


.jpg)
Mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya timu ya soka ya taifa ya wanawake ya Tanzania (Twiga Stars) dhidi ya Zimbabwe iliyotarajiwa kufanyika kesho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam imefutwa kutokana na wageni hao kutoa taarifa za kutokuja tena nchini.
Uamuzi huo wa kutokuja nchini umefanywa na Chama cha Soka cha Zimbabwe (ZIFA) baada ya kupata mechi nyingine dhidi ya Zambia ambayo itachezwa Harare kesho.
Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema jana kuwa licha ya mchezo huo kutokuwepo kikosi cha Twiga Stars kinaendelea na mazoezi chini ya kocha wake Charles Boniface Mkwasa katika kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) iliyoko Ruvu mkoani Pwani na shirikisho linaendelea kuitafutia timu hiyo mchezo mwingine wa kujipima.
Wambura alisema wanaamini kwamba kupatikana kwa mechi ya kirafiki kutawaweka wachezaji wa Twiga Stars imara kwa mchezo wao wa awali wa kusaka tiketi ya kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake dhidi ya wenzao wa Ethiopia ambayo utafanyika Mei 26 mwaka huu jijini Addis Ababa na kurejeana hapa nchini baada ya wiki mbili.
Twiga Stars iliyoshiriki fainali zilizopita mwaka juzi ilifika hatua ya pili baada ya kuwaondoa Namibia mapema mwaka huu kwa kuwapa kichapo cha jumla cha magoli 7-2.