


Unapotaka kifupisho cha EPA ndani ya mipaka ya Tanzania, walio wengi wanazielekeza fikra zao katika vita dhidi ya ufisadi, wakiielekea Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) iliyokuwa chini ya Benki Kuu (BoT).
Wapo wachache wanaotambua, ikilinganishwa na wasiotambua kwamba upo mchakato wa kutaka kusainiwa Mkataba wa Ushirikiano na Makubaliano ya Kiuchumi (EPA) kati ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Ulaya (EU).
Mkataba huo ndio EPA inayojadiliwa katika makala haya, ikimhusisha Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa.
ASILI YA EPA
Septemba 2011, Kamisheni ya Ulaya ilipendekeza kurekebishwa kanuni 1528/2007 ya Kamisheni ya Ulaya, lengo likionesha viashiria vya kulipendelea bara hilo lililopiga hatua kubwa za maendeleo.
Hivi sasa kanuni hiyo inatoa nafasi ya kwanza kwa nchi za Afrika, Caribbean na Pacific (ACP), kuondolewa kodi na ushuru ili kulihimili soko la Ulaya.
Hatua hiyo inafanyika wakati ambapo mataifa yaliyo chini ya ACP yapo kwenye majadiliano na Ulaya ya kupata muafaka kuhusu EPA.
Masuala yaliyomo ndani ya EPA kwa asili, yanahusisha moja kwa moja uhuru wa kufanya biashara, hapo ndipo Mkapa anapojenga hoja tofauti akikosoa mchakato huo.
Lakini mapendekezo ya kutaka marekebisho kwa kadri yaliyovyowasilishwa Septemba 2011, yanahusisha kuondolewa kwa fursa zilizopo kwa nchi za ACP ikiwa ifikapo Januari Mosi, 2014, hazikuwa zimeridhia mkataba wa EPA.
Lakini EU ilizidi kuzibana nchi za ACP ikitoa ukomo wa kusaini na kuridhia mkataba wa EPA kufikiwa ifikapo Juni mwaka huu. Hadi naandika makala haya, sina hakika ni hatua gani zimefikiwa kwa vile muda huo umeshapita!
Ingawa ni hivyo, Kamisheni ya Ulaya iliweka wazi tangu awali kwamba ‘msamaha’ wa kodi na ushuru kwa nchi za ACP vitaondolewa ifikapo Januari Mosi, 2014.
Kwa hali hiyo, nchi kama Kenya, Namibia, Botswana, Swaziland, Ghana, Ivory Cost, Cameroon zitashuhudia bidhaa zao kama maua, nyama, sukari, kahawa, ndizi miongoni mwa nyingine, zikitozwa kodi na ushuru mkubwa, zitakapoingizwa Ulaya.
Ikiwa itafikiwa hatua hiyo, ni dhahiri kwamba bidhaa hizo na nyingine kutoka Afrika (mathalani) hazitamudu ushindani wa soko. Zitadoda!
Mkapa anaielezea tangu awali, ikiwemo katika makala aliyoichapisha kwenye gazeti la Daily News la Mei, 4 mwaka huu, yakiwa na kichwa kinachosema, “Mkataba wa Ushirikiano na Makubaliano ya Kiuchumi kati ya Umoja wa Ulaya na nchi za Afrika.”
KASORO ZA EPA
Mkapa anasema upungufu anaouona katika vipengele vya EPA ni pamoja na kuwepo ishara zenye athari kubwa kwa uwezo wa nchi za Afrika kukua na kufikia kuwa zenye uchumi unaotegemea viwanda.
Akinukuu utafiti uliofanywa na taasisi ya Kituo cha Kusini mwa Afrika, Mkapa anasema mazao ya ndani yanayokabiliwa na hatari zinazotokana na makubaliano yaliyoainishwa kwenye EPA ni pamoja na mahindi, mbegu za nafaka, ngano na chakula cha mifugo.
Kwa upande wa bidhaa za viwanda vya ndani anazitaja kuwa ni pamoja na dawa za binadamu (chanjo, antibayotiki, vitamin), kemekali kama mbolea, vifaa vya usindikaji ikiwemo karatasi, vifaa vya chuma na shaba, vinavyoweza ‘kumezwa’ na zinazotoka Ulaya.
Mkapa anaainisha kuwa vipengele vingine vinavyokera katika EPA ni uhalisia wa bidhaa kwamba lazima zitoke nchi husika, kuondoa kodi kwa bidhaa zinazoingia nchini na zinazopelekwa nje na kutoziwezesha nchi zitakazosaini makubaliano hayo.
“Hili suala la kushinikiza kuondoa kodi kwa bidhaa zinazoingia ama kwenda nje ya nchi, kutachangia kudidimiza pato letu na kuua viwanda vyetu, binafsi nawaona hawa wenzetu (EU) si rafiki zetu, wanataka huu mkataba uwanufaishe wao,” anasema.
MATUMAINI MAPYA
Mkapa anasema pamoja na hali hiyo, yapo matumaini yanayotokana na Kamati ya Maendeleo (DEVE) ya Bunge la Ulaya ambapo Aprili 3, mwaka huu ilikataa pendekezo la EU kukata ‘misamaha’ kwa nchi za ACP ikiwa zitashindwa kusaini na kuiridhia EPA.
DEVE inaeleza kuwa muafaka kuhusu EPA unapaswa kufikiwa kwa pande zote kushiriki majadiliano yenye kujali maslahi husika na isiwe kwa kuwekewa kikwazo cha ukomo wa muda.
Mbali na DEVE, Kamati ya Bunge la Ulaya ya Biashara ya Kimataifa (INTA) yenye nguvu kubwa kwa masuala ya biashara , ilitoa pendekezo lake Aprili 13, mwaka huu, ikipendekeza kuongezwa muda wa utekelezaji wa marekebisho yanayohusu kusaini na kuiridhia EPA kutoka mwaka 2014 hadi 2016.
Kwa upande wake, Seneti ya Ubelgiji ilipitisha azimio lake Machi 13, mwaka huu, likitaka Jumuiya ya Ulaya kutambua msimamo wa kati iliyonayo, hivyo kuiagiza Kamisheni ya Ulaya isiwasilishe mapendekezo yake kuhusu EPA kwa Bunge la Ulaya.
USHIRIKIANO WA KIKANDA
Mkapa anasema nchi za Afrika kupitia jumuiya za kikanda kama Afrika Mashariki (EAC), zinapaswa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi ili kukuza masomo na uchumi wao.
Kwa mujibu wa Mkapa, nchi za Afrika zinapaswa kuufanyia kazi mbadala uliotolewa na Umoja wa Afrika na kuridhiwa na Wakuu wa nchi hizo Januari mwaka huu.
Kwamba EU inapaswa kuondoa kodi na ushuru si kwa nchi zinazoendelea zikiwa na uchumi mdogo tu, bali na zile zinazoendelea zenye uchumi unaokua, lakini zipo kwenye kanda zenye umoja wa forodha.
Kwenye ukanda wa Kusini mwa jangwa la Sahara, nchi nyingi zinazoendelea zenye uchumi mdogo, hazina wigo mpana wa tofauti na nchi zinazoendelea zikiwa na uchumi unaokuwa.
Nyingi miongoni mwa nchi zenye uchumi mdogo zinaweza kupata hadhi ya nchi zenye uchumi unaokua kama zikihitaji kufikia hadhi hiyo.
Mkapa anasema matokeo hasi ya EPA yataathiri ushirikiano wa kikanda hususani katika nyanja za biashara, huku ikiharibu Umoja wa Forodha.
“Hivyo tunaamini kwamba EU itatilia mkazo mapendekezo ya nchi za Afrika na ACP ili kuwepo ushirikiano wenye tija kwa pande zote,” anamaliza Mkapa kupitia makala hayo.
Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE. Anapatikana kupitia namba +255 754 691540, 06716635612 ama barua pepe: mgeta2000@yahoo.com.