Sunday May 1, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Polisi yazuia mikutano ya Chadema Iringa

19th May 2012
Print
Comments

Jeshi la Polisi, limezuia kufanyika kwa mikutano ya aina yoyote ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Wilaya ya Iringa kutokana na hali ya utulivu katika mji huo kutoridhisha kwa sasa.

Jana, chama hicho kilitangaza kufanyika kwa maandamano makubwa pamoja na mikutano ya hadhara katika viwanja vya Mwembetogwa na Nduli katika Manispaa ya Iringa, kwa nia ya kulaani vitisho na hujuma vinavyofanywa na watu wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Uamuzi huo, umefikiwa na jeshi hilo baada ya kuwapo kwa madai ya kutishiwa kuuawa kwa Mbunge wa Jimbo hilo la Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa na Diwani wa Kata ya Mivinjeni, Frank Nyalusi.

Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na jeshi hilo na kusainiwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), Mohamed Semunyu, kwenda kwa Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Susan Mgonakulima, inaeleza wazi kwamba hali ya utulivu katika Manispaa hiyo kwa sasa si ya kuridhisha.

Katika sehemu ya barua hiyo yenye kumbukumbu namba IRIA.23/14/VOL.XII/213 ya Mei 16,  mwaka huu ambayo nakala yake imepelekwa kwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa (Evarist Mangalla), inasema kuwa kutokana na hali ya utulivu kutoridhisha, mikutano yote ya chama hicho imesitishwa hadi hapo kutakapokuwa na hali ya utulivu.

Hata hivyo, katika mkutano wake na Waandishi wa Habari, Katibu wa Chama hicho, Susan Mgonakulima alisema licha ya jeshi la Polisi kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wanne wa vurugu zilizotokea Mei 13 katika Kijiji cha Nduli pamoja na kumburuza kortini Diwani wa CCM Kata ya Nduli, Idd Chonanga (65) kwa kutishia kumuua mbunge na Diwani wa chama hicho,

Chadema kimeingiwa na mashaka makubwa kwa sababu Chama cha Mapinduzi, viongozi wa serikali akiwamo Mkuu wa mkoa huo Dk. Christine Ishengoma na hata uongozi wa Wilaya, umeshindwa kukemea vitendo hivyo vya uvunjifu wa amani.

“Tuna mashaka makubwa na hali ilivyo kwa kuwa serikali yetu haijatoa tamko lolote hasa ukizingatia kuwa viongozi wa Serikali wana wajibu wa kujenga na kuendeleza demokrasia katika maeneo yao. Chadema ni watu tunaoheshimu utawala wa sheria,” alisema Mgonakulima.


SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles