Thursday May 5, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

CCM ijiandae kuipisha Chadema 2015

6th May 2012
Print
Comments
  Asema vijana wapewe nafasi kupigania rasilimali za nchi
Mzee Bob Makani (Kulia) akihojiana na mwandishi nyumbani kwake wiki hii

Wakati vuguvugu la kisiasa linavyozidi kushika chati nchini, ndivyo baadhi ya wanasiasa wakongwe wanavyotabiri hali ya baadaye ya nchi itakavyokuwa.

Huku vyama vingine vikionyesha kuwa na msuguano ndani yao, lakini vipo vingine vimeamua kujijengea utamaduni wa kuimarisha umoja na mshikamano, ingawa bado vinakabiliwa na changamoto kadha wa kadha.

Lakini vinajiimarisha ili kukabiliana na mazingira ya kisiasa na kujiweka vizuri kwa ajili ya kukubalika kwa wananchi na kupata ushindi wakati wa chaguzi mbalimbali.

Hali kama hiyo ndio ambayo mkongwe wa siasa nchini na muasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Bob Makani, ameamua kuiweka wazi baada ya kuibuka na vuguvugu la kisiasa hivi sasa.

Katika mahojiano na NIPASHE Jumapili, Makani aliyewahi kushika nafasi ya Katibu Mkuu wa Chadema wakati chama hicho kikianzishwa chini ya uenyekiti wa Edwin Mtei, anaelezea mambo mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi, mwenendo wa Chadema.

UIMARA WA CHADEMA

Kwanza Makani anaweka wazi msisitizo wake kwamba mafanikio yanayopatikana kwa Chadema yanafuta propaganda iliyonezwa awali kwamba kipo kwa ajili ya watu wa kanda ya kaskazini mwa nchi.

“Sasa hivi Chadema imekuwa chama kikuu cha upinzani, ni matokeo ya safari tuliyoianza na kurithisha kwa wengine, sasa hivi hakuna tena propaganda kwamba Chadema ni chama cha watu wa mikoa ya kaskazini,” anasema.

Baada ya kuitumikia Chadema katika wadhifa wa Katibu Mkuu, Bob Makani alichaguliwa kuwa Mwenyekiti, kufuatia kujiuzulu kwa mtangulizi wake, Mtei.

Makani anasema wakati chama hicho kinaanzishwa, kilikuwa kinaongozwa na Edwin Mtei ambaye ni mwenyeji wa moja ya mikoa ya Kaskazini.

Anasema kwa mantiki hiyo, kwa vile yeye (Makani) akiwa Katibu Mkuu akitokea mkoani Shinyanga, hapakuwa na sababu ya msingi kukitafsiri chama hicho kuwa cha watu wa Kaskazini.

“Lakini baada ya Mzee Mtei kuachia ngazi, nilichukua nafasi hiyo ya uenyekiti na kuongoza…sasa hao wanaoeneza propaganda kuwa Chadema ni chama cha kikabila, hawana ajenda nzuri na chama hicho,” anasema Bob Makani.

Makani anasema viongozi wa chama hicho wanachaguliwa vikaoni na wajumbe husika, na yule anayeonekana anafaa kuongoza ndiye anayechaguliwa kwa kupigiwa kura bila kuangalia ukabila wake.

SIRI YA USHINDI

Makani anasema Chadema inafanya vizuri kwa sasa katika chaguzi mbalimbali kutokana na mshikamano na umoja wake wanaouonyesha.

Anakitahadharisha Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichopo madarakani, kisishangae ikiwa hali ya mabadiliko yaliyopo sasa yataifanya Chadema kushinda Uchaguzi Mkuu ujao kwa urahisi.

“CCM ninawatahadharisha kwamba upepo wa Chadema ni mkali hivyo wakae tayari kukiona chama chetu kikiingia madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015,” anasema.

Anaongeza, “chama kipo pamoja, hakina majungu wala makundi…kinaendeshwa kwa umoja na mshikamano mkubwa na mtu yeyote anayeonekana anafaa kuongoza Chadema, ana haki ya kufanya hivyo iwapo vigezo na masharti vinazingatiwa.”

KASI YA VIJANA KWENYE SIASA

Makani anasema ni hatua nzuri kwa kundi la vijana wakiwemo wasomi kuingia katika nafasi za uongozi na unaharakati wa mageuzi kupitia vyama vya siasa.

Anasema hali hiyo inayojitokeza hasa kwa Chadema, inatoa haja ya kuwepo mifumo ya kurithishana nafasi za uongozi kwa kuzingatia Katiba na vigezo vilivyowekwa kwa kila taasisi.

Akasema “iwapo vijana wana sifa zinazofaa wana uwezo wa kuwania nafasi yoyote ndani ya chama, wafanye hivyo.

Makani anasema kuwepo kwa vijana ndani ya vyama vya siasa hakuna maana kwamba wazee hawatakiwi na hawapaswi kushika nafasi za uongozi.

UCHUMI

Makani anasema kwa sasa hali ya uchumi wa nchi ni mbaya sana, na hivyo kusababisha wigo mpana wa matabaka mawili tofauti; ya walionacho na wasionacho.

“Hawa ambao walionacho wanazidi kujiongezea zaidi kuliko wale ambao hawana, ambao nao (wasionacho) wanazidi kurudishwa nyuma kabisa kimaendeleo,” anasema.

Mbali na kukitumikia Chadema, Bob Makani amewahi pia kuwa Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.

Anasema licha ya serikali kushuhudia wananchi wake wakiporomoka kimaisha kutokana na kudorora kwa uchumi, lakini inashindwa kufanya jitihada za dhati kuwaokoa watu hao wanaoteseka na maisha.

Makani anasema, ndio maana mwelekeo wa uchaguzi kwa mwaka 2015, unaonyesha kabisa anguko la chama tawala huku wapinzani wao wakuu, Chadema wakiwa na nafasi kubwa ya kuchukua uongozi wa nchi.

“Utofauti wa kipato kwa walionacho na wasionacho, ndiko kunakosababisha kuona kwa sasa wanawake na vijana wengi kuamua kujitosa katika ulingo wa siasa, wakijiamini ndio wapiga kura wenye nguvu na walio wengi waliosahaulika,” anasema.

Aidha, anasema kuibuka kwa vijana katika siasa kumesababishwa na anguko la uchumi wa nchi, hivyo wao wakujitosa ili kuweza kuunusuru kwa kusimamia rasilimali za nchi zinazoibiwa na watu wachache na kuiacha nchi ikiwa ukiwa.

“Ni siri ya Chadema jinsi gani watakavyoshinda uchaguzi ujao…wananchi wameburuzwa kwa miaka mingi na CCM, lakini sasa wameamua kufunguka na kuelewa jinsi gani wanavyoumizwa na wachache,” Makani anaeleza.

KUJILIMBIKIZIA MALI

Muasisi huyo wa Chadema anasema licha ya kuwa na madaraka makubwa ya Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania kabla ya mfumo wa vyama vingina pia Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hakuweza kujipatia utajiri wowote na kuondoka akiwa maskini tofauti na viongozi wa sasa.

“Inauma sana kuona baadhi ya hawa viongozi wa serikali ya CCM wanadidimiza uchumi wa nchi yetu kwa kujilimbikizia mali, huku watu kila kukicha wanazungumzia ufisadi lakini serikali haizungumzi chochote,” anasema.

Mkongwe huyo wa siasa nchini anasema, kitendo hicho cha serikali kulifumbua macho suala la mafisadi wakati wanajulikana, ndilo jambo ambalo Chadema linawasumbua na hivyo kupita huku na huko kuelimisha wananchi.

“Chadema inawaelimisha wananchi kuhusu mambo mbalimbali ikiwemo jinsi chama tawala kinavyowasahau na kuwadidimiza kimaisha,” anasema.

KESI ZA UCHAGUZI

Makani ambaye kitaaluma ni Mwanasheria na Wakili, anasema kuibuka kwa kesi nyingi za uchaguzi kunatokana na changamoto ya kisiasa iliyopo hivi sasa nchini.

“Mtu yeyote aliyeshindwa lazima atalalamika iwe wa Chadema ama CCM. Ndio maana katika kupinga kwa matokeo ya kesi za ubunge, wabunge wa Chadema walipelekewa mahakamani na bahati nzuri wakashinda Sumbawanga na Singida,” anasema.

Makani anasema kufungua kesi kupinga malalamiko ya uchaguzi ni haki ya msingi ya kila mtu , kwani haki haipatikani mtaani bali lazima ipatikane kisheria ndani ya mahakama.

Akasema, kwa kutambua hilo Chadema imekuwa hairidhishwi na mwenendo wa baadhi za chaguzi zinazofanyika katika sehemu mbalimbali za nchi kwa ukiukwaji wa sheria, hivyo kukimbilia mahakamani pale panapoonekana pana kasoro.

KASI YA WABUNGE

“Kwa sasa tunashuhudia jinsi wabunge vijana wanavyoleta ushindani n dani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo lazima tubadilike na kuwapa nafasi ili waweze kuleta changamoto kwa nchi,” anasema Makani.

Makani anaeleza hiyo inatokana na vijana wengi kuathirika kiuchumi na umaskini unaowatawala miongoni mwao, hivyo kuamua kupata sehemu ya kusemea na kuwa wakali kwa serikali yao.

“Vijana wanatakiwa kupewa nafasi kwa sababu wameonyesha ni changamoto zaidi ndani ya Bunge.”

MTIZAMO

Anasema, “ inasikitisha kuona CCM imeingia katika matatizo makubwa ya kisiasa na kiuchumi, na kuamua kuwazibia masikio wananchi wanaogubikwa na matatizo lukuki.”

Hivyo, anasema iwapo CCM haitarekebisha mwenendo wake, lazima Chadema ichukue madaraka ya uongozi wa nchi katika uchaguzi ujao wa 2015 kutokana na watawala kuonekana kujineemesha wenyewe.

Kwa sasa Bob Makani ni mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu na Baraza Kuu la Chadema na pia ni mmoja wa wazee wa chama hicho ambaye hayupo tayari kuona chama kinapotea.

[email protected]

0715 006 970

0755 006 970

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles