Sunday May 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Vodacom ifute kadhia ya zawadi.

30th June 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Zawadi za washindi wa nyanja mbalimbali katika ligi kuu ya Bara msimu uliopita, imedaiwa zinataraji kukabidhiwa rasmi leo jijini Dar es Salaam na waliokuwa wadhamini wa michuano Vodacom.

Zawadi hizo, ambazo kimsingi zinalenga kutoa motisha kwa timu na wachezaji waliofanya vizuri katika shindano lililopita, zimechelewa mno hata hivyo na zinataraji kuchelewa zaidi.

Tunasema hivyo kwa sababu tuna uhakika, washindi mbalimbali wanaostahili tuzo hiyo baada ya kazi ngumu ya mwaka uliopita wa kisoka, watakabidhiwa vitita vyao katika 'mlio wa fedha" na si fedha zenyewe.

Uzoefu umeonyesha kuwa makabidhiano rasmi, ambayo ni kupiga picha mbele ya vyombo vya habari kwa lugha nyepesi zaidi, huwa ni katika mfano wa hundi.

Ni lini mifano ya hundi hiyo itageuka kuwa fedha halisi ndani ya akaunti za klabu na wachezaji binafsi? Kila mfuatiliaji wa ligi kuu ya Bara anafahamu kutokana na uzoefu uliopo.

Uzoefu uliopo ni kwamba si mapema, kwa vyo vyote, na hakuna uhakika wa kulipwa kwa fedha hizo na shirikisho la soka (TFF) kama ambavyo kisa cha mwaka jana cha mlinda mlango wa Yanga, Yaw Berko kinaweza kuwa picha halisi.

Viongozi wa klabu za Simba, mabingwa wa msimu uliopita, na Yanga wana picha inayofanana na ya Berko akilini.

Ni usumbufu wa kutosha kwamba zawadi za washindi wa ligi iliyokuwa imetengewa bajeti miaka mitano iliyotangulia zinapigiwa picha miezi miwili tangu kumalizika kwa shindano husika, Vodacom ni lazima itambue.

Lakini ni usumbufu pia, juu ya usumbufu huo wa kutosha, kwamba kitafuata kipindi cha msoto kwa klabu na wachezaji mpaka 'milio' hiyo ya fedha itakayorekodiwa na vyombo vya habari leo itakapokuwa fedha kamili.

Ndiyo maana, basi, tunachukua fursa hii kuziomba Vodacom, kama mdhamini wa ligi, na TFF kujaribu kutimiza jukumu lao kwa uadilifu ule ule ambao wadau wa ligi kuu ya Bara walitimiza kwazo kwa msimu mzima uliopita.

Vodacom na TFF zimekuwa na tabia ya kutupiana mpira kuhusu ucheleweshaji huu wa kila mwaka wa zawadi za washindi wa ligi kuu ya Bara licha ya malalamiko ya mara kwa mara ya viongozi wa klabu.

Ni kipi kinawezesha wenzetu, wakiwemo wa nyumbani kwa mwanahisa mkuu wa Vodacom kwa mfano, kutoa zawadi hizo punde baada ya kumalizika kwa ligi lakini hapa ikawa tatizo?  

Pengine ucheleweshaji huu si jambo la kuogopesha kwa taasisi hizo mbili. Pengine. Lakini zitaarifiwe, Vodacom na TFF, kwamba kadhia hii si tu ni maudhi kwa wadau wa soka la Bara bali pia ni moja ya viini vinavyosababisha kudorora kwa soka la nchi.

Haiwezekani mchezaji aliyejituma mwaka mzima na kustahili zawadi kutoka kwa wadhamini wa ligi kuendelea na moyo moyo ule ule wa msimu uliotangulia kama kile ambacho kilimsukuma kufikia mafanikio hayo atakipata si tu baada ya angalau miezi mitatu kupita bali pia kwa mbinde.

Fedha za zawadi za washindi si pambo klabuni, pia. Kama ambavyo baadhi ya viongozi wamekaririwa wakilia, baadhi ya klabu zilitaraji kutumia vitita hivyo kujiimarisha ili kutoa ushindani mkubwa zaidi msimu unaofuata kama huu wa 2012-2013.

Vodacom na TFF zitaona raha gani, kwa mfano, kama Simba na Yanga zisingekuwa na vyanzo vingine vya fedha za usajili, kwa mfano pia, kama mshindi wa msimu uliotangulia atabaki na mapungufu yale yale kama ligi mpya?

Bahati nzuri kwa Vodacom na TFF ni kuwa zipo katika mazungumzo ya mkataba mpya wa udhamini wa ligi kuu ya Bara.
Ndipo hapo pa kuhakikisha kuwa vipengele vya mkataba huo vinabana kote-kote ili washindi wapate zawadi zao ndani ya wiki mbili.

Hiyo italeta faraja kubwa na ari kwa washindi na wengine wanaowania ushindi siku za usoni.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment