Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Mkutano wa G8 umeipaiza Tanzania

20th May 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Rais Jakaya Kikwete mwishoni mwa wiki amekuwa mgeni maalum katika mkutano wa G8, nchi zilizoendelea kwa viwanda ambazo zilikuwa zinakutana mjini Washington, licha ya kuwa aliombwa kuhudhuria mkutano wa pembeni kuhusiana na tatizo la chakula barani Afrika.

Hapakuwa na shaka yoyote katika taarifa zilizosikika maeneo tofauti ya habari duniani, kuwa kati ya viongozi wachache wa Afrika waliokaribishwa, Rais Kikwete alikuwa na nafasi maalum. Ni hali ambayo viongozi wakuu wa nchi hii wamekuwa wakitambuliwa kimataifa, kutokana na uthabiti wa kisiasa na uwajibikaji wa serikali.

Suala lililokuwa linajadiliwa ni la umuhimu mkubwa, kwani nchi nyingi za Afrika hivi sasa zina uhaba wa chakula na kila mataifa makubwa hasa Ulaya na Marekani yanapoombwa kupeleka misaada inasuasua, mara nyingine mpaka ifikiwe hali ya janga, kama ilivyokuwa mwanzoni mwa mwaka huu nchini Somalia.

Yako maeneo mengine ambako hali ni mbaya ya upatikanaji wa chakula, kwa mfano Niger, lakini hadi sasa juhudi za kupata michango kuondoa tishio hilo imekuwa haba.

Hivyo ni muhimu kutafuta njia za kuzuia hali ya upatikanaji wa chakula isifikie mahali pabaya, na ndiyo sababu mkutano huo ukaitishwa.

Moja ya yale yaliyochangia Tanzania kupewa nafasi muhimu katika mkutano huo ni ufanisi katika kutumia fungu la misaada ya Marekani chini ya akaunti maalum ya malengo ya milenia (MCA). Ina maana kuwa kuna mazingira ya ushirikiano wa kina kati ya Marekani na Tanzania katika maeneo tofauti, ikiwemo suala la kilimo, licha ya kuwa zipo changamoto ambazo zinajitokeza.

Watanzania kwa jumla wamezoea mazingira ya ushirikiano ambako nchi za nje zinaweka fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi, hata ikiwa wana maofisa wao hapa, lakini wana mazoea haba ya kushirikiana na sekta binfasi.

Wazo hilo jipya linakumbusha mkutano wa Cancun mwaka 1983 nchini Mexico ambako Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere wakati huo alikaribishwa na viongozi wengine kadhaa wa nchi zinazoendelea, kuhusu suala hilo hilo la kuinua kilimo katika Afrika.

Wakati huo njaa kubwa iliyotokea Ethiopia mwaka1974 na kusababisha vifo vya maelfu ya watu na picha za kutisha ndege wala mizoga wakingoja mtu afe, aanze kuoza ndipo waanza kula zilisambazwa duniani kote. Rais Ronald Reagan akamwambia Mwalimu kuwa akitoa haki za ardhi, Marekani inaweza kutoa wakulima wanne wakazalisha chakula cha kutosha kwa nchi nzima.

Mwalimu na wenzake wa nchi zinazoendelea walikuwa wanataka ‘hali mpya ya uchumi duniani,’ ambao msingi wake ni kurekebisha mfumo wa biashara, na kutoa asilimia 0.7 ya mapato ya nchi zilizoendelea kusaidia maendeleo ya nchi changa, na Marekani ikakataa kabisa mawazo yote mawili.

Mkutano huu haukua unarudia yale ya 1983 kwani sasa hakuna tena suala la ‘hali mpya ya uchumi duniani,’ kwani dunia nzima inajua kuwa mfumo unaowezesha uchumi kufana ni ule wa soko. Kwa maana hiyo, Rais Obama yuko katika mwelekeo ule wa Rais Reagan kuhusu nafasi ya sekta binafsi, ila tofauti zimepungua.

Bado hakuna uhakika kama misingi ya ushirikiano huo iliwekwa wazi vya kutosha, kwani taarifa za vyombo vya habari vya kimataifa hazikueleza Marekani ilitaka Tanzania na nchi nyingine zinazotazamiwa kushiriki katika sehemu ya kwanza ya mpango huo wa usalama wa chakula zifanye nini ili sekta binafsi ya Marekani iweze kushiriki.

Hata hivyo, tunadhani si vigumu kubuni, kuwa hapa nchini kuwe na haki kamilifu za kilimo kuwa sehemu ya sekta binafsi, amana zake ziuzwe na kununuliwa. Nje ya hapo ni kutaka tu misaada.

Mkutano huo wa G8, ama kwa hakika umeipaiza Tanzania kutokana na ukweli kwamba uongozi wa Rais Kikwete umekuwa mfano wa kuigwa katika mikakati thabiti ya kuendeleza kilimo, sura inayojidhihirisha pia kimataifa.

Kwa mfano, Rais Kikwete ndiye aliyebuni na kuanzisha mpango wa miaka 14 wa Maendeleo ya sekta ya kilimo(ASDP). Mengi yamefanyika chini ya mpango huu ikiwa ni pamoja na wakulima kupata ruzuku na, mbolea na mahitaji mengine ya kilimo. Bajeti ya ruzuku imepanda kutoka sh. Bil saba mwaka 2005 na kufikia sh. Bil.121 kwa sasa. Hii ni hatua nzuri kwa serikali kutilia mkazo sekta ya kilimo na tunaipongeza sana.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles