Sunday May 1, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Polisi katika kashfa nzito Songea

25th September 2011
Print
Comments
  Familia yaituhumu kutorosha mtuhumiwa wa mauaji
  Polisi wasema baadhi ya ndugu wanahusika na mauaji

Mvutano mkubwa unaohusisha mauaji ya mkazi wa mjini Songea, mkoani Ruvuma, Flora Matembo na mwanaye, Dickson Matembo, waliouawa kwa kukatwakatwa na mapanga na kunyongwa, umeibuka kati ya familia ya marehemu na Jeshi la Polisi mkoani humo, kuhusu mtuhumiwa halisi wa mauaji ya watu hao.

Flora na mwanaye, waliuawa Januari 11, mwaka jana, eneo la Lizabon, Mtaa wa Kiblang'oma, baada ya kuvamiwa nyumbani kwao, majira ya usiku.

Wakati Jeshi la Polisi likiwataja watu 13, mmojawapo akiwa ni ndugu ya marehemu kuhusika na mauaji hayo, familia hiyo imeibuka na kudai kwamba, mtuhumiwa halisi ametoroshwa na askari wa jeshi hilo baada ya kukamatwa na kufikishwa kituoni.

Familia hiyo kupitia Matembo, inadai kuwa mtuhumiwa huyo waliyemtaja kwa jina moja la “Rasta”, amekuwa akionekana akitamba mitaani, lakini polisi hawamkamati ili kumfikisha mahakamani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Michael Kamuhanda, aliithibitishia NIPASHE Jumapili juu ya kutokea mauaji hayo pamoja na madai ya mtuhumiwa huyo kutoroka akiwa mikononi mwa polisi.

Kutokana na hilo, familia hiyo imemuomba Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha, na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, kuingilia kati suala hilo ili haki itendeke.

Matembo anasema wamefikia hatua hiyo baada ya kutafakari kwa kina jinsi polisi 'walivyowageuzia kibao' kwa kumkamata baba yake mzazi, Francis Matembo na mama yake mzazi, dada yake, Felister Matembo, kaka yake, Victory Matembo, Februari Mosi, mwaka jana na kuwashikilia kituoni kwa saa 14 mfululizo, kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 4 usiku.

Alisema yeye pia alikamatwa na polisi na kuwekwa gerezani pamoja na watuhumiwa wengine 10 kwa zaidi ya mwaka mmoja wakituhumiwa kuhusika na mauaji ya dada yake na mwanaye na kupora bunduki za polisi.

"kutokana na hayo, tumekubaliana kufufua hii kesi ili aliyetoroka, akamatwe. Kwa sababu amekuwa akionekana mitaani. Na wale, ambao niliowaripoti mwanzo, pia wakamatwe,” alisema Matembo alipozungumza katika ofisi za gazeti hili jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Alisema tayari wamekwishawasiliana na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kuomba msaada wa kisheria na pia hivi karibuni alifika makao makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kuonana na Kamishna Haule, ambaye alimuahidi kuwa atafuatilia malalamiko yao.

“Naomba sauti hii imfikie IGP Mwema na Waziri Nahodha kwani waliouawa ni binadamu. Pia nawaomba walinde usalama wangu. Nafahamu kwa kueleza ukweli huu, naweza kupata misukosuko na matatizo makubwa, ikiwamo kuuawa au kupewa kesi nisiyoifahamu, lakini siwezi kukaa kimya wakati damu ya dada yangu imemwagika. Narudia kumwomba IGP Mwema aliangalie kwa makini sana suala hili,” alisema Matembo, ambaye alijitambulisha kuwa marehemu Flora alikuwa ni dada yake.

Alisema baada ya dada yake na mpwa wake kuuawa kikatili, familia ilitoa taarifa ya tukio hilo katika Kituo Kikuu cha Polisi Songea kwa kuwaeleza wapelelezi, Abubakari na Suzan kwamba, kuna watu wanaowatuhumu kuhusika na mauaji ya ndugu zao, miongoni mwao akiwamo Rasta.

“Mpelelezi Abubakari alitushauri kuwa kwanza apatikane Rasta ndio watakamatwa watuhumiwa wengine. Tulikubaliana naye hilo kwa sababu hiyo ndiyo fani yake,” alisema Matembo. Alisema kwa kushirikiana na mdogo wake, ambaye ni askari wa Jeshi la Magereza, Joseph Matembo, Machi Mosi, mwaka jana, kati ya saa 2 na 3 asubuhi, walifanikiwa kumkamata Rasta na kumkabidhi kwa wapelelezi hao wawili katika Kituo Kikuu cha Polisi Songea.

Matembo alisema siku hiyo hiyo kati ya saa 7 na 8 mchana, walipigiwa simu na polisi wakitakiwa kwenda kituoni hapo. Alisema walipofika kituoni hapo walielezwa na mpelelezi Abubakari kuwa Rasta ametoroka kutokana na uzembe wa mpelelezi mwenzake, Suzan.

Matembo alisema baada ya taarifa hizo, Machi 4, mwaka jana, alikwenda ofisini kwa Kamanda Kamuhanda, na kumueleza kushangaza kwake na namna upelelezi wa kesi ya mauaji ya dada yake na mpwa wake unavyoendeshwa na polisi. Alisema baada ya kutoa kilio chake, Kamanda Kamuhanda alimueleza kuwa hata yeye hakufurahishwa na hilo.

Kutokana na hali hiyo, alisema Kamanda Kamuhanda alimweleza kuwa amewakamata askari waliohusika na uzembe huo na kuwaweka mahabusu.

Alisema Kamanda huyo alimhakikishia kuwa atakapowatoa mahabusu askari hao, atawapa muda wamtafute Rasta mpaka apatikane na wasipompata angewapa kesi hiyo ya mauaji au angewafukuza kazi.

Matembo alisema Machi 10-14, mwaka jana, mpelelezi Abubakari alimpigia simu na kumtaka aende kituo cha polisi.

Alisema alipofika kituoni, alikuta mpelelezi huyo akiwa amewakamata watu wawili, Frank Komba na Said Sandali, ambao wote ni wakazi wa Lizabon.

“Akaniuliza kama kati ya watu wale yupo Rasta aliyetoroka? Nikamjibu hayupo. Baada ya kukataa kumtambua Rasta kati ya watu wale wawili, aliniambia nimtaje mmojawapo kuwa ndiye Rasta ili wampe kesi ya mauaji yale kisha wapeleke taarifa kwa RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa) kuwa wameshampata Rasta kwani wasipofanya hivyo wanaweza kuharibu kibarua chao kwa kuwa RPC yuko serious (makini) sana na jambo hili. Nilikata nikaondoka,” alisema Matembo.

Alisema Machi 16, mwaka jana, alikamatwa na polisi, ambao walimweleza kuwa anahitajiwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa (RCO) wa Ruvuma, Naftali Nantamba, ofisini kwake. Matembo alisema aliwekwa ofisini kwa RCO huyo kuanzia saa 5 asubuhi hadi saa 2 usiku, baadaye aliondolea na kupelekwa mahabusu.

Alisema majira ya saa 5 usiku, alitolewa mahabusu na kupelekwa tena ofisini kwa RCO Naftali. Matembo alisema RCO huyo alianza kumkaripia kwa kumwambia kuwa anataka kuwaharibia kazi kwa kutumia jina la Rasta, bila kujua kwamba kipindi hicho polisi walikuwa wakihangaika kusaka bunduki zilizoporwa Songea kutoka mikononi mwa askari. “Akaniambia hiki kifo cha dada yako na mwanaye hata mimi nahusika na hata bunduki zetu zilizoporwa Songea, moja wameipata na nyingine mimi nitakuwa najua iliko,” alisema Matembo.

Alisema baada ya RCO Naftali kumueleza hayo, alirudishwa mahabusu, ambako alishikiliwa kwa siku 19 mfululizo, kuanzia Machi 16 hadi Aprili 8, mwaka jana.

Matembo alisema baadaye alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Songea, ambako aliunganishwa katika kesi ya watuhumiwa wengine kumi walioshtakiwa kwa kuhusika na mauaji hayo na kupora bunduki za polisi.

“Baada ya kusomewa mashtaka hayo, nilipelekwa gerezani Songea, ambako nilikaa hadi tarehe 29/11/2010. baadaye mimi na wenzangu tulifanya mgomo kushinikiza RPC Kamuhanda aje gerezani ili tujue hatima ya kesi yetu,” alisema Matembo. Alisema Desemba 3, mwaka jana, Kamuhanda akiongozana na RCO Naftali, walikwenda gerezani na kuwapa pole kwa mateso wanayoyapata.

Matembo alisema akiwa gerezani hapo, Kamuhanda aliwaeleza yeye na watuhumiwa wenzake kuwa aliwakamata kwa tuhuma za mauaji na kupora bunduki za polisi, lakini bunduki hizo zimepatikana na watu wawili wameuawa na polisi mjini Iringa na Makete.

Mbali na hilo, Matembo alisema Kamuhanda aliwaeleza pia kuwa kuna mtu waliyemkamata, ambaye walipomhoji alisema hafahamiani nao (Matembo na watuhumiwa wenzake).

Kutokana na hilo, alisema Kamanda Kamuhanda aliwaeleza kuwa hakuna kati yao hata mmoja mwenye makosa, hivyo lazima wangeachiwa. Alisema baada ya kuelezwa hivyo na Kamuhanda, waliendelea kukaa gerezani hadi Juni Mosi, mwaka huu, ambapo waliachiwa. NIPASHE Jumapili iliwasiliana na Kamanda Kamuhanda, kwanza alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na madai ya mtuhumiwa Rasta kutoroka.

Hata hivyo, alisema madai kuhusu Rasta, yamekuwa yakitolewa na Matembo na mdogo wake, askari Magereza na kusema: “Sisi kama Polisi, katika uchunguzi wetu hakuna Rasta.” Kamanda Kamuhanda alisema watuhumiwa wa mauaji hayo, wanaotambuliwa na polisi hadi sasa wako 13, mmojawao akiwa ni Matembo. Alisema watuhumiwa hao waliachiwa na mahakama kwa maombi ya wanasheria wa serikali.

Kamanda Kamuhanda alisema watuhumiwa hao waliachiwa kwa vile ushahidi uliopo kuhusu mauaji hayo, bado haujathibitishwa na watu, ambao bado wanatafutwa na polisi.

Alisema watuhumiwa hao wamewekwa na mahakama chini ya uangalizi wa polisi na kwamba, iwapo ushahidi utapatikana wanaweza kukamatwa na kurudishwa mahakamani.

Alisema watu wanaotafutwa na polisi kwa ajili ya ushahidi huo, walitoroka mjini Iringa na Makete na kwamba, wanatuhumiwa kuhusika na uporaji wa bunduki hizo, ambazo alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa zilitumiwa na mmoja wa watuhumiwa hao 13 wakati wa mauaji hayo.

“Hivyo, Stanley bado anaripoti polisi, uchunguzi unaendelea, kwani kesi iko mahakamani. Ushahidi ukipatikana wanaweza kurudishwa mahakamani,” alisema Kamanda Kamuhanda.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles