Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Soko Mbezi Beach lageuka danguro

2nd June 2012
Print
Comments
  Masoko Kariakoo wafanye hima kunusuru
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka

Baadhi ya mabanda yaliyojengwa kwa ajili ya   biashara katika soko la Makonde Mbezi Beach linalotakiwa kuvunjwa na Shirika la Masoko Kariakoo, yamegunduliwa kuwa ni madanguro na maskani ya wavuta bangi.

NIPASHE Jumamosi imegundua kati ya mabanda 195 yaliyojengwa kwa ajili ya kufanyia biashara mbalimbali, yanayotumika kwa sasa ni 40 tu hali ambayo huenda ilimshawishi Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka kuwapa siku 14 wamiliki wa eneo hilo, Shirika la Masoko Kariakoo, kuelezea eneo hilo watalifanyia nini.

Wakizungumza na mwandishi wa gazeti hili, baadhi ya wafanyabiashara sokoni hapo, walikiri mabanda mengi yaliyotelekezwa na wahusika yanatumika kwa kazi nyingine zisizoendana na soko kama; ‘gesti bubu’ na 'gheto' za kuvutia bangi.

“Kwa kuwa hapana ulinzi wa kueleweka hapa sokoni, basi kila mfanyabiashara huamua kutafuta mlinzi wake wakulinda eneo lake, na banda ambalo halina mwenyewe linafanywa danguro ama kambi ya wahuni,” alisema mmoja wa wafanyabiashara hao.

Aidha, alisema mabanda hayo yanashindwa kutumika na wamiliki wake kutokana na kutokuwa na idadi kubwa ya watu katika maeneo hayo wanaonunua bidhaa sokoni hapo, ndio maana wameamua kufunga.

Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili Mwenyekiti wa kamati iliyoundwa kuokoa soko hilo lisivunjwe na Masoko Kariakoo, Byamungu Bugingo, alikiri kuwepo na makazi ya watu katika baadhi ya mabanda sokoni hapo, lakini hana uhakika iwapo yanatumika kwa ukahaba.

“Baadhi ya watu walikuwa wakiishi hapa, lakini sina hakika kama walikuwa wakiendesha
madanguro…kamati yangu imefanya kazi ya kuhakikisha hali inakuwa nzuri mahala hapa,” alisema Bugingo.

Bugingo aliiomba Kariakoo kuwapa muda wa kuondoka katika kitalu hicho G, TP No.1/847/597 ya 97, kwani wamewasilisha ombi kwa wakili wao ili aweze kupinga mahakamani.

“Eneo hili halikuvamiwa na wafanyabiashara, isipokuwa Kariakoo walitumia maneno yasiyo na busara ya kutuambia tumevamia, hapa tumejenga kwa haki tangu 2001,” alisema mjumbe mwingine wa kamati hiyo, Lucas Kijana.

Akizungumza na gazeti hili juzi, Meneja wa Shirika la Masoko Kariakoo, Florence Seiya, alisema walishatoa muda kwa wafanyabiashara hao waweze kuhamisha na kubomoa mabanda yao ili kazi iliyopangwa ifanyike.

“Eneo hilo tunalimiki kihalali na tuna hati ya ardhi ya miaka 99, na kila muda tunalipia kodi ya ardhi, hivyo tunachowaomba waliojenga mabanda hapo waondoke ili kuweza kupisha wawekezaji wajenge ofisi na maegesho ya magari,” alisema Seiya.

Seiya alisema Masoko Kariakoo walikuwa wanamiliki viwanja namba 2000, 2001, 2002 na 2003, lakini kiwanja namba 2001 walikitoa ili ijengwe shule ya Esacs kutokana na agizo la Rais.

Aidha, aliwataka wafanyabiashara hao wasikimbilie kwa wanasheria kwa kufanya hivyo ni kujipotezea muda wao, na kutakiwa kuondoka ili kuwapisha wawekezaji waanze kazi.

“Tayari michoro kwa ajili ya ujenzi wa mahali hapo tunayo, lakini wanatukwamisha hao wafanyabiashara, lakini pamoja na kuwapa muda wa siku saba, wakili wao ametuomba tuwape muda kidogo ili wahamishe mali zao,” alisema.

Masoko Kariakoo wamechukua uamuzi wa kuwaondoa wafanyabiashara hao baada ya Waziri Tibaijuka kutaka maelezo ya siku 14 toka ndani ya shirika hilo waeleze watalifanyia nini eneo hilo.
 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment