Thursday Jun 20, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Taifa Stars ijifunze kwa Samatta

16th June 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Timu ya taifa inacheza kesho nchini Msumbiji katika mechi ya marudiano ya michuano ya awali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kuwania kucheza fainali za mwakani, 2013, za 'Sauzi' ambayo ni lazima kikosi cha kocha Jan Poulsen kishinde ili kuweka hai matumaini ya kurudia rekodi ya Taifa Stars ya kufika fainali za mwaka 1980.

Tangu kupatikana kwa uhuru, Tanzania imeshiriki mara hiyo moja tu fainali hizo, na ni faraja kuwa mechi hii imekuja siku mbili tangu mashujaa hao wa mwaka 1980 waenziwa juzi kwa mara ya kwanza katika halfa ya tuzo za Mwanamichezo Bora wa Mwaka zinazoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (TASWA).

Zimesemwa sababu nyingi za timu yetu kushindwa kurudia mafanikio hayo yaliyoipeleka Taifa Stars Lagos, moja wapo ikiwa ukosefu wa wachezaji wa kutosha wa kulipwa nje ya mipaka ya nchi.

Ni kweli, wachezaji wa kulipwa wana tofauti kubwa kimchezo kulinganisha na wale wa ligi kuu ya Bara ambao, kimsingi, ingawa hulipwa madau ya kujisajili na kuingia mikataba ya kisheria ya mishahara, bado ni wa ridhaa; hasa akilini.

Na tofauti hiyo isingeweza kuwa wazi zaidi ya kitendo cha mshambuliaji Mbwana Samatta wa klabu ya TP Mazembe ya JK Kongo kuamua kulala usingizi kambini badala ya kwenda kwenye hafla ya utoaji tuzo hizo za TASWA ambako Taifa Stars ilialikwa.

Mapumziko -- ya mwili na akili -- ni sehemu muhimu ya ujenzi wa mwili na maandalizi ya mchezaji soka na si rahisi kufahamu umuhimu wa hili kama mchezaji mwenyewe si wa kulipwa, ama kama mawazo ya kiongozi wake hayajajengwa kulitazama jambo hilo katika mtazamo wa kulipwa huko.

Palikuwa na kocha na wachezaji kadhaa wa timu ya taifa katika hafla hiyo ambayo beki wake Shomari Kapombe aliibuka kuwa Mwanamichezo Bora wa Mwaka 2011 na kukabidhiwa ukumbini humo 'hundi' ya sh. milioni 12.

Kwa msingi huo, Samatta ambaye mwaka mmoja uliopita alikuwa akicheza kwa ridhaa yenye mikataba ya kisheria Simba, angeweza kuwepo ukumbini kama bado mawazo yake yangekuwa ni ya kiridhaa-ridhaa.

Lakini katika kuonyesha kuwa kuna tofauti kubwa ya malezi kati ya klabu za TP Mazembe na Simba, nyota huyo aliyeng'ara katika mechi mbili zilizopita za Stars dhidi ya Ivory Coast na Gambia aliamua kulala, akipumzisha mwili na akili.

Aliamua kumpuzika kwasababu Stars ilikuwa ikisafiri alfajiri ya jana na kwasababu katika soka la kulipwa mapumziko ni moja ya misingi ya mafanikio ya uwanjani, muda wa kulala usingetosha kama naye angetoka ukumbini usiku wa manane.

Ni jambo dogo, wachezaji wa Taifa Stars na viongozi wake wanaweza kuona. Lakini wamuulize Samatta na endapo patafanyika utafiti wa kisayansi hatutashangaa, Nipashe, kuona kwamba ukosefu wa mapumziko ni moja ya sababu zilizoiwezesha TASWA kuwa na fursa ya kutunuku timu NZIMA ya mwaka 1980 katika kipengele cha Tuzo ya Mafanikio ya kutukuka.

Nchi ina wachezaji wengi wenye vipaji na uwezo wa kutosha kuondoa uwezekano wa kikosi kizima cha mwaka mmoja kupewa nishani, Nipashe tunaona.

Lakini nchi haifanikiwi Afrika na kwenye Kombe la Dunia, Nipashe tunaona, kwa sababu ya kuupuzwa kwa mambo madogo madogo kama haya ya wachezaji kupumzika vya kutosha kama ambavyo Samatta ameifundisha Stars.

Hata kama Kapombe na wenzake wa ridhaa walikuwa watajwa katika vipengele mbalimbali vya tuzo za TASWA, walipaswa kuamriwa kulala na uongozi wa Taifa Stars kwasababu usingizi wa angalau saa sita kwa usiku mmoja ni muhimu katika si tu ufanisi bali pia maendeleo ya mchezaji husika.







 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment