Friday Apr 29, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Ni kiama? Waumini wachimbua madhabahu kusaka dhahabu

26th April 2012
Print
Comments

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, madhabahu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheti Tanzania (KKKT), Usharika wa Branti uliopo katika kijiji cha Ihahi, kata ya Chimala, wilayani Mbarali, Mkoa wa Mbeya, yamevunjwa na waumini kwa lengo la kutafuta dhahabu.

Inadaiwa kuwa, waumini hao wamechukua maamuzi hayo baada ya kuwepo na taarifa kuwa wamisionari wa Kijerumani waliolijenga kanisa hilo walichimbia madini chini.

Zoezi la kuchimba madhabahu ya kanisa hilo lilianza Jumatatu wiki hii kwa amri ya viongozi wa kanisa hilo ambao walipata taarifa kuwa Wajerumani ambao walijenga kanisa hilo miaka 100 iliyopita walichimbia dhahabu chini.

Kufuatia tukio hilo, waumini wa kanisa hilo walizua vurugu kupinga zoezi hilo, ambapo hadi kufikia jana watu kadhaa wakiwemo waliokuwa wakiendesha zoezi la kuchimba na baadhi ya viongozi wa kanisa hilo walikuwa wametiwa mbaroni.

Taarifa za kuwepo dhahabu chini katika kanisa hilo lililojengwa mwaka 1905, zilitokana na ujio wa mara kwa mara wa Wajerumani ambao walikuwa wakitembelea kanisa hilo lililokuwa linaendelea kutumika.

Inadaiwa kuwa nao walikuwa na mpango wa kutaka kubomoa ili kutafuta dhahabu iliyowekwa eneo hilo.

Diwani wa Kata ya Chimala, Hussein Buhaye, akizungumza na NIPASHE, alisema zoezo la kuchimbua madhabahu lilianza Jumatatu wiki hii baada ya Mchungaji wa Usharika wa Branti aliyefahamika kwa jina moja la Lunda, kutoa taarifa kwa viongozi wa Jimbo na Dayosisi ya Kusini kwamba katika madhabahu ya kanisa hilo wamisionari walichimbia dhahabu.

Alisema baada ya Mkuu wa jimbo aliyefahamika kwa jina la Ng’umbi pamoja na Askofu wa Dayosisi ya Kusini, Isaya Mengele, kujulishwa taarifa hizo, waliitisha kikao cha wazee wa kanisa na baadhi ya waumini na kukubaliana kuwa wachimbue madhabahu ya kanisa hilo ili kutafuta dhahabu. Buhaye alisema baada ya makubaliano ya viongozi hao, walitafutwa wachimbaji wa madini ambao walikwenda na kifaa cha utambuzi kijulikanacho kama ‘ditector’ ambacho walikwenda nacho katika kanisa hilo na kupima madhabahu ambapo walibainisha kuwa ni kweli kuna madini katika kanisa hilo.

Alisema baada ya wataalamu hao kutoa taarifa hizo, viongozi wa kanisa hilo waliamuru zoezi la kuchimbua madhabahu kwa lengo la kupata dhahabu iliyopo eneo hilo lianze kwa kushirikisha wachimbaji ili madini hayo yatakapopatikana yauzwe na kuwa chanzo cha mapato ya kanisa hilo.

Kutokana na makubaliano hayo, zoezi la kuchimba madhabahu lilianza rasmi Jumatatu ambapo wachimbaji waliopewa kazi hiyo kwa kusimamiwa na viongozi wa kanisa waliifanya kazi hiyo usiku na mchana ili kuhakikisha inakamilika mapema.

Diwani huyo alisema hadi kufika juzi (Jumanne), madhabahu hayo yalikuwa yamechimbuliwa urefu wa futi kumi kwenda chini, lakini hakuna dhahabu iliyopatikana.

Kutopatikana madini hayo wakati tayari madhabahu ya kanisa hilo yalikuwa yamekwisha chimbuliwa urefu huo, waumini wa walikosa imani na wachimbaji pamoja na viongozi waliokuwa wakiendesha zoezi hilo kwa kudai kuwa dhahabu imepatikana, lakini hawataki kueleza ukweli kwa waumini.

Kufuatia wasiwasi huo, saa 4:00 juzi waumini walianzisha vurugu kukataza zoezi hilo kuendelea, kisha walikwenda kutoa taarifa polisi ambao nao walifika eneo la tukio kutuliza ghasia ambazo zilikuwa zimeanzishwa na wananchi wa kijiji hicho.

Polisi baada ya kufika eneo hilo jana waliwakamata vijana waliokuwa wakichimba dhahabu katika kanisa hilo pamoja na baadhi ya viongozi na kuwapeleka katika kituo kikuu cha polisi Rujewa kwa mahojiano zaidi.

Hata hivyo, viongozi wa kanisa hilo hawakupatikana mara moja kuelezea zaidi tukio hilo kwa madai kuwa walikuwa bado wapo polisi kwa mahojiano.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Barakaliel Msaki, licha ya kutafutwa mara kadhaa katika simu yake ya mkononi hakupatikana.

Mkurugenzi Mtendaaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Uswege Kamnyoge, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles