


Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) limewateua waamuzi kutoka Rwanda kuchezesha mechi ya raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho baina ya Simba na ES Setiff ya Algeria Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Simba imefika hatua hiyo baada ya kuifunga Kiyovu ya Rwanda jumla ya magoli 3-2.
Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), aliwataja waamuzi watakaochezesha mchezo huo kuwa ni Hudu Munyemana atakayesaidiwa na Felicien Kabanda na Theogene Ndagijimana huku Edouardo Bahizi akiwa mwamuzi wa akiba.
Wambura alisema CAF imempanga, Felix Tangawarima, kutoka Zimbabwe kuwa kamishna wa mchezo huo.
Alisema kuwa mechi ya marudiano kati ya ES Setiff na Simba itachezwa Aprili 6 jijini Algiers nchini Algeria na mshindi wa mechi hiyo atakutana na El Ahly Shandy ya Sudan au Ferreviario de Maputo ya Msumbiji mwishoni mwa mwezi Aprili.
Simba ndio wawakilishi pekee wa nchi waliobakia kwenye mashindano yanayoandaliwa na CAF baada ya Yanga ya Bara na timu mbili za Zanzibar kutolewa kwenye hatua ya awali.