Sunday May 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

CUF: Serikali iunde timu maalum ya uokoaji

21st July 2012
Print
Comments

Kufuatia ajali ya kuzama kwa meli ya Mv. Skagit iliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 100, Chama cha Wananchi (CUF), kimeitaka serikali kuviangalia vyombo vyake vya uokoaji ikiwa ni pamoja na kuvipatia mafunzo na zana za kisasa za uokoaji.

Aidha, CUF imeitaka serikali kuangalia uwajibikaji, utendaji na mwenendo mzima wa Mamlaka ya Udhibiti  wa Usafiri wa Nchikavu na Majini (Sumatra) kutokana na kitendo chake cha kushindwa kuwajibika ipasavyo pindi matukio yanapotokea.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Profesa Ibrahimu Lipumba, alisema CUF imepokea kwa masikitiko ajali hiyo iliyotokea Jumatano ya wiki hii katika bahari ya Hindi.

Profesa Lipumba alisema serikali inapaswa kufuatilia na kuhakikisha kuwa vyombo vyote vinabeba abiria na mizigo kulingana na uwezo wa ujazo wa chombo husika.

“Tunapendekeza serikali iunde kikosi maalum cha uokoaji  pia kuwepo na kamanda wa pamoja atakayesimamia na kuratibu vikosi vyote vitakavyoshiriki vikiongozwa na wataalam wa maafa na uokoaji, lakini kuwepo na vyombo vya uokoaji ambavyo muda wote vinakuwa tayari badala ya sasa tunaambiwa ajali imetokea lakini havikuwa na mafuta,” alisema.

Aliongeza kuwa, serikali inatakiwa kuwa na meli ambazo zitaendeshwa kibiashara ili zisiwe na gharama kwenye bajeti ya serikali ambapo faida yake itatumika kwa manunuzi ya meli nyingine.

Profesa Lipumba alisema licha ya Makamu wa pili wa Rais Zanzibar awali kuwahakikishia Wazanzibar kuwa, ajali ya Mv. Spice Islander iliyotokea miezi tisa iliyopita na kuuwa watu zaidi ya 941, kuwa tukio kama hilo halitatokea tena lakini mpaka sasa serikali haijajipanga kwenye shughuli ya uokoaji.

“Ofisi hii ya makamu wa pili wa Rais inatakiwa kuwajibika, naamini wahusika wanatakiwa kuwajibika kisiasa ili kumpa nafasi Rais kufanya kazi zake badala ya kuwepo kwa malumbano yasiyo na msingi” alisema.

Pia alisema ni muhimu kuhakikisha kunakuwepo na mawasiliano kati ya kituo cha hali ya hewa na chombo cha kusimamia usafiri ili tahadhari ziweze kuchukuliwa mapema inapotokea mabadiliko ya hali ya hewa.

Profesa Lipumba alisema nchi ina mapungufu katika kitengo cha Tiafa cha uokoaji na kwamba hawana vituo vya uhakika vya shughuli hiyo.

Alisema kutokana na upungufu huo, nchi imekuwa ikitegemea kuomba misaada ya uokoaji na zana kutoka nchi ya Afrika Kusini kama ilivyofanyika ilipozama meli ya Mv. Bukoba mwaka 2006 na Mv. Spice Islander mwaka huu.

Pia chama hicho kimeonyesha wasiwasi wake kwa manahodha na mabaharia pamoja na uwezo walionao katika kujua uwezo wa chombo kama kinaweza kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

“Hata Sumatra pamoja na wakala wa Meli Zanzibar (ZMA) haina sifa sahihi za manahodha na mabaharia hawa, pia hakuna uhakiki ikiwemo kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa usalama wa chombo cha abiria,” alisema.

Profesa Lipumba alisema kuwa, licha ya kuwepo kwa vikosi zaidi ya vitatu vya uokoaji kama Kikosi cha Wanamaji cha JWTZ (Navy), jeshi la polisi (Marine Police), na KMKM lakini vyote havikufika mapema wala kuwa na uwezo wa kuokoa abiria.

“Kikosi cha JWTZ kilipaswa kuwa na jukumu la uokoaji wa meli hii lakini hata hivyo halikufanyika mapema kutokana na  kutokuwepo na  vifaa vya kutosha  pamoja na kikosi imara cha dharura, ndio maana CUF tunataka kiundwe,” alisema.

Aidha, alisema awali Mkaguzi wa Dar es Salaam Institute alikikagua chombo hicho wakati kinafanya shughuli zake za usafirishaji abiria kutoka Zanzibar kuelekea Pemba baada ya kuonekana kinayumba .

Alisema baada ya ukaguzi huo, boti hiyo ilihamishwa safari zake na kuanza kutoa huduma Dar es Salaam kuelekea Zanzibar.

"Ninachokiona hapa ni kwamba tunatatizo la ukaguzi wa vyombo vivavyotoa huduma majini, hili ni tatizo linapaswa kuangaliwa upya," alisema.




 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment