Friday May 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Wananchi Arumeru kugawiwa mashamba

26th April 2012
Print
Comments
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo

Wilaya ya Arumeru imeanza kufanya tathmini ya mashamba makubwa 19 yanayomilikiwa na wawekezaji wa ndani na nje kwa lengo la kuangalia uwezekano wa wamiliki hao kupunguza baadhi ya maeneo yao ili kuwapatia wananchi ambao hawana kabisa ardhi wilayani humo.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, na kuwataka wananchi wilayani humo kuacha tabia ya kuuza mashamba yao yote hali ambayo itawafanya kuwa na maisha magumu zaidi.

Kikao cha kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na mambo mengine, kilikuwa mahususi kujadili na kutafuta ufumbuzi wa migogoro ya uvamizi wa ardhi wilayani humo, inayofanywa na baadhi ya wakazi wake wakitaka kuchukua kwa nguvu maeneo yanayomilikiwa na wawekezaji hao kwa madai kuwa hawana ardhi huku wawekezaji hao wakikwa wamehodhi ekari nyingi.

“Halmashauri inafanyia tathmini mashamba 19 yanayomilikiwa na wawekezaji wilayani humo…tunataka kuangalia uwezekano wa kupunguza baadhi ya ekari zinazomilikiwa na wawekezaji hao ili kuzigawa kwa wananchi ambao hawana mashamba kabisa,” alisema.

 

Hata hivyo, alisema suala hilo linafanywa kwa uangalifu kwa kuwa wawekezaji hao wanamiliki ekari hizo kihalali na kwa mujibu wa sheria, hivyo hayawezi kurudishwa isipokuwa kuangalia uwezekano wa kupunguza. Akijibu swali iwapo tathmini hiyo itafanywa hata kwa shamba la muasisi wa Chadema, Edwin Mtei, Mulongo alikubali kuwa shamba hilo nalo litafanyiwa tathmini hiyo.

Hivi karibuni, Aprili 14 na 15, baadhi ya wananchi na maeneo ya vijiji vya Kitefu, Migadini, Maroroni na kwa Ugoro wanaokadiriwa kufikia 450 walivamia shamba la Dolly Estate Ltd lililopo eneo la Maji ya Chai na kufanya uharibifu kwa kukata uzio unaozunguka eneo hilo la shamba na pia kuwajeruhi baadhi ya walinzi wa shamba hilo pamoja na kuchoma moto vibanda vyao. Shamba hilo lenye ukubwa ekari 4689 linamilikiwa na mwekezaji kutoka nchi moja ya Ulaya, Jerome Bruins.

Pamoja na uvamizi wa shamba hilo, Aprili 21 muda wa usiku na Aprili 22 kuanzia majira ya asubuhi watu wanaokadiriwa kufikia 500 walivamia shamba la Machuma Estate linalomilikiwa na Tosk Hans na Depee Hans.

Mulongo alisema sababu kubwa inayoelezwa na wananchi hao kuwa chanzo cha uvamizi huo ni kutaka kurejeshewa ardhi wanayodai kuwa ni mali yao na kwamba hata kama ardhi hiyo imepewa mwekezaji/wawekezaji, wao kama wananchi hawanufaiki kwa namna yo yote kutoka kwa wawekezaji hao.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles