



Hatimaye Waziri wa Fedha jana alitangaza bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha wa 2012/13 ambayo imeweka bayana ongezeko la kodi katika maeneo mengi, ikiwemo yale ambayo yamezoeleka.
Maeneo haya ni ongezeko la ushuru kwenye vinywaji jamii ya soda, bia, mvinyo, pombe kali na kwenye muda wa maongezi wa simu za mkononi. Kadhalika, kampuni ambazo zilikuwa zinapata msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani sasa zitawajibika kulipa kodi hiyo kwa kiwango cha asilimia 10 badala ya asilimia 18 ambacho kinatozwa kwa sasa.
Mikakati hiyo pia imepunguza nafuu ya kodi kwa magari chakavu kutoka yenye umri wa miaka 10 hadi miaka minane; ambayo sasa yataendelea kulipiwa asilimia 20.
Kadhalika, Waziri huyo amependekeza viwango vipya vya kodi kwa wafanyabiashara kutoka ngazi nne za zamani na sasa zitakuwa tano, huku biashara yenye mzunguko wa Sh. milioni tatu wakisamehewa kodi.
Mipango hiyo pia imegusa kodi ya mapato ya kulipa kadri unavyopata (PAYE) na sasa kodi itaanza kutozwa kwenye Sh. 170,000 badala ya Sh. 135,000 za awali.
Pamoja na mipango mingine katika bajeti hiyo kama vile kusaidia uhakika wa chakula, nishati na kuongeza mitaji katika benki za uwekezaji, kwa muonekano bajeti hiyo bado inaonekana kugusa zaidi maeneo yale asilia ingawa mikakati ya kutoza kodi uuzaji wa hisa kwa kampuni za nje zilizowekeza nchini imeanzishwa. Kwa ujumla bajeti hii inaakisi kodi kwenye maeneo yaliyozoeleka ingawa imejaribu kugusa maeneo mengine mapya.
Kwa kitambo kirefu sasa, hali ya uchumi imekuwa siyo ya kuaminika sana. Mathalan, pamoja na takwimu kuonyesha kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la makusanyo ya mapato ya kila mwezi yakiwa yamefikia wastani wa zaidi ya Sh. bilioni 600 kwa mwezi bado hali ya maisha kwa wananchi wengi imezidi kuwa ngumu.
Mwenendo wa mfumuko wa bei ambao ndiyo chanzo kikubwa cha kuathiri uwezo wa wananchi kumudu maisha yao, umekuwa na athari hasi kwa kiwango kikubwa sana, kwani kila siku mpya inayokuja uwezo wa mwananchi wa kumudu mahitaji yake muhimu unapungua sana.
Katika bajeti hii serikali inakusudia kuweka mikakati ya kurejesha mfumuko wa bei kwenye tarakimu moja, huku nguvu zikielekezwa kupambana na uhaba wa chakula na bei ya nishati ambazo zinaelezwa kuchangia kwa kiwango kikubwa mfumuko huo.
Pamoja na bajeti hii kuonyesha juhudi za kutaka kugusa maeneo mbalimbali kwa nia ya kuongeza wigo wa kodi, bado hisia zimebakia kuwa vyanzo vya kodi vimeendelea kuwa vile vile. Hii inafanya shughuli nyingine za kiuchumi hasa ambazo siyo rasmi kuendelea kujineemesha huku nchi ikijengwa na kundi dogo la walipaji kodi wale wale mwaka baada ya mwaka.
Tunajua, hakuna nchi inayojengwa kwa siku moja, kwa maana hiyo tunaelewa kuwa pamoja na ugumu wa bajeti ya mwaka huu, bado umma ukiamua, kila mmoja akafanya kazi, ndani ya serikali uwajibikaji ukazingatiwa bila kulindana, tunaweza kupiga hatua.
Tunasema kuwa pamoja na vyanzo vya kodi kuwa vile vile mwaka baada ya mwaka, kuna tatizo kubwa sana la matumizi serikalini na hasa katika eneo la mishamaha ya kodi, kwani wiki hii tu Kamati ya Viongozi wa Dini iliweka wazi kuwa serikali imekuwa ikipoteza wastani wa Sh. trilioni 1.6 kwa mwaka kutokana na mwanya wa misamaha ya kodi, ukwepaji kodi na utoroshaji wa rasilimali nje ya nchi.
Tunachoomba kwa serikali ni kwamba hii ndiyo bajeti ya kwanza ya kuanza kutekeleza wajibu wake wa kubana matumizi, kuachana na kasumba ya kununua magari ya kifahari, kuachana na ugonjwa wa semina warsha na kwa ujumla kuhakikisha kwamba hata hiki kidogo kinachopatikana katika bajeti hii ya Sh. trilioni 15 fedha zinasimamiwa vizuri ili wananchi waone mabadiliko katika maisha yao.
Tunafikiri serikali ikijipanga, umakini ukatawala, kila mmoja akwajibika, nchi hii pamoja na malalamiko yoyote yanayoweza kuelezwa, tutapiga hatua.