Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Bila nidhamu riadha `itaoza`

28th April 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Kamati ya Olimpiki ya Taifa (TOC) hivi karibuni ilimfungia kwa miezi minane mwanariadha wa mbio ndefu Fabian Joseph.

TOC ilimpa Joseph kifungo hicho kwa kosa la kuchelewa kujiunga na kambi ya timu ya taifa inayotarajiwa kushiriki Michezo ya Olimpiki ya London ya Julai 27 mapa Agosti 12 bila kutoa maelezo ya tatizo hilo.

Lakini ndani ya wiki moja, Chama cha Riadha (RT) kikatangaza kukutana na Joseph kwa ajili ya kujadili kifungo na kufukuzwa kwake katika kambi ya maandalizi ya Michezo ya Olimpiki.

Lengo la mkutano, RT imesema, ni kutaka busara itumike na kuona mkimbia marathon huyo anarudishwa na TOC kambini.

RT kama chama kikuu cha riadha, ndiyo mlezi mkuu wa wanariadha wetu na hakijatoka nje ya mipaka yake wakati kikitafuta suluhu ya kutimuliwa kambini kwa mkimbiaji huyo.

Lakini ambacho RT imepotoka, tunaona Nipashe, ni jitihada inazofanya kumrejesha Joseph kwenye timu ya taifa huku kikiwa chenyewe hakijakemea kitendo cha mkimbiaji huyo cha kutoripoti kambini licha ya jitihada kubwa za TOC za kumuita na kumtafuta.

Upo uwezekano mkubwa kwamba Joseph hakuripoti kambini katika muda aliotakiwa kutokana na sababu halisi; kama mwenyewe anavyodai kwamba alikuwa akiuguliwa na mwanawe mkoani Arusha.

Lakini Joseph na RT ni lazima wafahamu kuwa kutokana na kupanuka kwa teknolojia na urahisi wa matumizi ya TEKNOHAMA siki hizi, mwanariadha huyo alikuwa katika nafasi ya kutoa taarifa rasmi kwa TOC juu ya kadhia iliyomkuta hivyo madai yake hayana nguvu.

Na kwasababu ya urahisi wa matumuzi ya TEKNOHAMA, kitu cha kwanza ambacho Joseph na RT walipaswa kufanya si kupingana na maamuzi ya TOC.

Kitu cha kwanza ambacho Joseph na RT walipaswa kufanya ni kuomba radhi kwa TOC kwa kosa la kushindwa kuripoti kambini kwa wakati na ndipo, baadaye, wafikirie kuiomba kamati hiyo kumrejesha kwenye timu ya taifa.

Hata kama mkimbiaji huyo na chama chake wangefanya hivyo, bado Nipashe tunaona, upo umuhimu wa RT na vyama vingine vyote vya michezo kwa ujumla kufahamu kuwa hakuna mchezaji yeyote anayeweza kufanikiwa kwenye fani hiyo bila ya kuzingatia nidhamu.

Nidhamu kwake mwenyewe kama mchezaji akiheshimu mchezo huo kama ndiyo ajira na maisha aliyochagua, lakini pia nidhamu kwa viongozi wa mchezo wenyewe.

Katika 'uhai' wa miaka 50 wa Tanganyika na baadaye Tanzania, riadha ndiyo mchezo pekee ambao umeweza kuitangaza nchi kwa kiwango cha dunia baada ya wakimbiaji mahiri wa zamani kama Filbert Bayi na Suleiman Nyambui kuwahi kurudi nchini na medali za Michezo ya Olimpiki.

Viongozi wa RT wamewahi kukaririwa wakijivunia hilo katika midahalo na kauli mbalimbali za kutetea maslahi ya mchezo huo nchini.

Lakini RT ni lazima ifahamu kuwa enzi za Bayi na Nyambui nidhamu ya wakimbiaji hao ilikuwa juu, juu, juu zaidi.

Ni enzi ambayo mchezaji binafsi alijua wajibu wake kama mkimbiaji na kwa taifa lake hivyo vitendo kama vya kuchelewa kujiunga na kambi ambayo inalenga kumuandaa vizuri mchezaji husika vingekuwa ni ajabu.

Kwa mtizamo huu wa RT na mkimbiaji husika wa kuchukulia mambo kwa wepesi tu, haishangazi basi kuona riadha imeshuka kule kule kwenye soka na michezo mingine inapokuja suala la kuleta heshima kimataifa.

Na ndiyo maana basi, wakati kina Bayi na Nyambui walikwenda kwenye Olimpiki na kurudi kishujaa baada ya kuwa washindi wa michuano ya Jumuiya ya Madola na mingine yeye hadhi ya kimataifa, RT leo inapigania kumrejesha kambini mchezaji ambaye ni bingwa wa mbio za Nusu Marathon za Ngorongoro!

Bila nidhamu ya kutosha mchezoni, mwanariadha hatopeperusha bendera ya nchi kwenye Olimipiki kama ambavyo RT inalilia.

Bila nidhamu ya kutosha mchezoni, mwanariadha ataishia kwenda kuwa mtalii na kusababisha RT ije na sababu yake ya kawaida ya kufanya vibaya kwa timu zetu katika mashindano makubwa kama ya Olimpiki -- maandalizi duni.

Tutakosaje kuwa na maandalizi duni kama wito wa kujiunga na kambi tu, kwa mfano, unapuuzwa?

RT ni lazima ifahamu kuwa riadha ya sasa nchini, ukilinganisha na enzi za kina Bayi na Nyambui, imeshakufa na ndiyo maana pamekuwa na matokeo mabaya mfululizo kwa miaka mingi.

Hivyo RT ni lazima ifahamu pia kuwa bila kurudi katika msingi wa mafanikio ya mwanamichezo -- nidhamu -- riadha ambayo imeshakufa, itaoza kabisa.
Zitabaki stori.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles