa sababu ya migogoro yetu," Akilimali alieleza.

Alitishia kuwa endapo Nchunga ataendelea kukaa madarakani na TFF ikaendelea kumtambua watafanya taratibu za kuihamishia klabu hiyo Zanzibar ambapo wanaweza kutwaa ubingwa na kushiriki kwenye mashindano ya kimataifa.

Naye Bakili Makele alisema kuwa tayari wameshafikisha rasmi taarifa za mgogoro wao na uongozi katika ofisi ya Afisa Utamaduni, TFF na kwa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo wa Wilaya ya Ilala.

Makele alisema kuwa TFF imewadhalilisha wana-Yanga na ili kumaliza mgogoro uliopo walipaswa kuwakutanisha na si kuzungumza na upande mmoja.

"Soka haliendeshwi kwa migogoro, tunachotaka sisi ni kuona Yanga iko vizuri hakuna anayekiuka katiba," aliongeza.

Alisema kuwa wao wanachotaka kuona ni kufanyika kwa Mkutano Mkuu mapema ili kupata viongozi wengine watakaoendesha zoezi la usajili na kufanya maandalizi ya timu yao hatimaye waweze kutetea Kombe la Kagame na kujifariji.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles