Sunday May 1, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Safari ya Simba Sudan yajaa nuksi

11th May 2012
Print
Comments
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage

Simba juzi usiku ilitua salama Khartoum lakini jana ilishindwa kuanza safari ya kuelekea kwenye mji wa Shendi ulioko Kaskazini mwa Sudan kutokana na wenyeji wao kutotokea na kuwaongoza kwenye safari hiyo, huku wakiacha kwenda wenyewe kwa hofu ya usalama.

Awali Simba, ambao walisota kwa zaidi ya saa moja kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam kutokana na kuchelewa kwa ndege yao, waligandishwa tena kwa saa mbili kwenye uwanja wa ndege wa Khartoum huku mwenyeji wao aliyefika kuwapokea kutoka katika Chama Cha Soka cha Sudan (SFA) akidai kwamba alikuwa akikamilisha taratibu za kiusalama kabla ya kuondoka uwanjani hapo.

Jana wachezaji na viongozi wa Simba walikaa kwa zaidi ya saa tano hotelini na wenyeji hao ambao walikuwa wameahidi kuwapeleka mji wa Shendi hawakutokea kama walivyokubaliana kwamba safari hiyo ingeanza saa tatu asubuhi.

Hadi kufikia saa nane mchana, hapakuwepo na basi lolote au mwakilishi yeyote wa kutoka Shendi au SFA aliyekwenda kwenye Hoteli ya Safiga ilikofikia Simba na kwa mujibu wa mawasiliano, walidai kwamba wamekwama kwenye foleni.

Hali hiyo ilisababisha wachezaji na viongozi wa Simba kushinda nje ya hoteli hiyo wakiwa wamekaa nje kwenye viti vichache, huku wengine wakiwa wamesimama tu kwa muda wa zaidi ya saa mbili kwa vile muda wa kutoka hotelini ulikuwa umepita.

Kwa mujibu wa kanuni ya 14 (b) ya mashindano yanayosimamiwa na CAF, timu yeyote inatarajiwa kusafirishwa kutoka eneo moja kwenda jingine katika muda ambao unakubalika, labda kama imechelewa yenyewe.

Kuna umbali wa kilomita 150 kutoka mji mkuu wa Sudan, Khartoum iliko Simba hadi mji wa Shendi na kama Simba itachelewa kuondoka jijini hapa, maana yake ni kwamba itashindwa kufanya mazoezi leo jioni na hivyo Shendi na SFA wamekiuka kanuni hiyo.

Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, alieleza kuchukizwa kwake na tukio hilo akisema linaonyesha namna Shendi na SFA walivyojipanga kutumia mbinu za nje ya uwanja kushinda pambano hilo la marudiano.

“Sisi tulitarajia kukumbana na yote haya ambayo tunayaona sasa. Wanajua kwamba hawataweza kuishinda Simba ndani ya uwanja na hivyo wameamua kutumia mbinu chafu," alisema Rage.

Daktari wa Simba, Cosmas Kapinga, alisema inachofanyiwa Simba ni kitu ambacho kwa kitaalamu kinaitwa uchoshwaji wa kisaikolojia, lengo lake likiwa kuiathiri timu kiakili lakini tayari walishawaandaa wachezaji wao kwa hali hiyo.

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' alisema kwamba wachezaji wote wako salama na wamejiandaa kupambana na 'fitna' kutoka kwa wenyeji wao hazitawakatisha tamaa.

Kaburu alisema kuwa wachezaji wanasikia joto lakini bado hali hiyo haijawasumbua sana kwa sababu wengi wameshaizoea hewa hiyo wakiwa jijini Dar es Salaam.

"Na kwa sababu mechi itachezwa usiku kwetu itakuwa ni nafuu kwa sababu muda huo joto hupungua," alisema.

Wakiwa Khartoum msafara wa Simba ulioko chini ya Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Nchini (TFF), Hussein Mwamba, ulifikia katika hoteli ya Shariqa na mechi yao ya keshokutwa itachezwa kwenye Uwanja wa Shendi wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 10,000.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles