Thursday May 5, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Kimbunga kwa watendaji kinapoendelea... TRA panueni wigo zaidi

20th May 2012
Print
Comments

Kinachoendelea sasa katika sura ya uwajibikaji kwa viongozi wa awamu hii baada ya Rais Kikwete kubomoa Baraza la Mawaziri hivi karibuni, ni ishara tosha kuwa viongozi hao wamedhamiria kutekeleza ilani na kanuni za uwajibikaji kwa kiwango kikubwa.

Ni imani yetu kuwa kama kasi waliyoanza nayo itaendelea, lazima matokeo yake yatapimika kwa urahisi baada ya muda si mrefu kuanzia sasa.

Ni dhahiri kuwa yote yaliyojitokeza katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa serikali yalitokana na kashfa za ulaji na ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma.

Ni fedha za wananchi wa kada mbalimbali, wakulima, wafanyakazi walioajiriwa serikalini, katika makampuni binafsi, taasisi zote pamoja na kodi za wafanyabiashara mbalimbali hapa nchini.

Wote kwa pamoja wanawajibika kusimamia matumizi halisi ya fedha zao kwa ajili ya maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Wakati kazi ya ukusanyaji wa kodi imekasimiwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ni wajibu wa wananchi pia kuisaidia mamlaka hayo ili ifanye kazi kwa ufanisi zaidi, nchi hii ni kubwa sana na sehemu kubwa ya wajasiriamali wametapakaa katika kila kona ya nchi hii, kama serikali itawategemea waajiriwa wa Mamlaka hayo pekee katika kukusanya kodi, wafanyabiashara wengi wataendelea kutolipa kodi za biashara wazifanyazo.

Moja ya sifa za wafanyabiashara ndogo ndogo hapa nchini ni kukwepa kulipa kodi. Wengi wao hata leseni za biashara hawana, na wanaendelea kupata faida kubwa bila kulipa kodi, wajasiriamali kama hao hawana tofauti kubwa na watendaji wabadhirifu wa fedha za umma. Lazima nao wadhibitiwe!

Yapo maeneo mengi ambako wajasiriamali wamewekeza na wanafanya biashara zenye faida kubwa bila kulipa kodi, baadhi ya biashara ambazo hazilipiwi kodi ni za maduka, mabaa, nyumba za kulala, famasi, zahanati nk.

Mfano upo utitiri wa maduka katika kila kona ya jiji la Dar es Salaam, na hata ukimwuliza mwenye duka kama anayo leseni ya biashara aifanyayo atakushangaa na kudhani wewe ni mmoja wa wapinzani wa maendeleo yake, suala la kulipa kodi kwa biashara nyingi hapa nchini siyo utamaduni wa wajasiriamali wengi.

Utafiti wa haraka uliofanyika hivi karibuni na mmoja wa wapangaji katika moja ya kontena la mfanyabiashara maarufu ambaye pia anamiliki kampuni ya mafuta nchini, ulibaini kuwa mwekezaji huyo amewapangisha wajasiriamali zaidi ya 15, walioweka maduka na wengine baa.

Cha kushangaza anawapangisha bila kuwa na mikataba nao, wapangaji kazi yao ni kwenda kulipia kodi la pango kwa miezi sita na wala hawapewi stakabadhi ya aina yoyote. Utafiti ulibaini kuwa mwekezaji huyo tayari amekwepa kodi serikalini ya mamilioni ya fedha.

Sina uhakika namna TRA wanavyojipanga kuwabaini wasiolipa kodi, lakini nina uhakika kuwa wanaolipa kodi hapa nchini ni nusu ya wote waliostahili kulipa kodi kihalali, na kutokana na utamaduni wa kutopenda kulipa kodi kwa baadhi ya wafanyabiashara hao, makusanyo ya fedha zitokanazo na kodi yataendelea kutegemea biashara zenye mitaji mikubwa mikubwa tu, wakati huo huo serikali ikiendelea kupoteza fedha nyingi kutokana na biashara nyingi zisizosajiliwa.

Athari kwa TRA ya kutofanya makusanyo yanayostahili, yamesababisha manung'uniko mengi kutoka kwa taasisi na asasi mbalimbali zilizotegemea ruzuku ya fedha toka serikalini, ambapo hadi sasa serikali nayo imesema haina mafungu ya fedha kwa huduma hizo.

Moja ya walioathirika sana kutokana na serikali kudai kuwa haina fedha ni wastaafu wanaopata pensheni zao kila baada ya miezi mitatu mitatu sasa. Wastaafu hao ambao walitumikia idara na sekta mbalimbali za serikali bado wanapata pensheni kwa kiwango cha chini kabisa, fedha anazozipata mstaafu baada ya miezi hiyo mitatu zinamwezesha kuishi kwa muda wa wiki moja au mbili tu.

Nina imani kuwa kama vitengo vyote, au asilimia 75 tu ya vitengo vinavyotakiwa kulipa kodi vingefanya hivyo, makusanyo ya kodi yangesaidia serikali kutoa huduma bora zaidi kwa upatikanaji wa madawa katika mahospitali, madawati kwa wanafunzi, mishahara mizuri ya watendaji pamoja na kuboresha huduma nyingine muhimu za kijamii.

Wastaafu nao wangefaidi matunda ya uasisi wao katika maendeleo ya taifa hili, kwani wastaafu wa miaka hii ndio waasisi halisi wa misingi ya uchumi uliopo, wanastahili kuenziwa kwa utumishi wao uliotukuka, lakini si kuwaenzi kwa maneno, wanastahili kuhudumiwa ipasavyo na wasijutie kustaafu kwao!

Idara ya TRA, ijaribu kushirikisha wananchi wote kwa kuwapa aina fulani ya motisha kwa kuwataja wajasiriamali wanaokwepa kodi huko mitaani, wananchi wanawajua na TRA watumie mbinu kama za ki-polisi za ulinzi shirikishi, kwa kuwabaini wakwepa kodi.

Inawezekana kabisa hata kama ni kiasi kidogo cha fedha za kodi lakini kwa ujumla wa wanaokwepa, fedha hizo ni nyingi sana. Mfano yapo majumba yanayokodisha wanafunzi wa Vyuo Vikuu kwa kuwatoza kila kitanda Sh.60,000 kwa mwezi, na wanawajibika kulipa kwa miezi sita, na jumba hilo unakuta lina vitanda 50. Wakilipa wote kwa miezi sita mmiliki wa jumba hili ambaye wala halipi kodi yoyote anavuna zaidi ya milioni 36/- kwa miezi sita tu! Naye huyu ni mhujumu wa uchumi, abanwe na kuwajibishwa!

Maoni: 0715-047304, 0762233116.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles