Tuesday May 3, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Samata, Ulimwengu watua, Stars yaitosa Misri

23rd May 2012
Print
Comments
Timu ya Soka ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars

Wakati kikosi cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kilichoitwa kujiandaa na mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Malawi itakayofanyika Jumamosi kimekamilika baada ya wachezaji wawili, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu, wanaocheza mpira wa kulipwa katika klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kujiunga na wenzao kambini tangu juzi usiku, timu hiyo imekataa ombi la kucheza mechi ya kirafiki dhidi Mafarao wa Misri, imefahamika.

Misri iliomba kucheza dhidi ya Stars jijini Cairo Mei 28 lakini Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na benchi la ufundi liliona kuwa Stars haitaweza kucheza mechi hiyo kwa sababu tayari ilikuwa imeialika Malawi hapa nchini.

Samata na Uliwengu jana jioni walifanya mazoezi ya pamoja na wachezaji wenzao chini ya kocha, Kim Poulsen.
Kiungo wa Simba, Haruna Moshi 'Boban', ambaye alikuwa amekwenda Kinshasa kwa ajili ya kumzika marehemu Patrick Mafisango, naye pia alirejea nchini juzi usiku na jana aliungana na wenzake kwenye mazoezi ya timu hiyo.

Akizungumza jana, Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alisema kuwa wachezaji wa timu hiyo wanaendelea na mazoezi na kuwasili kwa nyota hao pekee wanaocheza soka nje ya nchi walioitwa kikosini, kutampa nafasi Kim kuendelea na programu yake kikamilifu.

Wambura alisema kuwa baada ya mechi hiyo, Stars itaondoka nchini Mei 30 kuelekea Abdijan kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia Kanda ya Afrika hatua ya makundi dhidi ya wenyeji wao Ivory Coast itakayochezwa Juni 2.

Wakati huo huo, Wambura alisema kuwa Malawi pia itakwenda visiwani Zanzibar kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Zanzibar Heroes itakayofanyika Mei 28 mwaka huu kabla ya kuondoka Mei 30 mwaka huu kuelekea Kampala kuikabili Uganda Cranes katika mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia.

Awali, TFF iliichagua timu ya Simba kuivaa Malawi lakini baada ya wachezaji wake 11 kuitwa kwenye kikosi cha Stars, imebidi nafasi hiyo iende kwa timu ya Zanzibar Heroes.

Timu hiyo ya Zanzibar Heroes tayari iko kambini na mapema mwezi ujao itaelekea nchini Afghanistan kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia kwa nchi zisizo wanachama wa FIFA.


SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles