Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Berko: Nilisikia kizunguzungu nikaomba kutoka

8th May 2012
Print
Comments
Kipa wa Yanga, Mghana Yaw Berko

Kipa wa Yanga, Mghana Yaw Berko, alisema jana kuwa katika mechi ya funga dimba ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Simba juzi aliomba kufanyiwa mabadiliko kutokana na kuona hali ya kizunguzungu uwanjani.

Berko ambaye mzunguko wa pili msimu huu alikaa benchi kwa muda mrefu kutokana na kuuguza bega lake alianza katika kikosi cha kwanza lakini hakurejea tena uwanjani baada ya mapumziko.

Nafasi yake ilichukuliwa na kipa aliyekuwa kwenye benchi, Saidi Mohammed ambaye alifungwa magoli manne huku Berko yeye akifungwa goli moja na Emmanuel Okwi, ambalo lilikuwa ni la kwanza katika mechi hiyo iliyokuwa ya kukamilisha ratiba kwa timu zote mbili.

Akizungumza na gazeti hili jana mchana, Berko, alisema kwamba hali yake ilibadilika ghafla akiwa uwanjani tofauti na alivyokuwa akijisikia kabla ya kuanza kwa mchezo huo.

Berko alisema kuwa anashukuru daktari wa timu, Juma Sufiani, kwa kumweleza kocha wao, Fred Minziro, ambaye aliamua kufanya mabadiliko na kumuingiza kipa wa akiba, Mohammed.

"Sijadanganya na wala sikuwa naogopa, sikujua yatakayotokea mbele," alisema kwa kifupi kipa huyo ambaye si mzungumzaji, ambaye amekuwa akituhumiwa kusingizia kuumia kila anapoona atachafua rekodi yake kwa kufungwa magoli mengi katika mechi ngumu.

Alidaiwa kufanya hivyo katika mechi dhidi ya Dedebit ambapo Yanga walikomboa magoli na kupata sare ya 4-4 jijini Dar es Salaam kabla ya kwenda kutolewa kwa 2-0 nchini Ethiopia katika Kombe la Shirikisho Februari mwaka jana.

Berko aliumia bega katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi yaliyofanyika mapema mwaka huu na alitoka nje akiwa tayari ameshafungwa magoli 3-0 na Azam.

Akiwa amemaliza mkataba wake bado hatma yake ya kuendelea kuichezea Yanga bado haijajulikana sawa na Davis Mwape ambaye anamaliza mkataba mwezi Julai mwaka huu.

Berko na nyota wengine wa kigeni wanaoichezea Yanga (Keneth Asamoah, Khamis Kiiza, Haruna Niyonzima na Mwape) wanatarajia kurejea makwao wakati wowote kwa ajili ya likizo na watarudi kuanza mazoezi ya kujiandaa na Kombe la Kagame mapema mwezi ujao.

Kuna taarifa kutoka katika kambi ya Yanga kuwa siku mbili kabla ya mechi hiyo ya watani kipa aliyekuwa anatarajiwa kuanza, Shabani Kado, alielezwa kwamba hatacheza mechi hiyo kutokana na kuhofiwa ataihujumu timu.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles