Thursday May 23, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Ajali yaua sita Manyara

26th May 2012
Print
Comments

Watu sita wamefariki dunia baada ya lori walilokuwa wakisafiria kupinduka kwenye mteremko wa mlima Sigino uliopo Kata ya Sigino, katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Mkoa wa Manyara, jana asubuhi.

Mashuda wa ajali hiyo wakizungumza kwa njia ya simu toka eneo la tukio walisema jana kuwa, lori hilo lililokuwa limebeba mbao likitokea mkoani Iringa kuelekea mjini Babati, kabla ya kutokea lori lilionekana likiwa limekosa mwelekeo.

“Wakati likiteremka lilionekana linayumba na kukosa mwelekeo hatua ambayo iliyafanya mabasi na magari mengine yaliyokuwa yakipanda kuelekea Singida, kusimama pembeni mwa barabara kwa kuhofia kugongana,” alisema Deo Kisima mkazi wa Dareda.

Alisema kabla ya kupinduka, baadhi ya mbao zilianza kuanguka barabarani na kuwajeruhi watembea kwa miguu wanne ambao majina yao hayakuweza kupatikana na kisha kupinduka karibu na daraja.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo ambayo alisema chanzo chake ni kutokana na hitilafu kwenye mfumo wa breki.

“Ni kweli kuna ajali imetokea huku majira ya asubuhi kwa lori moja aina ya Scania ‘semi trela’ lililokuwa limebaba mbao kutokea Iringa, chanzo ni kukosa breki na akashindwa kulimudu kwenye mteremko huo mkali,” alisema na kuongeza, watu sita akiwemo dereva na mmiliki wa lori hilo ambaye ni mfanyabiashara maarufu mjini hapa walifariki dunia.

Alisema watu hao walikufa papo hapo na maiti zimehifadhiwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Babati.
Miongoni mwa waliofariki ni dereva aliyetambuliwa kwa jina la Paulo Charles (38) mkazi wa Mafinga Mkoa wa Iringa na mmiliki wa lori hilo Josephat Mkalama mkazi wa Oysterbay mjini Babati.

Hii ni ajali ya pili kutokeo mkoani humo katika kipindi cha wiki moja baada ya watu sita kufariki dunia baada gari aina Noah kupinduka wakati waombolezaji hao wakitokea msibani katika kijiji cha Hala mjini Babati.

 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment