Sunday May 26, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Kim amuonya Samatta

14th June 2012
Print
Comments
Mbwana Samatta

Kocha wa timu ya taifa ya soka (Taifa Stars), Kim Poulsen amemtaka nyota wake, Mbwana Samatta aache tabia ya kukaa na mpira kwa muda mrefu na pia akawataka washambuliji wengine kuongeza umakini mbele ya lango la wapinzani ili wafunge mabao na kuipa mafanikio timu yao.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana kuhusiana na maandalizi yao kabla hawajaondoka kesho kwenda kucheza na Msumbiji katika mechi ya marudiano ya kuwania kufuzu kwa fainali za mwakani za Kombe la Mataifa ya Afrika(AFCON 2013), Kim alisema kuwa anachotaka kukiona katika mechi ijayo ni kwa washambuliaji wake kufunga mabao.

Alisema kuwa kutokana na dhamira yao ya kushinda Msumbiji, ameamua kuwapa 'dozi' ya ziada ya mazoezi wachezaji wake wote wa safu ya ushambuliaji ili watimize wajibu wao wa kupachika mabao.

"Tunahitaji kufunga ili tushinde," alisema kocha huyo ambaye tayari ameiongoza Stars katika mechi tatu, ambazo ni ile iliyomalizika kwa sare ya 0-0 dhidi ya Malawi, waliyolala ugenini kwa mabao 2-0 dhidi ya Ivory Coast na ya wiki iliyopita dhidi ya Gambia ambayo walishinda 2-1 kutokana na mabao yalifungwa na mabeki Shomari Kapombe na Erasto Nyoni.

Akieleza zaidi, Kim alisema kuwa amemtaka Samatta anayeichezea klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo atoe pasi kila mara anapoona kuwa hayuko kwenye nafasi nzuri ya kufunga, huku akimsifu kiungo-mshambuliaji Haruna Moshi 'Boban' kwa kuwa mwepesi wa kutoa pasi kwa wenzake.

"Nimemwambia (Samatta) hayuko uwanjani peke yake, anapokuwa amebanwa atoe pasi haraka, arahisishe kazi na kuacha kuzunguka uwanja," aliongeza Kim; akirejea rai aliyowahi kuitoa mtangulizi wake Jan Poulsen, ambaye baadaye alikwenda mbali zaidi kwa kumuacha Samatta nje ya kikosi chake kwa madai kuwa hachezi kwa ushirikiano na wenzake.

Hata hivyo, Samatta ni miongoni mwa nyota waliong'ara katika mechi dhidi ya Gambia iliyokuwa ya Kundi C la kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia ambapo chenga zake kali zilimbwaga sakafuni beki mmoja kabla hajapiga krosi iliyozuiwa kwa mkono na beki mwingine na kuzaa penati iliyowekwa wavuni na Nyoni.

Samatta ambaye pia ni mchezaji wa kutegemewa wa Mazembe,  hakuwemo katika mechi ya awali ya Stars ya Jan Poulsen dhidi ya Msumbiji iliyochezwa Februari 29 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na timu hizo kutoka sare ya 1-1.

CHOLO, MWADINI

Kikosi cha Stars kitaondoka nchini kesho alfajiri kikiwa na wachezaji 20 huku Nassor Masoud 'Chol'o, Waziri Salum na Mwadini Ali wakiachwa kutokana na kuwa majeruhi.

Kim alisema kuwa licha ya kutarajia ushindani mkali katika mechi hiyo itakayochezwa Jumapili mjini Maputo, anaamini kuwa watafanya vizuri kwani ndoto yake ni kuona wanafuzu kwa fainali za AFCON na katika soka lolote huweza kutokea.

Aliongeza kuwa wachezaji wake wako tayari kwa mechi hiyo na amefurahi kufanya mazoezi kwenye uwanja wa nyasi halisi kama watakazokutana nazo Msumbiji.

Stars itarudi nchini Jumanne ambapo wachezaji watarejea kwenye timu zao kuanza maandalizi ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame).




 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment