Thursday May 5, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Wachumaji karafuu kuanza kulipwa fidia

17th April 2012
Print
Comments
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, amesema serikali imeamua kuanza kuwalipa fidia wachumaji wa zao la karafuu wanaoathirika na zoezi hilo wakiwemo wale wanaoanguka na kusababisha madhara ya viungo na wengine kupoteza maisha yao.

Uamuzi huo aliutangaza jana alipokuwa akizungumza na Kamati ya kikosi kazi ya kitaifa ya uokoaji wa zao la karafuu na kupambana na biashara ya magendo, katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi wilayani Wete kisiwani Pemba.

Dk.Shein alisema tangu kuanza kwa zoezi la uchumaji, Julai, mwaka jana, kesi 114 zimeripotiwa na mtu mmoja kupoteza maisha kutokana na kuanguka katika miti ya mikarafuu na kuwasababishia maumivu ya viungo vya miili yao.

Alisema serikali imeamua kuanzisha mfuko wa maendeleo wa zao la karafuu, na tayari sheria hiyo imeshapitishwa katika Baraza la Wawakilishi ambayo italiwezesha Shirika la Biashara Zanzibar (ZSTC), kuanzisha mfuko huo wenye lengo la kuendeleza zao la karafuu na kusaidia wakulima wa zao hilo.

Dk.Shein aliongeza kuwa tangu kuundwa kwa kamati hiyo, mafanikio makubwa yamepatikana katika suala zima la kuzuia magendo, ambapo yeye mwenyewe amefuatilia kwa karibu katika nchi jirani inayonunua zao hilo, na kubaini kuwa biashara hiyo imedhibitiwa kwa kiwango kikubwa.

Awali, Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Ahmed Nassor Mazrui, alisema serikali imefanikiwa kuokoa idadi kubwa ya karafuu ambazo zilikuwa zisafirishwe kwa njia ya magendo, kutokana na uamuzi wake wa kupandisha bei ya zao hilo kutoka Sh. 3,500 hadi 15,000 kwa kilo moja.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles