Sunday May 1, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Tusiwatarajie malaika washuke kumsaidia JK

6th May 2012
Print
Comments

Rais Jakaya Kikwete ametangaza muundo na majina ya wajumbe wa Baraza la Mawaziri, huku kukiwa na tofauti ndogo ikilinganishwa na lililopita.

Mawaziri wengi waliokuwepo kabla ya Bunge kupendekeza, serikali iwashughulikiwe waliotajwa kwa ubadhirifu na wizi wa mali za umma, wamerejea.

Kwa sehemu kubwa, mawaziri waliotajwa kwa kashfa tofauti kule bungeni, kupitia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na ile ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, wamefukuzwa kazi.

Rais Kikwete hakutaka kupoteza hata sekunde moja ndani ya muda alioutumia kulisuka upya baraza, kupenyeza majina ya `watuhumiwa’ hao.

Safari ya Mawaziri Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Omar Nundu (Uchukuzi), William Ngeleja (Nishati na Madini), Mustapha Mkulo (Fedha) na Cyril Chami (Viwanda na Biashara) imefika tamati. Wamefukuzwa kazi.

Lakini hata waliokuwa Naibu Mawaziri, Dk Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii) na Athuman Mfutakamba (Uchukuzi) nao wamefutwa kulitumikia taifa katika nyadhifa hizo. Hawamo.

Akitangaza baraza hilo, Rais Kikwete akayataja majina mengine yaliyokuwa nje ya baraza hilo tangu aingie madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2005 na baadaye 2010.

Hata alipolivunja baraza hilo kutokana na kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa February 2008, majina mapya yaliyojitokeza sasa hayakuwemo katika serikali yake.

Msingi wake ni kwamba kama ilivyotokea mwaka 2008 na hatimaye hivi karibuni, kutangazwa kwa baraza jipya kulisababisha kuachwa kwa baadhi ya mawaziri. Hilo linaweza kuonekana ni jambo la kawaida.

Pili, mabadiliko yote yanafanywa baada ya kuibuliwa kwa kashfa chafu zenye taswira ya kuhujumu na kupora rasilimali za nchi.

Uhujumu na uporaji unafanywa na waliopewa dhamana ya uongozi, wakiwa katika nyadhifa za uwaziri!

Hata alivyotangaza majina ya mawaziri wapya na wale wanaoendelea, bado wanatoka katika chama kile kile, kuitumikia serikali ile ile iliyogubikwan na mitandao ile ile ikiwemo ya kifisadi!

Wateuliwa wapya, watafanikiwa vipi kupenya katikati ya mizizi iliyoimarika, ikipenya na ‘kuitafuna’ nchi katika sekta tofauti za maendeleo na ustawi wa jamii?

Jambo la msingi na linalostahili kuaminiwa ni kwamba umma usitarajie malaika washuke kutoka mbinguni, kuja duniani kwa ajili ya kumsaidia Rais Kikwete kutekeleza kazi na wajibu wake kwa umma.

Atawatumia wasaidizi wanaotambulika kwa mujibu wa Katiba ya nchi, kama ilivyo kwa mawaziri wanaotokana na kuwa wabunge wa majimbo, viti maalum ama kuteuliwa na Rais.

Kwa hali hiyo, watakaoutumikia umma katika baraza la mawaziri, watatokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), wataingia kwenye mifumo ya serikali ya CCM na kushirikiana na waliomo ndani yake.

Kama nguvu ya ufisadi itakuwa kubwa kuliko wanaojali maslahi ya umma, ni wazi kwamba ufisadi utajenga mkondo wake kiasi cha kuwafanya wasaidizi wa Rais kuipitia njia hiyo kwa wingi zaidi.

Wasaidizi wa Rais kwa sehemu kubwa ni mawaziri. Ndivyo tulivyoona na kushuhudia kwenye taarifa ya CAG na ile ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira.

Wametajwa mawaziri walioingia ndani ya CCM, ndani ya mifumo ovu ya serikali ya CCM wakachangamana na wasiokuwa waadilifu, wakawa sehemu ya wasiokuwa waadilifu, wakafanya kinyume cha uadilifu! Wamefukuzwa kazi.

Ingawa ni hivyo, hakuna sababu ya kukata tamaa, hakuna sababu ya kulalamika, hakuna sababu ya kufumba midomo, lazima umma uyamulike maeneo hatarishi kwa kuhujumiwa.

Umma ukimiliki rasilimali na mali za umma, umma ukiwa mlinzi wa rasilimali na mali za umma, umma ukisema `hapana’ kwa wezi na wahujumu wa rasilimali na mali za umma, utakuwa unamsaidia Rais Kikwete.

Kuliacha jukumu la kuwamuliki wezi na wahujumu wa rasilimali na mali za umma kuwa mikononi mwa Rais Kikwete pekee, ni sawa na kumuonea, ingawa yeye anahodhi mamlaka hayo kwa mujibu wa sheria.

Watanzania hawapaswi katika hatua hii, kuvunjika mioyo, kukata tama na kuliona baraza la mawaziri kuwa sawa lenye ‘watu wale wale’, ingawa ukweli huo haukwepeki.

Katikati ya mazingira yanayolindwa na Katiba iliyopo sasa, Tanzania haiwezi kulikwepa baraza la mawaziri kama alilolitangaza Rais Kikwete, kwa maana ametimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria.

Umma unapaswa kuzitambua na kuzilinda rasilimali na mali za umma. Wanaobainika kushiriki uhujumu ama aina nyinge ya ufisadi, apigiwe kelele, azomewe, akaripiwe kwa ustahimilivu wote, mpaka ang’oke.

Ndivyo ilivyofanyika wakati wa Mkutano wa Saba wa Bunge ambapo umma kupitia kwa wawakilishi wao bungeni, walipaza sauti, wakasema ‘imetosha’ na kweli ikatosha.

Kama jukumu walilolitekeleza wabunge lingeachwa mikononi mwa Rais Kikwete, kwamba CAG asingeibua uozo ule, Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ingenyamaza, wabunge wasingeunganisha nguvu zilizo kando ya itikadi za vyama, mabadiliko yasingetokea.

Kama asasi za kijamii zingeogopa mkono wa Dola na kushindwa kutimiza wajibu wake, vyombo vya habari ‘vingelala’ ili kukidhi matakwa ya magwiji wa kutoa vipande vya fedha, taifa lingeangamia.

Kwa hali iwayo yote, jamii izichukue changamoto zote zinazolikabili baraza la mawaziri, iwaibue na kuwaumbua mawaziri na watendaji wengine wasiofuata maadili ya utumishi wa umma, ili haki na usawa visimame. Isitarajiwe kwamba atatokea msaidizi zaidi ya umma wa Watanzania, umma unaochagizwa na kasi ya upashaji habari na taarifa zikiwemo za mabadiliko ya kijamii, kisiasa na kiuchumi kutoka mataifa ya nje.

Kila la heri baraza la mawaziri. Tunawasubiri.

Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE. Anapatikana kwenye simu namba +255 754691540, 0716635612 ama barua pepe: HYPERLINK "mailto:[email protected]" [email protected]

 

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles