Thursday May 23, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Wabunge mmesikia uoza huu, uwafunue mjadala wa bajeti

14th June 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Jana vyombo vingi vya habari viliandika kwa kina habari za misamaha ya kodi inayotolewa na serikali ikielezwa kuwa katika mwaka wa fedha wa 2009/10 kiasi cha Sh. trilioni 1.59 zilipotea katika mwanya huo, huku serikali ikiendelea kulalama kuwa haina fedha za kutosha kugharimia huduma muhimu za kijamii kama elimu, afya na hata ujenzi wa miundombinu.

Taarifa hizo zinatokana na ripoti ya utafiti uliofanywa na Kamati ya Viongozi wa Dini ya Haki za Kijamii, Uchumi na Hifadhi ya Uumbaji ambayo ilibainisha kuwa kuna misamaha mingi ya kodi ambayo kimsingi haimnufaishi mwananchi na kwamba wakati sasa umefika kwa serikali kutafakari kwa kina faida ya misamaha hiyo ambayo imekuwa ikitolewa kila mwaka aghalab kwa makampuni makubwa yenye mitaji mikubwa katika uwekezaji.

Taarifa hii inatolewa wakati macho na masikio ya Watanzania yakiwa yameelekezwa Dodoma kusubiri bajeti ya serikali ya mwaka 2012/13 itakayowasilishwa leo saa 10 jioni na Waziri wa Fedha.

Taarifa hiyo inasema wazi kuwa mbali na misamaha hiyo pia kuna ukwepaji wa kulipa kodi na utoroshwaji wa mali nje ya nji kwa mbinu mbalimbali ambazo zinaacha taifa katika umasikini na watu wake kushindwa kunufaika na rasilimali walizojaliwa na Muumba.

Ripoti hii inaongeza msumari juu ya kidonda kilichofunuliwa na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha wa 2009/10 ambayo ilisababisha kuwashwa kwa moto mkubwa bungeni katika mkutano wa saba, huku ikiungwa mkono na ripoti tatu za Kamati za Kudumu za Bunge, Hesabu za Serikali (PAC), Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), zikisisitiza kile kile alichozungumza CAG.

Hakuna ubishi kuwa kiasi hicho cha fedha ni kikubwa kwa vigenzo vyovyote vya fedha katika dunia hii; kwa Tanzania kiwango hicho ni kikubwa sana hasa kinapolinganishwa na fungu la fedha zilizotengwa kwa sekta muhimu kwa jamii katika mwaka wa fedha wa 2009/10 ambao bajeti ya serikali ilikuwa Sh. trilioni 9.5.

Katika bajeti hiyo elimu ilitengewa Sh. trilioni 1.7, afya Sh. bilioni 963, miundombinu Sh. trilioni moja, kilimo bilioni 666.9, maji Sh. bilioni 347.3 na nishati na madini Sh. bilioni 285.5, ni dhahiri kuwa fedha hizi ambazo zinatoroshwa, kusamehewa au kukwepa kulipa kodi ni nyingi na kama zingetumika kwa ajili ya maeneo hayo hakika hatungehitaji kutembeza bakuli kwa nchi wahisani kuchangia bajeti kila mwaka.

Tunaamini kuwa ripoti hii haikutolewa wiki hii kwa bahati mbaya, ni mkakati wenye lengo la kuwafungua macho wawakilishi wa wananchi, wabunge, kutambua kuwa pamoja na moto waliowasha Aprili mwaka huu na kusababisha mawaziri sita na naibu wawili kufutwa kazi, unapaswa kuendelezwa katika mkutano wa bajeti ili kujenga kinga kuliko kusubiri tiba ambayo gharama yake ni kubwa  sana.

Serikali imekwisha kusema kuwa katika mwaka wa fedha wa 2012/13 itatumia kiasi cha Sh. trilioni 15 likiwa ni ongezeko la takribani Sh trilioni 2.5 ikinganishwa na mwaka unaomaliza wa 2011/12 ambao bajeti ilikuwa Sh. trilioni 13.5, fedha hizi nazo ni nyingi, lakini kutokana na hali halisi ya maendeleo nchi kuna maeneo mengi hajapata fedha kwa kuwa bajeti ni kidogo na mahitaji ni makubwa zaidi ya uwezo.

Kwa miaka mingi sasa serikali imekuwa na majibu mepesi juu ya uhaba wa fedha za kugharimia huduma muhimu kwamba haina fedha, haya yamekuwa ni kama majibu ya kudumu kwa kila changamoto inayohitaji fedha inapotolewa.

Kwa bahati nzuri sasa umma umeamka, makundi mbalimbali katika jamii yanafanya tathmini na kueleza bayana kwamba tatizo la taifa hili siyo ukosefu wa fedha, bali mipango na maamuzi yetu kuhusu fedha ndiyo ya ovyo kabisa.

Mojawapo ni kama ilivyobainishwa na ripoti ya Kamati ya Viongozi wa Dini ambayo imeweka wazi kuwa kiasi cha Sh. trilioni 1.59 kimeyeyuka hivi hivi chini ya mwavuli wa misamaha ya kodi, ukwepaji kodi na utoroshaji wa rasilimali nje ya nchi.

Ni kwa kutambua ukweli huu tunawaambia wabunge kuwa wamepewa kitendea kazi kingine katika kuishughulikia bajeti ya serikali ya mwaka 2012/13 inayowasilishwa bungeni leo saa 10 jioni. Kila la heri.


 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment