Wednesday Jun 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Wanazuoni wajadili mgawanyiko bungeni kuhusu Wizara ya Nishati

29th July 2012
Print
Comments
Dk. Benson Bana

Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, amesema kuwa, mgawanyiko uliopo bungeni wa baadhi ya wabunge kuunga mkono na wengine kutetea uozo uliopo Tanesco ni kudhihirisha kuwa Nishati kuna matatizo na kutaka iundwe kamati teule itakayohusisha watu kutoka nje.

Dk. Bana alisema kuwa, uozo wa wizara hiyo ulianza kuonekana toka awali ndio maana bunge lilitaka Waziri Mkuu kuwajibika huku aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, William Ngeleja na Katibu Mkuu wake, David Jairo, waliwajibishwa.

"Tafsiri ya haya yanayoendelea bungeni ni kidhihirisho kuwa wizara hii haijatulia na ndio maana wabunge wanagawanyika kwa sababu wapo wanaohoji kihalali ukiukwaji wa kanuni za manunuzi na kuona kuna maslahi binafsi yaliyotangulizwa huku wengine wanaonyesha kutumiwa na watendaji kutetea uozo," alisema na kuongeza:

"Hii ndio iliyomfanya Mbatia atoe nyaraka za mkataba zinazoonyesha jinsi mke wa Mhando wa Tanesco alivyopewa tenda, lakini ninachoweza kusema Mhando anajua maadili ya utumishi hivyo busara itumike," alisema.

Pia amemlipua Mbunge wa Kigoma, Zitto Kabwe kuhusiana na kauli zake zilizokinzana kuhusu Mkurugenzi Mkuu Mtendaji Tanesco aliyesimamishwa, Mhandisi William Mhando na kueleza kuwa amekuwa kigeugeu kwa sababu awali alitaka mkurugenzi huyo aondolewe jenereta lililopo nyumbani kwake na sasa anamkingia kifua.

"Anayemtetea Mhando anamaslahi binafsi kwa sababu upo ushahidi uliotolewa dhidi ya mke wake," alisema.

Alipotakiwa kutoa maoni yake ya nini kifanyike kutokana na mgawanyiko huo, Dk. Bana alisema kunatakiwa kuundwe kamati teule ikibidi baadhi ya watu wake watoke nje ya nchi ili iiangalie Tanesco ikiwezekana ichambuliwe upya.

Kuhusu kauli za baadhi ya wabunge wakitaka waliohusika kutajwa majina, mhadhiri huyo alisema kufanya hivyo ni kuligawa bunge na badala yake amewataka wazingatie maslahi ya umma.

Pia amewataka Watanzania kuendelea kushinikiza wabunge wao watende haki na wale wanaotetea uovu na uozo wawajibishwe.

"Wabunge wajadili hoja zao kwa haki na watafute taarifa sahihi na waachane na mambo ya kutetea uovu kwa maslahi yao wenyewe, wakumbuke wapo pale kama wawakilishi wa Watanzania," alisema.

Naye, mbunge wa zamani wa Temeke (CCM), John Kibasso, alisema kuwa utawala unapokuwa wa haki na sheria mara nyingi huwa kuna kitu kinapungua kwa wabunge.

Alitaja baadhi yake kuwa ni pamoja na haki ya kuaminiana, ubinafsi na kusahau kilichowapeleka bungeni.

"Baadhi ya wabunge husahau nini kilichowapeleka bungeni badala yake wanaingilia kazi za mihimili mingine, wanafanya kazi za serikali za kiutendaji, kwenye hili Rais Jakaya Kikwete anatakiwa kuingilia kati kwa kuitisha kikao ambacho kitawakumbusha majukumu ya kila mhimili," alisema.

Kuhusu kutajwa majina waliotuhumiwa, Kibasso ameomba kama kuna matatizo ya kimahesabu ifanyike kama ilivyokuwa awali kwa kumuita Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utoh bungeni.

Pia amewataka wananchi kutokubali kama 'bendera fuata upepo' badala yake wakubali kuongozwa kwa haki.

Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Profesa Issa Shivji, kwa upande wake alieleza kuwa kifupi kuwa, wanaotuhumiwa hawawezi kuhukumiwa bila ushahidi.

KANISA LANENA

Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Mhashamu Methodius Kilaini, kwa upande wake alisema kuwa, anapata mashaka kuamini kama baadhi ya wabunge wapo bungeni kwa maslahi yao binafsi au kwa taifa.

Askofu Kilaini alisema kwa kawaida yule anayetetea kwa kuokoa mali za Watanzania hupaswa kushukuriwa na kuungwa mkono kinyume na hapo hatufai.

Kadhalika ameunga mkono hoja za baadhi ya wabunge ambazo zimetaka wahusika watajwe hadharani na kusema kuwa, itakuwa fundisho kwa wengine.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment