Wednesday May 4, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Kocha Papic hatimaye arejea kwao Serbia

11th May 2012
Print
Comments
Kocha wa mabingwa wa Kombe la Kagame, Yanga ya jijini Dar es Salaam, Kostadin Papic

Kocha wa mabingwa wa Kombe la Kagame, Yanga ya jijini Dar es Salaam, Kostadin Papic, alitarajiwa kuondoka nchini jana usiku na kurejea kwao Serbia, imefahamika.

Papic alifikia maamuzi ya kujiweka pembeni tangu Aprili 24 kutokana na mkataba wake wa kuifundisha Yanga pamoja na kibali cha kufanya kazi nchini kumalizika siku hiyo.

Akizungumza na gazeti hili jana mchana, Papic, alisema kuwa anaondoka lakini madai yake ya malimbikizo ya mishahara ambayo ni zaidi ya Sh. milioni 24 atayawasilisha katika Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) baada ya kuona Shirikisho la Soka Nchini (TFF) lilishindwa kumsaidia kwa muda wote aliowaeleza.

Papic alisema kuwa anaamini Yanga itaingia kwenye matatizo kwa sababu kushindwa kumlipa haki yake ni kinyume na makubaliano ambayo walisaini wakati anajiunga na timu hiyo.

Kocha huyo alisema kuwa jana mchana alitarajiwa kukutana na Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Sunday Kayuni, ambaye alikuwa anafahamu malalamiko yake lakini ilishindikana kutokana na kumueleza kwamba alikuwa amebanwa na majukumu.

"Baada ya kusikia kwamba naondoka ndiyo Katibu Mkuu (Selestine Mwesigwa) alisema niende nikachukue barua eti wanaahidi kwamba watanilipa, wakinipa sawa na wasiponipa nitaendelea na taratibu za kuwashitaki CAF na FIFA pia nitawajulisha," alisema Kocha huyo ambaye mwaka jana alirejea kuifundisha Yanga na kuufanya uongozi umtimue Mganda, Sam Timbe.

Aliongeza kwamba ameamua kurejea kwao kutokana na kuishi katika mazingira magumu jijini Dar na kubwa ni kukosa kibali cha kuishi nchini kama raia wa kigeni.

Mechi ya mwisho kocha huyo kuiongoza Yanga ilikuwa ni katika mchezo dhidi ya Polisi Dodoma iliyofanyika Aprili 21 mwaka huu ambapo waliibuka na ushindi wa magoli 3-1.

Papic alikuwa jukwaani akiiangalia timu yake ikipokea kipigo cha fedheha cha magoi 5-0 kutoka kwa watani zao Simba ambao tayari walikuwa wameshawavua ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu wa mwaka 2011/ 2012.

Mwishoni mwa mwaka jana Papic alizungumza na vyombo vya habari akilalamikia maandalizi ya zimamoto ya timu hiyo ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi na mashindano ya kimataifa akisema kuwa wachezaji wake hawajalipwa mishahara yao hivyo wasilaumiwe kwa matokeo yoyote yatakayopatikana.

Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga, alikiri klabu hiyo kudaiwa na Papic na kusema kuwa Kamati ya Utendaji iliyotarajiwa kukaa jana ilikuwa na mijadala mbalimbali ikiwemo kushughulikia madeni ya wachezaji na kocha huyo.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles