Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Wafanyakazi wa benki kortini kwa kuibia wateja mabilioni

22nd May 2012
Print
Comments

Wafanyakazi sita wa Benki ya Stanbic, wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka 113 ya kula njama, kughushi na kuiba zaidi ya Sh. bilioni 1.3  kutoka katika akaunti mbalimbali za wateja na mwajiri wao.

Mmoja wa washitakiwa, Evance Komu, alipelekwa eneo la mapokezi ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na gari huku akisaidiwa kuteremka na kuingizwa kwenye chumba cha mahakama katika machela kutokana na kuwa na majeruhi ya ajali ya pikipiki.

Mshtakiwa huyo alipanda kizimbani na wenzake mbele ya Hakimu Mkazi Ritha Tarimo. Washtakiwa wengine ni Vicent Korosso, Frank Koko, Josemart Sanga, Uzzelotte Manyanga na Herieth Lema, wote ni waajiriwa wa Stambic Bank.

Wakili wa Serikali, Leonard Challo, alidai kuwa kati ya mwaka 2010 hadi Desemba 2011 katika benki hiyo, Kinondoni jijini Dar es Salaam washtakiwa walikula njama ya kutenda kosa la wizi, kughushi na utakatishaji wa fedha haramu.

Alidai kuwa washtakiwa walikula njama ya kuiibia benki hiyo kati ya Januari, 2010 na Desemba 2011 kwa kujiingizia salio katika kaunti zao, kuacha kuingiza ingizo sahihi katika akaunti za wateja na kuiba.

Challo alidai kuwa Korosso, Komu, Koko na Sanga ambapo kwa nyakati tofauti waliacha kuingiza ingizo sahihi katika akaunti za wateja mbalimbali waliofika kuweka fedha zao kwenye benki hiyo, walijiingizia fedha hizo katika akaunti na kumwibia mwajiri wao huku wakijua ni makosa kufanya hivyo.

Ilidaiwa kuwa washitakiwa waliiba Sh. 127,495,484.93, Dola 709,925.9 za Kimarekani na Euro 29,009.34 zilizokuwa zikiingizwa na wateja katika akaunti zao, badala ya kuziingiza kama zilivyowekwa walikuwa wakihamishia katika akaunti zao na kisha kuzitoa kwa kutumia vitambulisho vyao.

Shitaka la 112 linamkabili mshitakiwaManyanga ambaye ni Meneja wa benki hiyo na Mtunza mali wa benki hiyo, Lema wanakabiliwa na shitaka la uzemba wa kushindwa kubaini makosa hayo yalipokuwa yakifanyika.

“Mshitakiwa wa kwanza, Korosso, mshtakiwa wa pili, Komu, wa tatu, Koko na wa nne, Sanga wanakabiliwa na shtaka la 113 la kutakatisha fedha kati ya Juni, 2010 na 2011...Washtakiwa walikutwa na Dola za Marekani, 417,225.72 katika akaunti namba 0296000236611 huku wakijua zilikuwa za wizi,” alidai Challo.

Washitakiwa walikana na upande wa mashitaka ulidai hawana pingamizi ya dhamana kwa Manyanga na Lema, lakini washtakiwa wengine walinyumwa dhamana kwa sababu mashitaka ya kutakatisha fedha yanayowakabili hayana dhamana kisheria.

Wakili wa utetezi, Daudi Malima aliiomba mahakama kulifuta shitaka la kutakatisha fedha kwa madai kwamba halina msingi kwani maelezo yake hayaonyeshi yametokana na shitaka lipi.

Hata hivyo, wakili Challo alidai maombi ya utetezi hayapo kisheria kwani kosa hilo wanaweza kulithibitisha wakati ukifika na shtaka halali linastahili kuwepo hapo hivyo aliomba Hakimu Tarimo kuyatupilia mbali maombi ya kufuta shtaka hilo.


SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment