Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Hazina ya gesi iwe neema siyo laana

3rd August 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Akihutubia Taifa juzi Rais Jakaya Kikwete alisema kuwa pamoja na neema kubwa ya kuvumbuliwa kwa hazina kubwa ya gesi asilia nchini inayokadiriwa kufikia futi za ujazo trilioni 28.9, kuna changamoto nyingi za kukabiliana nazo ili nchi inufaike na rasilimali hiyo.

Alisema kuwa pamoja na faida nyingi za matumzi ya gesi, kama vile uzalishaji wa mbolea kwa ajili ya kilimo; uzalishaji wa umeme, nishati kwenye viwanda, magari na majumbani, ili kufikia manufaa hayo taifa ni lazima lijipange kimkakati kwa kuwa na mifumo, sera, sheria na wataalam wa kusaidia kufikiwa kwa matarajio hayo.

Katika hotuba hiyo iliyorushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni, Rais alikumbusha kuwa kuna nchi kadhaa ambazo hazina kubwa ya gesi na mafuta imegundulika lakini badala ya kuwa neema kwa watu wake imekuwa laana.
Zipo nchi zenye neema hiyo lakini bado mafuta wala umeme haupatikani kwa watu wake, kibaya zaidi hata umasikini wa watu wake ni mkubwa kama nchi ambazo hazijajaliwa kabisa rasilimali kama hizo.

Kwa maana hiyo, ili taifa linufaike Rais alisema kuwa jambo la umuhimu wa kipekee ni kujipanga kimfumo kuwa na wataalam, lakini zaidi sana kusimamia kwa karibu mapato yatokanayo na gesi ili yasaidie kubadili hali ya umasikini katika nchi.

Tunasema kuwa kauli ya Rais juu ya kugundulika kwa hazina kubwa ya gesi nchini ambako visima 22 kati ya 61 vilivyochimbwa na kufanyiwa utafiti vimegundulika kuwa na hazina hiyo, 14 vikiwa nchi kavu na 8 baharini kwenye kina kirefu, na mikakati ambayo serikali inakusudia kuchukuwa ni ya kutia moyo.

Nasi tunamuunga mkono Rais katika hili kwa maana moja kubwa; kwamba kama taifa kama hatutajipanga ni kweli tupu neema hii haitakuwa na maana yoyote kwa watu wetu kwa ngazi ya mtu mmoja mmoja lakini hata na taifa kwa ujumla wake.

Tunasema hivyo kwa sababu duniani kote kazi ya uchimbaji mafuta na gesi pamoja na madini imekuwa ni shughuli ya kampuni kubwa zenye nguvu kubwa ya kimitaji na tekinolojia; kwa maana hiyo huingia mikataba na mataifa ambako hazina hiyo hugundulika ili shughuli ya uchimbaji iendelee.

Ni katika mikataba hiyo taifa hujikuta ama kubakia na ukiwa na umasikini wake au kubadilika kwa kufaidi rasilimali hizo. Nchi hubakia na ukiwa kama mikataba hiyo inaegemea kunufaisha kampuni za uchimbaji ama kutokana na kufungwa katika vipengele vya kupendelea kampuni hizo kwa hali ya uficho au dhahiri shahiri; lakini pia inawezekana kuwa na neema kwa taifa na watu wake kama mikataba hiyo inazingatia maslahi ya taifa kwa kuhakikisha kuwa vipengele vya mikataba vinalinda haki yao ili  kunufaika na rasilimali hiyo. 

Tunapenda kueleza bayana kuwa uzoefu wa taifa hili katika mikataba ya madini kwenye migodi mikubwa siyo kitu cha kufarahisha sana, malalamiko ambayo yaliibuliwa na wananchi kwa kipindi kirefu yalionyesha wazi kuwa katika kuingia mikataba hiyo kwa kiwango fulani maslahi ya taifa hayakuzingatiwa.

Ni baada ya mapambano na harakati nyingi sheria zilibadilishwa na baadhi ya mikataba kubadilishwa ili walau taifa linufaike na rasilimali hiyo. Hatua zimechukuliwa.

Kwa maana hiyo, tungependa kuona uzefu huo ukituongoza ili kweli mikataba yote ya uchimbaji wa gesi iwe na manufaa kwa taifa; juhudi zaidi zielekezwe kufundisha Watanzania katika fani mbalimbali zinazosimamia shughuli ya uchimbaji wa gesi katika eneo la sheria na mikataba; uhasibu na ukaguzi, uchumi, biashara na masoko; uhandisi na ufundi; kwa nia ya kupata nguvu kazi ya Kitanzania inayoelewa sekta hiyo kwa mapana yake.

Tungependa Watanzania watambue kwamba kugundulika kwa kiasi kikubwa cha gesi nchini hakutupi nafasi ya kutulia na kula raha, ila wajibu unaongezeka, tunatakiwa kufanya kazi kwa bidii zaidi, kusimamia kwa umakini zaidi sekta hiyo, na kwa ujumla kuwa makini kadri iwezekanavyo ili uchimbaji wake uwe na maana kwa taifa hili kuanzia kwa kizazi cha sasa na kijacho.

 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment