Monday May 20, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Mabasi ya mikoani yatishia kugoma

17th May 2012
Print
Comments
Kituo cha mabasi yaendayo mikoa cha Ubungo.

Wamiliki wa mabasi yaendayo mikoani kupitia chama chao cha (Taboa), wametishia kugoma nchi nzima wakati wowote kuanzia sasa, ili kuishinikiza serikali itekelezea madai yao mbalimbali.

Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu, wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu maazimio ya kamati ya utendaji ya chama hicho.

Alitaja moja ya kero za wenye mabasi kuwa ni kitendo cha Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), kukataa ombi lao la kupandisha nauli za mabasi yaendayo mikoani.

Alisema gharama za uendeshaji zimepanda sana na walikuwa na kila sababu ya kuomba kupandisha nauli ili kufidia gharama kubwa za uendeshaji kwa wamiliki wa mabasi.

Alisema kero nyingine ni kuvunjwa kwa ofisi za chama hicho zilizopo ndani ya kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo jijini Dar es Salaam bila kupewa eneo jingine la ofisi na la kufanyia matengenezo ya magari yao.

“Wamevunja ofisi za chama bila makubaliano, pale ndipo wenye mabasi walikuwa wakifanya matengenezo ya magari kila siku, hali hii itatuathiri sana, hatujui kuanzia sasa magari yatakuwa yanatengenezewa wapi na tulishazungumza na Wizara ya Tamisemi  kuhusu suala hili lakini hawakuchukua hatua zozote,” alisema.

Pia alisema Taboa walishakutana na Sumatra kuhusu usimamizi wa ratiba na namna ya kuwaondoa wapiga debe kwenye stendi za mabasi yaendayo mikoani, lakini hakuna hata moja ambacho kimetekelezwa licha ya agizo la aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu.

Aidha, alilalamikia usumbufu wanaopata wenye mabasi katika vituo vya ukaguzi barabarani, ambao alidai unafanywa holela na kinyume na taratibu zilizowekwa.

Alisema ingawa vituo vya ukaguzi vimeandikwa katika ratiba za mabasi hayo ambako mabasi hukaguliwa, lakini kumekuwa na utitiri wa vituo barabarani ambavyo hawajui vimewekwa kwa utaratibu upi.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment