Tuesday Jun 18, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Wachezaji Yanga kujazwa 'mapesa' Ijumaa

1st August 2012
Print
Comments
Wachezaji wa Yanga

Wachezaji  wa Yanga ambao walifanikiwa kutetea ubingwa wa mashindano yaliyomalizika Jumamosi ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) na kutwaa zawadi ya dola za Marekani 30,000 (Sh. milioni 45), watapewa sehemu ya fedha hizo keshokutwa ikiwa ni sehemu ya kuenzi jitihada walizoonyesha.

Yanga ilitetea ubingwa wake baada ya kuwafunga Azam magoli 2-0 na kurejesha furaha katika klabu hiyo ambayo ilishindwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu uliopita baada ya kupokwa taji hilo na mahasimu wao wa jadi, Simba.

Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa viongozi wa Yanga alisema kuwa hadi kufikia jana walikuwa bado hawajaafikiana ni kiasi gani cha fedha ambacho watawapatia wachezaji, lakini walishawaahidi kwamba watapatiwa mgawo huo baada ya kuanza mazoezi ya kujiandaa na msimu ujao wa ligi ifikapo keshokutwa Ijumaa.

Kiongozi huyo alisema kuwa licha ya kutofikia maamuzi, lakini sehemu kubwa ya fedha zinatarajiwa kwenda kwa wachezaji ambao walipigana kufa na kupona ili kuhakikisha kuwa kombe hilo linabaki mikononi mwao.

Wachezaji wa Yanga walipewa ruhusa na kocha wao, Mbelgiji Tom Saintfiet na wanatarajiwa kuanza kujinoa upya Ijumaa.

Kocha huyo ameeleza kwamba anataka kuona nyota wote waliosajiliwa wakifika katika mazoezi hayo na lengo ni kuhakikisha kwamba anawaandaa vyema wachezaji wake ili wafanye vizuri katika msimu ujao wa ligi ambayo itaanza kufanyika kwenye viwanja mbalimbali nchini kuanzia Septemba Mosi mwaka huu.

Saintfiet alieleza kuwa hataki kuona Yanga inaanza vibaya msimu mpya kama ilivyokuwa kwenye msimu uliopita na kupoteza ubingwa.

 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment