Thursday Jun 20, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Mkono: Sina muda wa kulumbana tusubiri 2015

19th March 2012
Print
Comments
Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono

Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono, amesema hana muda wa kulumbana na watu na wanaotaka kuongoza jimbo hilo wasubiri uchaguzi mkuu wa 2015.

Akijibu habari zilizochapishwa na baadhi ya magazeti juzi kupitia kwa George Marato, ambaye ni msemaji wake binafsi wa masuala ya jimbo, Mkono alisema baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu, wanasiasa hao hasa kutoka katika chama chake (CCM), wamekuwa wakiendeleza malumbano ambayo hayawasaidii wananchi katika kuharakisha maendeleo yao.

“Kura za maoni zilipigwa mwaka 2010 nikawashinda vibaya na uchaguzi mkuu tulishamaliza. Sasa leo wanaendelea na malumbano yote haya ya nini? Kwanini wasijipange tukutane mwaka 2015...twende kwa wananchi wakayaseme hayo sio katika magazeti,” alisema.

“Kuna mtu anasema nimepeleka maendeleo katika kata yangu eti nimeacha kata nyingine. Je, ni kwanini nilishinda hata katika kata yake kama wananchi na wanaCCM hawakuridhika na utendaji wangu, nawashauri wenzangu kutambua kuwa sasa ni wakati wa kutekeleza ilani na kama wana mchango hata wa mawazo, waulete katika kuharakisha maendeleo ya wananchi wetu,” alisisitiza.

Hata hivyo, akijibu hoja kwamba amekuwa akitumia fedha za wafadhili kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika jimbo hilo, Mkono alisema si jambo baya kutumia fedha za wafadhili kufanya hivyo lakini pia aliwaambia wanasiasa kuwa milango iko wazi kwa kila mtu kuwaomba wafadhili fedha za kufanyia maendeleo.

Akifafanua kauli yake kuwa mbunge wa milele katika Jimbo la Musoma Vijijini, Mkono alisema hawezi kuwa na hatimiliki ya ubunge wa jimbo hilo kwa vile wenye maamuzi ni wananchi na ndio watakaopima mchango wake.

Aliwataka wanasiasa hao kutambua kuwa wana wajibu wa kuwasaidia wananchi wa jimbo hilo kama walivyokuwa wakiahidi wakati wa kura za maoni mwaka 2010, jambo ambalo litawezesha kuaminika kwa wananchi na wana CCM.

“Leo Musoma Vijijini iko katika ramani inafikika kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma, shule zimejengwa kama njugu, barabara zinapitika hadi kwenye vitongoji, zahanati zimejengwa na sasa kazi yetu ni kujenga nyumba za walimu kwa kasi, shule za awali huku tukielekeza nguvu zetu katika ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere. Je, hapo unasema Washington DC haiwezekani?,” Alihoji Mkono.

Chadema wamshangaa Mkono.

Wakati huo huo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeelezea kutostushwa na kauli ya Mbunge wa Musoma Vijijini mkoani Mara, Nimrod Mkono, kuwa hawezi kuiacha nafasi hiyo mpaka kifo kitakapomchukua.

Katibu wa Chadema katika halmashauri ya Musoma Vijijini, Richard Magori Choge, aliiambia NIPASHE jana kwa njia ya simu kuwa, vitendo vya kung'ang'ania madarakani ni moja ya hulka kuu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo Mkono ni mwanachama wake.

Akizungumza katika kijiji cha Mwibagi jimboni humo hivi karibuni, Mkono alikaririwa akisema hana mpango wa kuacha kuwania nafasi hiyo mpaka atakapofariki ama kufa.

 “Hatumshangai Mkono kwa maana ni hulka ya watu wa CCM kung'ang'ania madaraka isipokuwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyestaafu kwa hiari yake,” alisema.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment