Friday May 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Wakuu wa Wilaya umma unataka uwajibikaji

11th May 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Uteuzi wa wakuu wa wilaya uliofanywa juzi na Rais Jakaya Kikwete ni kama kuhitimisha upangaji safu ya uongozi katika ng’we ya mwisho ya utawala wake wa miaka 10.

Katika uteuzi huo wa wakuu wa wilaya wa zamani 51 waliachwa na wapya 70 kuteuliwa katika jumla ya nafasi 133 za viongozi hao wa ngazi ya wilaya.

Uteuzi huu ni sehemu ya mtiririko wa viongozi wa kisiasa wa kuteuliwa kutoka waziri mkuu, mawaziri, naibu mawaziri, wakuu wa mikoa na sasa wakuu wa wilaya.

Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa kama hakuna dhoruba yoyote itakayokumba awamu ya nne ya uongozi, huu ni uteuzi wa mwisho mkubwa kufanywa na Rais Kikwete.

Tunajua uteuzi huu ulikuwa umesubiriwa kwa shauku kubwa na wengi, wapo waliokuwa wanalala na kusali kuwa wawe miongoni mwa watakaoteuliwa, lakini pia wapo waliokuwa wanaomba fulani na fulani asiwepo katika uteuzi mpya kwa sababu mbalimbali, nyingine zikiwa za kiutendaji au binafsi.

Kwa vyovyote itakavyotazamwa uteuzi umekwisha kufanywa na hao waliotangazwa ndio watakuwa wakuu wa wilaya walau hadi baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Tunachukua fursa hii kuwapa hongera wote walioteuliwa, tunawatakia kila la heri katika wajibu huo mpya wa kuwa wawalilishi wa serikali kuu katika ngazi ya wilaya.

Tunaamini watakuwa wawakilishi wema wa serikali kuu kwa njia ambayo watasaidia kuhamasisha shughuli za maendeleo katika maeneo yao, ili walau Watanzania wapige hatua za maendeleo katika kutokomeza adui mkubwa umasikini.

Kwa bahati nzuri kama wahenga walivyotuasa, kila zama ina kitabu chake, wakuu wa wilaya hawa wameteuliwa katika kipindi ambacho umma umeshuhudia moto wa uwajibikaji ndani ya serikali ukiwashwa na wawakilishi wa wananchi.

Ni katika kipindi ambacho mawaziri sita wamepoteza nafasi zao siyo kwa sababu nyingine yoyote ila ni kutokana na jinsi walivyotekeleza majukumu yao katika kusimamia matumizi ya fedha za umma kwenye maeneo yao na kutoa maamuzi ya kiuongozi kwa maeneo waliyoyasimamia.

Haya yalibainishwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2009/10, lakini pia yakapigiwa msumari na ripoti za kamati za kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC), Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), kisha Bunge likapitisha azimio la kutaka uwajibikaji kwa madudu yote yaliyotajwa kwenye ripoti hizo.

Ndiyo kusema wakuu wa wilaya walioteuliwa wanaingia katika ofisi za umma katika kipindi ambacho moto wa uwajibikaji uko juu sana, na kwa kweli wananchi wamefunguka macho wakitaraji matendo yanayodhihirisha uwajibikaji kutoka kwa wote wanaokalia ofisi za umma.

Kidogo kidogo hatua hizi zinaanza kuigeuza nchi yetu kutoka katika utamaduni mbaya wa kupeana vyeo kwa nia ya kupeana ulaji kuwa kupeana vyeo kwa nia ya kuwatumikia wananchi. Ni kipindi ambacho umma unataka kuona mabadiliko ya kiutendaji kwa wote walikabidhiwa ofisi za umma.

Tunafarijika uteuzi wa wakuu wa wilaya umetangazwa wakati kuna joto hilo la kudai uwajibikaji zaidi kutoka kwa viongozi wa umma, lakini pia katika kipindi ambacho mwamko wa kudadisi na kutathmini utendaji wa kila kiongozi unapewa nafasi kubwa sana katika harakati za kuendesha nchi.

Tunajua wakuu wa wilaya ni sehemu ya serikali kuu katika ngazi ya wilaya eneo ambalo hata hivyo kuna mfumo wa utawala wa serikali za mitaa kwa maana ya kuwako kwa halmshauri zinazoongozwa na madiwani waliochaguliwa na wananchi wa eneo husika, si matarajio yetu kwamba watakuwa chanzo cha mgongano baina yao na wananchi kupitia kwa madiwani wao kwa sababu tu ya kuvaa kofia ya uwakilishi wa rais au serikali kuu.

Ni matarajio yetu kuwa wakuu wa wilaya watajitahidi kadri wawezavyo kujivua ukereketwa na ukada wa chama tawala na kuwa watumishi wa umma wasiofungamana na chama chochote ili kuwa nguzo kuu ya kuhamasisha uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali za umma kwa maendeleo ya wote.

Wakuu wa wilaya wakumbuke wakati wote kuwa zama za kupewa dhamana na kuzigeuza vichaka vya kula raha bila uwajibikaji zimepita, tena zimepita kwa kasi kubwa.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles