Friday May 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Kandoro apokea barua kujiuzulu kwa DC Mbozi

6th May 2012
Print
Comments
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya imethibitisha kupokea barua ya kujiuzulu kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Gabriel Kimoro.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, akizungumza na NIPASHE Jumapili jana alisema amepokea rasmi barua ya mkuu huyo wa wilaya ambayo ameeleza sababu kadhaa zilizomfanya achukue uamuzi huo.

Kandoro alisema miongoni mwa sababu alizozieleza ni mkataba wake wa kuwa Mkuu wa wilaya umekwisha tangu 2010 hivyo amekuwa akifanya kazi bila ya kuwa na uhakika kama ataongozewa muda.

Alisema Mkuu huyo wa wilaya pia ameeleza sababu nyingine kuwa ni ugomvi na kampuni moja inayonunua kahawa mbichi ambayo hata hivyo hakuweza kuitaja.

Kandoro alisema kiutaratibu barua hiyo itafikishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ndiye mwenye mamlaka ya uteuzi kwa maamuzi.

Hata hivyo, kujiuzuru kwa Mkuu huyo wa wilaya ambako siyo jambo la kawaida kwa viongozi wa Serikali kumezua maneno mengi wilayani Mbozi na Mkoa wa Mbeya kwa ujumla.

Baadhi ya wananchi na viongozi wa Serikali wamesema mkuu huyo ameamua kuchukua hatua hiyo kwa sababu inawezekana alikuwa amekwishajulishwa mapema kwamba hatakuwepo katika uteuzi wa wakuu wa wilaya unaotarajia kufanywa na Rais kutokana na madai ya kashfa kadhaa zilizokuwa zinamkabili.

Wakati viongozi wa Serikali wakibashiri hivyo, baadhi ya wanasiasa wamesema mkuu huyo wa wilaya ambaye ni kada wa CCM na aliyewahi kugombea ubunge na kubwagwa kwenye kura za maoni, ameamua kuachia ngazi hiyo kwa madai kuwa ana mpango wa kutimkia katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Mapema Februari, mwaka huu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha alielezwa na viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbozi aondoke na Mkuu wa Wilaya, Kimoro kwa kumpakiza katika gari lake kwa madai hawawataki katika wilaya hiyo.

Viongozi na wanachama hao walimweleza hivyo Nahodha kwenye Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ambao pia ulihudhuriwa na Katibu wa CCM mkoa wa Mbeya, Verena Shumbusho uliofanyika mjini Tunduma katika hoteli ya High Class.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles