


.jpg)
Serikali imetenga Sh. bilioni 104 katika bajeti ya mwaka 2012/13 kwa ajili ya kuimarisha na kuboresha utendaji wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL).
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alipokuwa akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2012/13.
“Fedha hizi zitatumika kutekeleza mirdi mbalimbali ikiwa pamoja na kujenga upya, injini za treni nane aina ya 88XX, kufanya malipo ya awali ya ununuzi wa injini za treni mpya 13,” alisema na kuongeza:
“Kufanya malipo ya awali ya ununuzi wa mabehewa mapya ya abiria 22 kukarabati mabehewa mabovu ya mizigo 125, kufanya malipo ya awali ya ununuzi wa mabehewa mapya ya mizigo 274, kufanya malipo ya awali ya ununuzi wa mabehewa mapya ya breki 34 na ukarabati wa karakana za Tabora na Dar es Salaam.”
Aidha, alisema katika fedha hizo, Sh. bilioni 18.9 zimetengwa kwa ajili ya kulipa madeni ya kimikataba na Shirika la Kimataifa la Fedha (IFC), RITES , RVR (Uganda) na wadai wengine nchini.
“Ni matumaini ya wizara kuwa uwezeshaji huu kifedha utaongeza idadi ya treni za abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma kufikia treni tatu kwa wiki ifikapo mwishoni mwa mwaka huu,” alisema.
Katika hatua nyingine, Dk. Mwakyembe alisema Sh. bilioni 4.75 zitatumika kwa ajili ya ukarabati wa injini na mabehewa ili kuwezesha usafiri wa njia ya reli kati ya stesheni ya Dar es Salaam hadi Ubungo kuanza kazi Oktoba mwaka huu.
Alisema kuwa fedha hizo zitatumika katika ukarabati wa injini tatu za treni na mabehewa 14 ya abiria.
“Fedha hizi zimepatikana na kazi ya ukarabati wa njia ya reli, injini na mabehewa imeanza na inatarajiwa kukamilika Oktoba mwaka huu,” alisema Dk. Mwakyembe na kuongeza:
“RAHCO (Shirika Hodhi la Mali za Reli), inaendelea na kazi ya kukarabati njia na tayari mataruma mabovu zaidi ya 1500 yamekwishabadilishwa na kazi ya kuweka sawa mataruma ili yakae pembe mraba na reli imekwishafanywa umbali wa kilometa 10.5.”
Hata hivyo, alisema RAHCO inaendelea kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ili kupata ufumbuzi wa changamoto hizo kwa mujibu sheria na taratibu zilizowekwa.
“Huduma hii itaanza kwa treni mbili ambazo zitatoa huduma asubuhi na jioni kuanzia Jumatatu hadi Jumamosi. Treni moja itaanzia stesheni ya Dar es Salaam na nyingine Ubungo Maziwa na kupishana maeneo ya Buguruni kwa Mnyamani,” alisema.
Dk. Mwakyembe alisema treni hizo zitasimama kwenye vituo sita, ambavyo ni stesheni ya Dar es Salaam, Kamata, Buguruni kwa Mnyamani, Tabata Matumbi, Mabibo na Ubungo Maziwa.
Alisema kila treni itakuwa na mabehewa sita yenye uwezo wa kubeba abiria waliokaa na wale waliokaa na wale waliosimama takribani 1000 kila safari.
Kadhalika, alisema Wizara ya Uchukuzi inafanya mazungumzo na Wizara ya Viwanda na Biashara, ili jukumu la kukagua magari yaliyotumika yanayoingia nchini lifanywe na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
“Chuo tayari kimepokea msaada seti nne za vifaa vya kisasa vya ukaguzi wa magari kutoka Benki ya Dunia,”alisema.
Alisema vifaa hivyo vinauwezo wa kukagua magari 800 kwa siku.
Wakati huo huo, Dk. Mwakyembe alisema katika mwaka huu wa fedha Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), itaendelea kutoa huduma kwa kutumia ndege ya kukodi aina ya Boing 737-500 na ndege yake aina ya Dash 8-Q300 ambayo inafanyiwa matengenezo makubwa hapa nchini. Alisema matengenezo hayo yatakamilika katikati ya Agosti mwaka huu.