Sunday Feb 7, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Dk. Slaa ahimiza kuwepo haki, matumaini

17th April 2012
Print
Comments
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amesema kuzungumzia amani na utulivu majukwaani bila kwanza kudai kuwepo kwa haki na matumaini ya Watanzania ni kazi bure, akisema kukosekana kwa mambo hayo muhimu ndiyo chanzo cha migogoro inayoendelea kuliyumbisha taifa.

Akito kauli hiyo juzi katika mkutano wa hadhara mjini Shinyanga, Dkt. Slaa alimtaka Rais Jakaya Kikwete kukaa chini na kutafakari kwa makini juu ya migogoro mbalimbali inayolikumba taifa kwa sasa chini ya uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akisema mojawapo vya vyanzo vikubwa ni kukosekana kwa haki na wananchi kukosa matumaini kwa viongozi wao ambao badala ya kuongoza wamejigeuza kuwa watawala.

Kiongozi ambaye yuko katika ziara ya mikoa mitano, aliwaambia maelfu ya waliohudhuria wa mkutano huo, kuwa daima amani na utulivu ni tunda la haki na matumaini katika jamii.

“Suala la pili ndugu zangu nitasimama katika tamko letu ambalo tulilitoa mwanzo kabisa wa mwaka huu. Tulisema kwa mwaka huu kipuambele cha Chadema ni kujikita katika kutafuta viini au vyanzo vya matatizo yanayoikabili nchi kwa sasa, kijamii, kisiasa na kiuchumi. Taifa limekuwa la migogoro sasa, wananchi hawana matumaini kabisa.

“Namwambia Kikwete akae chini atafakari kwa nini sasa nchi inayumba, migogoro imejaa kila mahali, maandamano kila mahali…kama hajui basi atuite sisi tumsaidie hiyo kazi ya kutafakari na kuchukua hatua. Haki haionekani ikitendeka, wananchi wanasaka haki, hawana matumaini katika nchi yao. Hakuna amani kama hakuna haki,” alisema.

“Kuhubiri amani bila kuwepo kwa haki na matumaini miongoni mwa watu hawa ni sawa na kazi bure, nawaomba viongozi wangu wa dini zote, kuhubiri amani inayotokana na haki na matumaini.

Mwalimu Nyerere katika hotuba zake amewahi kusema msihubiri amani bila haki, haki ni matokeo au tunda la kuwepo kwa haki na matumaini, tunasema haya mapema wasiseme hatukuonya,” alisema Dkt. Slaa.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment