Sunday May 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Milovan: Simba haijalewa 3-0 Sudan

10th May 2012
Print
Comments
Kocha wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic

Licha ya kusota kwa zaidi ya saa moja kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar es Salaam jana kutokana na kuchelewa kwa ndege yao ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ), kocha wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic amesema kuwa timu yake inakwenda kupambana jijini Sudan na haitabweteka na ushindi wa magoli 3-0 ilioupata katika mechi ya kwanza iliyofanyika jijini Dar es Salaam dhidi ya wapinzani wao Al Alhy Shandy.

Kikosi cha Simba ambacho kilitarajiwa kuondoka saa 9 alasiri kilisota uwanja wa ndege kwa zaidi ya saa moja ambapo walikuwa wakiambiwa "samahani kwa ndege kuchelewa" kabla ya kuondoka kuelekea Khartoum nchini Sudan kwa kupitia Nairobi, Kenya na siku ya mchezo Jumapili asubuhi ndio watakaelekea mjini Shandy.

Akizungumza na gazeti hili jana asubuhi, Cirkovic alisema kuwa wanafahamu kwamba wao ndio wanaingia uwanjani wakiwa mbele lakini kwenye soka ni lazima kupambana ili kulinda matokeo mazuri waliyonayo.

Cirkovic alisema kwamba somo walilolipata Algeria wakati wanapambana na ES Setif ndio linalowafanya waelewe kuwa ni lazima wacheze kwa juhudi kupata magoli mengine mapema ili kuwaweka wapinzani wao kwenye wakati mgumu.

"Tunakwenda Sudan kupambana na si kukamilisha ratiba, naamini tutaendeleza matokeo mazuri na kusonga mbele kwa kishindo," alisema kocha huyo.

Aliongeza kwamba kasi ambayo wachezaji wake wanayo ndio itaendelea kwenye mchezo huo wa kimataifa.
"Kawaida ukitoka kwenye matokeo mazuri timu huwa bora, kuifunga Yanga kwetu kumetuongezea hali ya kuamini kwamba sisi ni wapambanaji," aliongeza.

Nahodha wa Simba, Juma Kaseja, alisema kuwa wanakwenda Sudan kutafuta matokeo mazuri na wanaamini wachezaji watatimiza majukumu yao.

"Kila kitu kimekwenda vizuri, tunakwenda kupambana na kilichobaki ni kuombeana dua ili turejee na furaha," alisema Kaseja ambaye alikuwa ni mmoja wa wafungaji katika mechi dhidi ya watani wao Yanga iliyomalizika kushinda 5-0.

Wachezaji wa Simba walioondoka jana ni pamoja na Kaseja, Ally Mustafa 'Barthez', Shomari Kapombe, Derick Walulya, Amir Maftah, Juma Jabu, Obadia Mungusa, Kelvin Yondani, Victor Costa, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Patrick Mafisango, Haruna Moshi 'Boban', Salum Machaku na Uhuru Selemani.

Wachezaji wengine ni Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Edward Christopher Shija na Gervais Arnold Kago wakati viongozi ni pamoja na mwenyekiti wao, Ismail Aden Rage, Swedy Mkwabi (mjumbe), Cirkovic, Amatre Richard (kocha msaidizi), James Kisaka (kocha wa makipa), Cosmas Kapinga (daktari), Nicholaus Nyagawa (meneja) na Ezekiel Kamwaga ambaye ni Afisa habari wa klabu.

SALAMU ZA BMT
Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dionis Malinzi, jana aliwakabidhi Simba bendera ya nchi na kuwataka waende Sudan kupambana ili waweze kusonga mbele.

Malinzi kwa niaba ya serikali aliikabidhi Simba Dola za Marekani 3,000 ili ziisaidie timu hiyo ikiwa Sudan kununua mahitaji mbalimbali ikiwemo chakula cha wachezaji.

Kiongozi huyo alisema kuwa serikali hivi sasa inajipanga kuhakikisha inasaidia maandalizi ya timu zote za soka zitakazokuwa zinashiriki mashindano ya kimataifa kama inavyofanya katika michezo mingine.

Aliwaambia wachezaji kuwa huu ni wakati wao wa kuonyesha wanaweza na kuwataka viongozi nao watimize majukumu yao kikamilifu ili kuwaongezea morari wachezaji wao.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment