Thursday Nov 26, 2015
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Amani ya Zanzibar itumike kutengeneza ajira kwa vijana

17th June 2012
Print
Comments

Waswahili wamekuwa na msemo kuwa vijana ni Taifa la kesho, ingawa neno hilo linapingwa na wanaoamini kuwa vijana ni taifa la leo.

Vijana ni nguvu kazi ya Taifa na wengi wanaamini kama watatumika vizuri malengo ya kuondoa umaskini na kupiga hatua za maendeleo.

Tofauti ya mtazamo huo, imekuwepo changamoto inayojengeka na kuwaumiza vijana wengi ambao wanaishi bila ya ajira na kusababisha Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Zanzibar (MKUZA) kuendelea kutekelezwa katika mwendo wa kuchechemea.

Changamoto hiyo inahusu hali ya kundi kubwa la vijana visiwani Zanzibar kutokuwa na ajira zilizo rasmi.

Hali hiyo imechangiwa na vijana wengi kukosa mitaji na nyenzo za kufanyia kazi, hivyo kuwafanya washindwe kujiajiri katika sekta isiyoa rasmi, hivyo kusababisha kuzorotesha harakati za kupambana na umasikini.

Hata hivyo, msemo wa vijana ni Taifa la kesho umekuwa ukitetewa hasa na wazee waliofikia umri wa kustaafu, lakini bado wamo katika ajira za mikataba wakati zaidi ya wasomi 3,000 wakiwa hawana ajira visiwani humo.

Tatizo la ajira linaaminika kuwa chanzo kwa baadhi ya vijana kujiingiza katika vitendo visivyofaa kama matumizi ya dawa za kulevya, ukahaba, uhalifu na wakati mwingine kulazimika kutumiwa na wanaharakati na wanasiasa kwa maslahi binafsi.

Hata hivyo serikali ya awamu ya saba visiwani Zanzibar, imeamua kufanya mageuzi katika sekta ya kilimo kwa kuanzisha kilimo cha kisasa cha umwagiliaji, na program maalum ya kuwawezesha vijana kushiriki moja kwa moja katika shughuli za kiuchumi.

Hatua ya serikali kutangaza mpango huo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013 imeleta faraja kwa kundi la vijana hasa wasiokuwa na ajira rasmi, hivyo kusababisha lengo la MKUZA kutofikiwa kwa muda muafaka.

“Serikali imeandaa programu maalum ya kuwawezesha vijana katika shughuli za kiuchumi ikiwemo uvuvi, kilimo, kazi za usafi wa maji, ujasiriamali na utalii,” anasema Waziri wa Fedha na Uchumi, wakati akiwasilisha mpango wa bajeti ya serikali.

Hatua ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuwasilisha mpango huo inastahili kuungwa mkono na wananchi, kwa vile mafanikio yake yatatokana na vijana kuacha kuchagua kazi badala yake kuanzisha vikundi vya ushirika ili waweze kunufaika.

Ukweli usiopingika ni kwamba soko la ajira katika sekta ya umma na binafsi bado halilingani na mahitaji na programu ya mpango huo.

Lakini itasaidia kuondoa kilio cha tatizo la ajira kama serikali itawapatia nyenzo vijana na kuweka mazingira mazuri ya ujasiriamali kama kuanzisha viwanda vya samaki katika maeneo ya visiwa vya Unguja na Pemba.

Pamoja na Zanzibar kuzungukwa na bahari, kasi ya uwekezaji katika sekta ya uvuvi wa bahari kuu bado ni ndogo kutokana na kukosekana kwa kiwanda hata kimoja cha samaki.

Kunahitajika mkakati maalum kukaribisha wawekezaji katika sekta hiyo.

Sekta ya uvuvi na kilimo bado zina nafasi kubwa ya kupambana na tatizo la umaskini, mathalani kilimo, inategemewa na asilimia 70 ya wananchi katika maisha ya kila siku wakati sekta ya uvuvi imekuwa tegemeo kubwa licha ya wavuvi kuendelea kutumia nyenzo zisizokuwa na tija.

Bahati mbaya, Zanzibar imeendelea kutegemea sekta ya utalii na zao la Karafuu baada ya sekta ya biashara na viwanda kuyumba na kusababisha ukubwa wa tatizo la ajira kwa vijana visiwani.

Hatua ya serikali kuanzisha shughuli maalum za kuwasaidia vijana kupata ajira ni jambo muafaka, lakini jamii inahitaji kudumisha hali ya amani ili wawekezaji waweze kujitokeza na kuwekeza na kuanzisha vitega uchumi katika sekta ya viwanda na uvuvi wa bahari kuu.

Nchi yoyote iliyopiga hatua kubwa ya maendeleo imetokana na kuimarika kwa amani na umoja wa kitaifa kwa wananchi wake hivyo wananchi hawana budi kuendelea kuenzi misingi ya amani iliyojengwa na Serikali ya Umoja wa kitaifa Zanzibar.

Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya vijana watano wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 24 visiwani humo, mmoja hana kazi.

Sekta ya uwekezaji bado ni mkombozi mkubwa katika kupambana na tatizo la umasikini kama wawekezaji watajitokeza wakiwemo wazalendo ambao wamekuwa wakitumia bidhaa nyingi kutoka nje ya nchi.

Hatua ya wafanyabiashara wazalendo kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya ndani pia kuna umuhimu kwa wafanyabiashara wazalendo kuunga mkono uwekezaji katika sekta hiyo ili kuongeza kasi ya kuondoa tatizo la ajira na kuongeza pato la Taifa.

Kutokana na sekta ya utalii kuonyesha matumaini makubwa kwa kuchagia asilimia 80 ya fedha za kigeni na asilimia 27 ya pato la Taifa, muhimu Chuo cha Maendeleo ya Utalii Zanzibar kikaboreshwa.

Hata hivyo malengo ya kuondoa umasikini na kukuza uchumi yatafikiwa iwapo SMZ itafanya kazi kama timu moja katika kuimarisha amani na umoja wa kitaifa kwa wananchi wa visiwani humo.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment