Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Ukatili wa kijamii wakithiri nchini

29th July 2012
Print
Comments

Mmomonyoko wa maadili nchini umeelezwa unachangiwa na vitu vingi yakiwemo malezi mabaya, usimamizi mbovu wa familia lakini pia na vyombo vya habari na hivyo kuchangia kuongezeka kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Kutokana na mazingira hayo, serikali na taasisi za dini zimeshauriwa kutokomeza ukatili wa jinsia na kudhibiti lugha na picha chafu kwenye vyombo vya habari.

Kauli hiyo ilitolewa na viongozi wa dini na wananchi walioshiriki kwenye kipindi cgha ‘zungumza’ kilichokuwa kikijadili wajibu wa viongozi wa dini katika kutokomeza ukatili wa kijinsia (Uwaki).

Katika mjadala huo, ulioandaliwa na mradi wa sera za afya chini ya taasisi ya Future Group International kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) kupitia mpango wa dharura wa Rais wa Marekani wa kupunguza Ukimwi (PEPFAR), baadhi ya viongozi wa dini wameeleza kuwa kupokonywa umiliki wa shule zao kumesababisha kuporomoka kwa maadili kwani walikuwa wakizitumia shule hizo katika kuelimisha watu.

Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Newala, Oscar Mnung'a, alisema ukatili wa kijinsia hasa wa wanandoa, unasababishwa na kutoandaliwa ipasavyo kwa wanandoa hao.

Alisema kanisa lake hulazimika kuingilia kati kuvunja ndoa hiyo endapo mwelekeo ni kuleta athari kwa mwanandoa moja.

Kwa mujibu wa askofu huyo, endapo kunatokea migogoro ya ndoa inayosababisha ukatili, wajibu wa kanisa ni kuwaita wanandoa hao katika vikao mbalimbali vya usuluhishi, lakini ikishindikana humtenga mmoja wapo na kanisa na wakati mwingine hulazimika kunusuru maisha ya wanandoa hao kwa kuwatenganisha na kila mmoja kuwa huru kuoa, kuolewa.

Alisema hatua hizo zimesaidia kuwaweka sawa wanandoa na hivyo kuepusha kuwepo kwa tatizo la ukatili wa kijinsia.

Hata hivyo alisema ukatili wa kijinsia chanzo chake kikubwa ni kuporomoka kwa maadili kunakosababishwa na kutokuwepo kwa maandalizi ya maisha ya imani kutoka kwa watoto na vijana.

"Zamani taasisi za dini zilikuwa na shule zake, humo kulikuwa kunafundishwa masuala mbalimbali ya dini, lakini baada ya serikali kutaifisha shule hizo, sasa hivi elimu hiyo haitolewi," alisema.

Alisema Makanisa yote yaliyopo chini ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kila Jumapili hutoa elimu ya dini kwa watoto na msisitizo sasa hivi ni kujenga madarasa mengi ili kutoa elimu hiyo kwa wakati.

Hata hivyo alisema vyombo vya habari vinachangia kwa kiasi kikubwa kuporomoka maadili ya Watanzania.

Kwa upande wake Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaji Musa Salum, alisema anachoamini hakuna dini hata moja inayofundisha kuporomoka kwa maadili na kwamba hali hiyo inachangiwa na wanajamii wenyewe.

Alisema viongozi wa dini nao wanatakiwa kuwa karibu na watu wanaotaka kufunga ndoa, kwa kuwajua vizuri kama waumini wao ili kuepusha ndoa za muda mfupi na za hatari.

"Mtu asiye na maadili ifikie wakati asipewe mke. Akipewa kwa sababu ya fedha zake, anaweza kufanya vitu vya ajabu sana. Uadilifu huanzia kwa wazazi kwani mke, mume na mtoto mwenye maadili hutoka kwa wazazi wenye maadili," alisema.

Sheikh Salum alisema matukio mengi ya ukatili wa kijinsia yako vijijini, ambako wananchi hawapati elimu ya dini zaidi ile ya mila zao kutokana na viongozi wengi wa dini kujikita zaidi mijini.

Alisema kumekuwa na ukatili katika maeneo mengi na waathirika zaidi ni wanawake na watoto hasa katika mila na desturi ambazo hazimruhusu mwanamke kupata urithi, mali, elimu, kushirikishwa.

Mchungaji kutoka Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekosti, Sixtus Mallya, alisema kanisa hilo linahamasisha watu hasa wanaume kutumia rasilimali za familia kwa manufaa ya familia husika.

Alisema hata misahafu inasisitiza mwanaume kumpenda mkewe na mwanamke kumtii mumewe.

Mjadala huo ambao ulihusisha makundi mbalimbali ya kijamii, ulijikita zaidi katika ukatili wa wanandoa ambao wameelezwa kuwa ndio chanzo cha familia kusambaratika na kuzalisha watoto wa mitaani.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment