


Wafanyakazi wa Hospitali Teule ya Bunda mkoani Mara, wamefanya mgomo wa siku kadhaa na kulilazimisha Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) mkoani hapo kumuondoa madarakani Daktari Kiongozi wa hospitali hiyo, Dk. Said Karamba.
Kufuatia mgomo huo wagonjwa waliolazwa na wanaopata huduma katika hospitali teule ya Bunda mkoani Mara, walikosa matibabu kufuatia mgomo wa wafanyakazi wa hospitali hiyo wanaotaka Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, awajibike.
Wagonjwa hao kwa siku mbili mfululizo kuanzia Alhamisi na Ijumaa walikosa kuhudumiwa kwa saa kadhaa kutokana na madaktari, wauguzi na wafanyakazi wengine kugoma kuingia mawodini wakimtaka daktari kiongozi wao ajiuzulu wadhifa wake kwa madai kuwa hawatendei haki.
Habari kutoka hospitalini hapo zilisema juzi wafanyakazi wote wa hospitali hiyo waliitisha kikao cha pamoja na kumtaka Katibu Mkuu wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Mara, Robert Kaunda, kukutana nao ili kusikiliza kilio chao.
.Hata hivyo hadi saa 12:00 jioni katibu huyo hakuonekana jambo lililowapandisha hasira wafanyakazi hao.
Kufuatia hali hiyo wagonjwa wakiwemo waliozidiwa wakiwa wamepangiwa kufanyiwa upasuaji, waliendelea kutaabika kwa kukosa huduma, huku madaktari na wauguzi wakisema mpaka kieleweke kwa kumtoa daktari kiongozi wa hospitali hiyo,
Hadi jana asubuhi wafanyakazi hao walikusanyika ukumbini na kuzidi kumsubiri katibu mkuu huyo pamoja na Dk. Karamba mtuhumiwa aliyesababisha mgogoro, na kwamba waliwasili saa 3:00 na kukutana na wafanyakazi saa 8:00 mchana na kuazimia kumuondoa kiongozi huyo kwenye wadhifa wake.
Wafanyakazi hao walisema hawana imani na daktari huyo, kwa sababu anatumia madaraka yake vibaya, ikiwa ni pamoja na kuwapangia kazi zisizo wahusu, kuwahamisha kwenye idara, kutoa kauli na lugha chafu kwa wafanyakazi zikiwemo za kuwatishia kuwafukuza kazi au kuwafanyia mambo mabaya.
Katibu Mkuu Dayosisi Mkoani Mara, alisema uongozi umechukuwa jukumu la kumuondoa kwenye nafasi yake Dk Karamba na kwamba utaratibu wa kuteua daktari mwingine kiongozi utafanyika, ikiwa ni pamoja na kuteua mwingine kukaimu nafasi hiyo kwa muda.