Sunday May 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Spika makinda akemea vyombo vya habari

30th June 2012
Print
Comments
Spika wa Bunge, Anne Makinda

Spika wa Bunge, Anne Makinda, amevikemea vyombo vya habari vinavyomshutumu kupendelea Chama cha Mapinduzi (CCM), wakati wa uendeshaji wa shughuli za Bunge.

Aliyasema hayo mara baada ya kutangaza matangazo ya wageni bungeni jana.

Spika alisema amekuwa akiendesha Bunge kwa mujibu wa kanuni na si kufikiri.

Aliwasisitiza  waandishi wa habari kusoma kanuni za Bunge, ili waweze kuzijua na hivyo kuepuka kujenga chuki miongoni mwa jamii.

Wakati Spika akivilaumu vyombo vya habari naye Mbunge wa Korogwe Vijiji  (CCM), Stephen Ngonyani, maarufu kama Maji Marefu, alieleza masikitiko yake kuhusiana na kunukuliwa vibaya na baadhi ya vyombo vya habari (sio NIPASHE).

Ngonyani akiongea kwa masikitiko, alisema kuwa alinukuliwa vibaya kuhusiana na mgomo wa madaktari ambapo ilielezwa kufurahia kutekwa na kujeruhiwa kwa kiongozi wa mgomo wa madaktari.

“Mimi nilitibiwa kwa muda wa wiki tatu kabla kuandikiwa na hao hao kwenda India kwa ajili ya matibabu zaidi... Na pia madaktari bingwa masaa 24 walikuwa wakipokezana kuja kunihudumia, leo hii nifurahie kutekwa na kupigwa kwa Dk. Ulimboka, jambo hili limenifedhehesha na kuniuzunisha sana,”alisema.

Alisema hata angekuwa ni kichaa asingeweza kamwe kufurahia tukio hilo, kwa kuwa madaktari ndio wanaowahudumia  watu wote.

Alisema yeye ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, iliyotumwa na Bunge kwenda kuchunguza sakata la mgomo uliopita na walifanya kazi hiyo kwa ushirikiano mkubwa na Dk. Ulimboka.

“Dk. Ulimboka ni mmoja wa watu ambao walitusaidia kwa kiasi kikubwa katika kutupa taarifa kuhusiana na mgomo wa madaktari na tukamuelewa…leo hii hata wananchi wa jimbo langu watakosa imani kwangu kwasababu katika maisha yao ya kila siku wanategemea huduma za madaktari,”alisema na kuongeza:

‘’Habari hizi zimenidhoofisha na nimejisikia vibaya sana…Ninaomba msamaha kwa Dk. Ulimboka kwa taarifa hiyo na ninamuomba Mwenyezi Mungu amponye haraka.”
 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment