



Makampuni 21 kati ya 60 kutoka nchi za Afrika Mashariki yamefanikiwa kuingia katika kinyanganyiro cha kupewa tuzo kwa kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo ya jamii.
Mkuu wa Ushirikiano wa Benki M, Ambrose Nshala, alisema tuzo hizo zitatolewa Aprili 17, 2012 ambazo zimeshirikisha nchi za Afrika ya Mashariki pamoja na makampuni.
Alisema tuzo hizo ambazo zimelenga katika nyanja za afya mazingira,uchumi na mambo mengine ya kijamii, zimeandaliwa na benki hiyo kwa kushirikiana na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC).
Aidha Nshala alisema tuzo hizo zijulikanazo kwa jina la CSR ni mara ya pili kufanyika nchini ambapo alisema kampuni nyingi zimeitikia wito wa kushiriki ukilinganisha na kipindi kilichopita.
“Tuzo hizi zinalenga kuhamasisha makampuni mbalimbali kusaidia miradi ya maendeleo kwa jamii katika nyanja mbalimbali tunaomba mwaka ujao kampuni nyingi zijitokeze zaidi,” alisema Nshala.
Alisema baada ya makampuni mengi kutuma maombi hayo, walikaa majaji na kufanya mchujo na kuchagua makampuni hayo kwa kuzingatia vigezo mbalimbali.
Baadhi ya kampuni zilizoingia katika kinyanganyiro hicho ni Coca-Cola, Vodacom Tanzania Ltd, kupitia huduma yake ya M-Pesa,Tigo, Benki ya Exim, Swissport na Serengeti.