Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Nida saidia kumulika uchafu wote

17th May 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Taarifa kwamba Jeshi la Ulinzi la Wananchi Watanzania (JWTZ) na Jeshi la Polisi wameanza kufanyia kazi taarifa zilizotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) za kuwepo kwa wanajeshi 248 na polisi 700 walioghushi vyeti vya elimu, zinatia moyo.

Vyeti vya watumishi hao vinadaiwa kufanana na vyeti vilivyowasilishwa na watumishi wengine wa umma. Huu unaelezwa kuwa ni udanganyifu mkubwa uliobainishwa na Nida katika mchakato wa kutoa vitambulisho vya taifa unaoendelea kufanywa na mamlaka hiyo.

Taarifa kwamba JWTZ na Polisi wanafanyia kazi taarifa hizo zilitolewa kwa waandishi wa habari na kuahidi kuwa watashirikiana na wadau wengine ikiwemo Nida, kwa kufanya uchunguzi ili wahusika watakaobainika wachukuliwe hatua kwa mujibu wa kanuni za majeshi.

Matamko haya yanatia moyo kwa sababu ni hatua za kujisafisha na kuondokana na tatizo hilo katika taasisi hizi nyeti za ulinzi wa taifa, raia na mali zao.

Tunajua na kama walivyosema wasemaji wa JWTZ na Polisi kuwa kuwasilisha vyeti vya kughushi kulingana na kanuni za utumishi wa vyombo hivyo viliwili ni kosa za kufukuzwa na kushitakiwa, pia kwa mujibu wa sheria za nchi kughushi nyaraka ni kosa la jinai.

Tunaamini wakati uchunguzi ukifanywa na vyombo hivi suala hilo litaangaliwa kwa makini na siyo kuchukuliwa kijuujuu tu. Tuhuma hizi hadi sasa zimeacha taasisi hizo katika taswira mbaya sana mbele ya jamii.

Kama walivyosema wasemaji wa majeshi haya kwamba hadi sasa taarifa hizi zinabakia kuwa ni madai tu hadi uchunguzi utakapofanywa na kukamilika, nasi tunaunga mkono, lakini ikumbukwe kuwa tuhuma hizi hazionyeshi picha nzuri katika mambo mawili makubwa; kwanza utaratibu wa kusaili maombi ya wanaotaka kujiunga na majeshi yetu una mianya mingi inayoruhusu udanganyifu, lakini la pili, uadilifu wa baadhi ya watu wanaoomba kujiunga na taasisi hizi zenye wajibu adhimu wa ulinzi, usalama wa taifa, uhai wa raia na mali zao ni wa kutiliwa shaka sana.

Tunasema haya kwa kuwa katika mazingira ya kawaida jeshini siyo mahali pa kuruhusu usaili ufanywe kwa njia nyepesi ambazo hazijiridhishi pasi na shaka yoyote kuwa huyo anayewasilisha nyaraka zozote kuhusu maisha yake, kwa hakika ndiye mwenye nazo. Hili linawezekana sana kufanywa uthibitisho (verification) wa kila cheti.

Uthibitisho huu ungehusu kwa mfano, kufuatilia kokote vyeti hivyo vilikotolewa, kulinganisha taarifa zote kama zinaoana kwa nia ya kujihakilishia pasi na shaka kuwa wanaochukuliwa kuunda majeshi yetu, ni watu wakweli, waadilifu na ambao hakika wako mbali na kile kinachotokea mitaani, kuungaunga tu vyeti kwa ajili ya kupata kazi.

Tunajua taifa hili kwa sasa linakabiliwa na janga kubwa la kughushi vyeti vya elimu. Watu wengi ambao waliona ni udhia kusoma kwa bidii wakiwa shuleni, huja kushtuka baadaye kwamba walipoteza muda wao wakifanya mambo ya ovyo ovyo, kwa bahati mbaya hali hiyo hutokea katika kipindi ambacho ama hawawezi tena kurejea shule kupata vyeti kama vya kidato cha nne na sita, au wanaona kuwa gharama ya kufanya hivyo haibebeki tena kwa sababu tayari wanakabiliwa na wajibu mwingine kulingana na umri wao.

Haya yalipata kutokea kwa watu walioomba kugombea ubunge na kufanikiwa kisha wakachaguliwa, lakini wakaishia kuwa aibu ya mwaka kwa jamii.

Hata hivyo, inawezekana sana kwamba wapo baadhi ambao wamekalia ofisi kubwa za umma kwa kutumia vyeti vya kughushi, na inawezekana wakawa sababu mojawapo ya mambo kutokwenda kama iliovyotarajiwa katika ofisi za umma.

Tunafarajika kwamba pamoja na ukweli kwamba Nida hawajaanza kutoa vitambulisho vya uraia rasmi, umuhimu wa kuwako kwa mamlaka hii kwa ajili ya kusaidia taifa kujipanga kwa kujua watu wake wako wapi, wanafanya nini na wana nini, umeanza kujionyesha.

Kwa kawaida Nida imekuwa na msemo wake maarufu kwa wadau wake wakati ikijitangaza, kwamba itasaidia mifumo kuzungumza. Kwa hili la kughushi vyeti inaanza kuthibitisha kwamba sasa mifumo itazungumza. Tuongeze ushirikiano kujenga taifa.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles