Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Upande wa pili wa Steven Charles Kanumba

11th April 2012
Print
Comments

Udongo wa ardhi ya manispaa ya Kinondoni  jijini Dar es Salaam, umeufunika mwili na kuhitimisha safari ya maisha ya msanii nguli wa filamu nchini, Steven Charles Kanumba.

Kijana aliyelitangaza jina la Tanzania nje ya mipaka ya nchi, tena kwa kutumia Kiswahili kilicho moja ya alama kuu za taifa hili, akitumia zaidi kipaji cha uigizaji kama silaha na rasilimali yake kuu, amelala katika usingizi wa milele-Mwenyezi ailaze roho yake mahali pema peponi-Amina.

Yapo mambo mengi yanazungumzwa na mengine yatazidi kuzungumzwa kumhusu Kanumba na mauti yaliyomkuta, lakini ukweli ni kwamba ‘amekwenda’. Hatutamuona muona tena akiigiza, akicheka, akitania, akila, akinywa na kufanya jambo lolote katika umbile la kibinadamu, bali kupitia picha alizoigiza, akiwa kivutio kwa kila aliyezitazama.

Jambo kubwa lililothibitishwa na na mamlaka tofauti likiwemo jeshi la polisi, ni kwamba kabla ya kufikwa na mauti, Kanumba alikuwa katika ugomwi na mpenzi wake.

Mpenzi huyo anatajwa kuwa ni Elizabeth Michael, binti ‘mchanga’ ambaye pia alikuwa akihudumu kupitia sanaa ya filamu nchini.

Kanumba amekwenda, lakini ukweli unabaki kwamba vijana wasanii wataendelea kushiriki na kuiendeleza fani hiyo. Hivyo, swali la kujiuliza ni kwamba, pamoja na kusononeka, kutokwa machozi na kuangua vilio, jamii inajifunza nini upande wa pili wa kifo cha Kanumba? Kanumba ametuachia nini?

Nilipopata taarifa za kifo cha Kanumba, kwamba kilitokana na ugomvi wa kimapenzi, nilikumbuka kifo cha mwanariadha nguli wa Kenya, Samwel Wanjiru kilichotokea Mei mwaka jana.

Wanjiru aliyekuwa mmoja wa vijana waliojikusanyai utajiri mkubwa kutokana na kushiriki kwake mbio za masafa marefu, alikuwa kijana wa kuigwa (kutokana na mafanikio yake) nchini Kenya.

Niliposikia kifo cha Kanumba, niliyaona mambo machache yanayofanana na ilivyomkuta Wanjiru. Mosi wote walikuwa vijana maarufu katika ukanda wa Afrika Mashariki, ingawa nyota ya Wanjiru iliwaka hadi nje ya mipaka ya Afrika aliposhiriki na kuishinda mbio kwa nyakati tofauti.

Wote wawili, Wanjiru na Kanumba walikuwa vijana, Wanjiru akifariki katika umri wa miaka 24 wakati Kanumba ametutoka akiwa na miaka 28. Wameondoka wakiwa na umri wa chini ya miaka 30.

Wote wamekufa kutokana na ugomwi unahusishwa na mapenzi, ingawa Wanjiru aligombana na mkewe wa ndoa, Triza Njeri, Kanumba amehusishwa na ugomvi na mpenzi wake, Elizabeth maarufu kama Lulu.

Wanjiru alifia nyumbani kwake, akisemekana kudondoka kutoka  ‘balcony’ ya nyumba yake iliyopo eneo la Nyahururu kule Nakuru, wakati Kanumba anasemekana kufariki baada ya kudondoka akiwa nyumbani kwake, Sinza-Vatican jijini Dar es Salaam.

Matumizi ya kileo yalihusishwa katika kifo cha Wanjiru, ambapo hapa nyumbani, zipo taarifa zinazotaja kileo katika kadhia ya kifo cha ‘kijana wetu’ Kanumba.

Wanjiru na Kanumba wanatofautiana kwa maeneo mengi vile vile, lakini ukweli ni kwamba wote wawili walikuwa kioo na mfano bora wa vijana, namna wanavyoweza kutumia vipaji na karama zao kujikwamua kimaisha.

Hivyo ndivyo nilivyokumbuka na kuwianisha vifo hivyo. Lakini kama nilivyoeleza awali, lazima maisha yatasonga mbele, vijana wataendelea kuigiza huku wakizitunza tunu bora zilizoachwa duniani na Kanumba.

Kwa mtazamo wangu vijana wanaokua, tena wakiwa katika sura ya kuwa ‘kioo’ cha jamii, wanahitaji kutunzwa katika malezi yatakayowafanya wamudu kuzikabili changamoto na misongo inayotokana na ujana.


Kwa maana Kanumba ameondoka, tena katika hali inayomhusisha na ugomvi dhidi ya mpenzi waliyekuwa wote katika tasnia moja. Ninaamini wapo wengi katika uigizaji wa filamu na nje ya hapo, wenye uhusiano wa kimapenzi.

Jamii inawaandaa ama kuwasaidia vipi katika kukabiliana na changamoto na misongo ya ujana, hasa wakati ambapo fani hiyo inazidi kukua, inawaingizia kipato na wanakuwa wenye kujulikana sana kwa umma?

Wadau wa tasnia ya filamu nchini na asasi nyingine za kijamii vikiwemo vyombo vya habari, wanawajibika kulitazama kundi hilo kwa namna ya pekee, kuwashirikisha ili waweze kuiona mipaka isiyo na mwisho ya thamani yao kwa jamii.

Ipo dhana iliyojengeka kwamba ‘kifo hakiepukiki’. Dhana hiyo inahitaji mjadala mpana, lakini kwa namna iwayo yote, ipo haja ya kushiriki kuziba mianya inayoweza kuibua matatizo yanayowakabili ‘vijana wetu’ wakiwemo wasanii wa michezo ya filamu na sanaa nyinginezo.

Inawezekana Kanumba ‘aliivishwa’ kiasi cha kuwa na uwezo wa kutambua thamani ya vipaji vyake, kwa maana kupitia uigizaji wake na namna alivyokuwa akihojiwa na vyombo vya habari, alionekana na kudhihirika alikuwa ‘kichwa’, kijana aliyetulia na mwenye maono chanya kwa jamii.

Lakini hata unapopita katikati ya watu waliowahi kukutana na Kanumba wakati wa uhai wake, wanasema hakuwa mtu wa majivuno, aliuishi ubinadamu na kwamba binadamu yoyote kwake kilikuwa kiumbe chenye maana kubwa sana.

Majirani zangu katika kitongoji cha Busaraga kule Kiabakari,wilaya mpya ya Butiama mkoani Mara, Makona George na Muhozi Magoma, walinipigia simu mara kadhaa, wakielezea kutoamini kwao kwamba Kanumba hayupo duniani.

Kutokana na ugumu wa maisha yaliyopo kijijini , walichangishana fedha ili waweze kunipigia simu mara kwa mara, wakitaka niwasaidie kuthibitisha taarifa walizokuwa wanazisikia kupitia vyombo vya habari, wakiamini kuwa Mwandishi wa Habari jijini Dar es Salaam kunatoa fursa ya kupata taarifa sahihi.

Huyo ni Kanumba aliyezigusa nyoyo za Watanzania wa vijijini na mijini, matajiri na masikini, wasomi na wasiosoma, wanawake kwa wanaumbe, wazee kwa watoto, wasichana kwa wavulana na taja kada nyingine yoyote kwenye jamii!

Upande wa kwanza wa maisha ya Kanumba umefungwa. Mwili wake umelala kaburini. Je, kurasa za upande wa pili wa maisha yake, unaihusisha vipi jamii wakiwemo vijana wasanii, kufuata nyayo njema za Steven Charles Kanumba. Zaidi ya yote kuzihimili na kuzikabili changamoto na misongo yenye athari kwa wanadamu?

Apumzike katika usingizi wa amani-AMINA

Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE. Anapatikana kwenye simu namba +255 754 691540, 0716635612 ama barua pepe: [email protected]

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles