Tuesday May 3, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Walimu watingisha kibiriti

21st May 2012
Print
Comments
Naibu Waziri wa wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Phillipo Mulogo

Walimu nchini wamepuuza madai yaliyotolewa na Naibu Waziri wa wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Phillipo Mulogo kwamba wamechakachua madai yao na kusisitiza kuwa wanataka nyongeza ya mshahara kwa asilimia 100, posho ya kufundishia na ya mazingira magumu ya kazi.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba alisema walimu wamechoka kunyanyaswa na kwamba safari hii watagoma hadi madai yao yafanyiwekazi.

Mukoba alisema fedha za madai yao zilikwatolewa tangu Januari mwaka huu na kupelekwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi nyingine Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) lakini cha kushangaza hadi leo walimu hawajalipwa.

Alisema mbali ya madai hayo ya muda mrefu, safari hii walimu wanalenga kushinikiza nyongeza ya mshahara kwa asilimia 100, asilimia 30 ya posho ya mazingira magumu kazini na asilimia 50 hadi 55 ya posho kwa walimu wa sanaa na sayansi.

Alisema serikali inao uwezo wa kuwalipa walimu fedha hizo hivyo hakuna sababu ya kutoyatekeleza.
"Tutafanya hekaheka ambayo haijawahi kutokea, tunawasilisha madai yetu haya mapema kabisa ili serikali inapoandaa bajeti iyafanyiekazi," alisema Mukoba.

Mukoba alisema serikali imekuwa ikiongeza mishahara na posho mbalimbali kwa kada lakini walimu hawafanyiwi hivyo jambo ambalo alisema hawawezi kuendelea kulikubali.

"Mwaka 2007 Serikali iliongeza mishahara ya madaktari na sasa hivi tena inataka kuiongeza sisi hatuna shida na hilo tunachotaka ni nyongeza, kama itaona haina fedha basi wasitishe kuwaongezea madaktari ili ituongezee sisi kwa sababu ni mwaka 2007 tu imewapa nyongeza," alisema.

Akizungumza juzi, Mulugo alisema Serikali imeokoa zaidi ya Sh. milioni 400 zikiwa ni madai hewa yaliyokuwa yamewasilishwa kwa ajili ya kulipa stahili mbalimbali za walimu.

Alisema fedha hizo zimeokolewa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kufuatia uhakiki wa vielelezo vya madai uliofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa serikali anayechunguza, kuhakiki na kuidhinisha stahili za wanaoidai.

Ijumaa iliyopita walimu walitangaza mgogoro na serikali wakiitaka ndani ya wiki mbili iwe imewalipa madai ya Sh. bilioni 13 na pia kuwapa nyongeza ya mshahara kwa asilimia 100 utakaolipwa kuanzia Julai, mwaka huu.

Waziri Mulogo, alifafanua kuwa fedha za walimu zinalipwa kila wakati na uhakiki umewezesha kuokoa kiasi hicho cha fedha ambacho kingeishia mikononi kwa wadai hewa.

Katika utetezi wake, alisema kinachochelewesha malipo ni uhakiki kwani baadhi ya viambatanisho vinavyotolewa si sahihi, vingine vina upungufu, wengine hawana vithibitisho na wakati mwingine wasio waadilifu wanawasilisha madai zaidi ya mara mbili.

Alitoa mfano kuwa mwaka 2009 malipo yalipoanza kutolewa baadhi ya walimu walilipwa lakini waliposikia suala la kulipwa mafao waliwasilisha madai ambayo kama yasingehakikiwa Serikali ingepata hasara kwa kulipa madai hewa.
 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles