Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Kikwazo cha fursa kwa raia Mtwara

25th March 2012
Print
Comments

Jumapili iliyopita, safu hii ilielezea undani wa tatizo la uvuvi wa haramu wa kutumia baruti unavyofanyika mkoani Mtwara. Mwandishi wa makala haya aliyefanya ziara ya mkoani humo kwa udhamini wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) anaeleza zaidi.

Wananchi wa Mtwara wanategemea samaki kwa kitoweo, ambapo ili kufanikisha hilo, ununuzi na uuzaji samaki unakuwa sehemu ya shughuli zenye kukuza kipato na kuboresha hali ya uchumi.

Kwa hali hiyo, ukosefu wa samaki wa kutosha, unatajwa kama sehemu ya kupunguza ushiriki wa idadi ya wafanyabiashara wa bidhaa hiyo, lakini na walaji pia, kwa maana bei yake inapanda na kuwa kubwa kuliko vitoweo vingine.

Abass Salum Waziri (40) ni mmoja wa watu walioshiriki uvuvi halali kwa zaidi ya miaka 5, lakini sasa amebadili mwelekeo kutokana na changamoto zilizopo baharini, ikiwemo upatikanaji duni wa samaki.

Waziri anasema hivi sasa mvuvi anatumia nguvu nyingi kwenda na kuvua baharini, lakini kiasi cha samaki anachokipata ni kidogo. Hivyo ameamua kufanya biashara ya uchuuzi wa samaki.

Hivi sasa samaki hawazaliani kwa wingi kama ilivyokuwa miaka 10 iliyopita, ukiingia baharini unatumia nguvu nyingi kuliko bidhaa unayoipata, baadhi ya wavuvi hawafanyi shughuli hiyo kwa sasa nikiwemo mimi,” anasema.

Mmoja wa watu waliowahi kushiriki uvuvi haramu, lakini sasa hashiriki uvuvi wa aina yoyote, anasema matumizi ya baruti ni hatari kwa mazingira ya bahari, rasilimali zake na watumiaji.

Mtumiaji baruti huyo ambaye hata hivyo anaomba jina lake lihifadhiwe kwa vile alishajisalimisha na kutangaza wazi kutoshiriki uvuvi huo, anasema kwa kawaida mlipuaji baruti anashika bomu mkononi na kuzama nalo chini ya maji, kiasi cha mita 20.

Anasema kwa kawaida mabomu huelekezwa umbali wa kile kinachojulikana kwa watumiaji kama pima (pengine ni kama mita). Zinakuwa kati ya moja na hadi kumi kutoka eneo lenye samaki ama mazalia yake.

“Tulipofika hapo tulikuwa tunatupa baruti yenye utambi unaowaka hadi ndani ya maji, kisha tunaelea kurejea juu kwa kasi ili kuepuka mlipuko,” anasema.

Kwa mujibu wa ‘mvuvi haramu’ huyo, baada ya muda baruti kulipuka kwa mshindo, maji yanapanda juu na kuwa ishara kwao, ndipo wanapokwenda na nyavu kwa ajili ya kuvua.

Anasema samaki wanaoathiriwa kwa baruti hufa kwa haraka na wengine kupasuka. Wanaovuliwa wakiwa hai huathirika na kuwa na alama kama mabaka.

Baruti zinapolipuliwa, ‘mvuvi haramu huyo’ anasema zinabomoa makazi ama mazalia ya samaki maarufu kama matumbawe, ambayo kwa asili hayajengeki tena.

Baruti zinazotumika kwa uvuvi haramu zinatengenezwa kwa kutumia mbolea ya chumvi chumvi inayohifadhiwa kwenye chupa ya maji ya kunywa yenye ujazo wa mililita 300, ikifungwa na jiwe dogo, futo jeusi na kuwekwa kibati maalum na utambi usizimike hata unapokuwa kwenye maji.

Baruti inapokamilika kutengenezwa kwa njia za asili, inauzwa kwa seti kati ya Sh 18,000 hadi 20,000. Wakati mwingine inakuwa juu zaidi kutokana na kupanda kwa idadi ya wahitaji.

Anasema katika kipindi cha ushiriki wake uvuvi haramu, amewahi kushuhudia watu waliokatika vidole vya mikono kutokana na kujeruhiwa na mabomu ya baruti, ingawa inasadikiwa kuwa matumizi ya baruti yanaweza kusababisha vifo.

Lakini Waziri ambaye hajawahi kufanya uvuvi wa kutumia baruti, anasema wahusika wa kadhia hiyo wanatumia sababu kadhaa, ikiwemo ukosefu wa njia mbadala za kujipatia kipato na kukuza uchumi wa familia zao.

“Ninadhani kama pangekuwa na mkakati wa kulishughulikia tatizo la uvuvi wa kutumia baruti kwa kuibua njia mbadala za kujipatia kipato, nadhani tatizo hilo lisingefika hapa lililopo,” anasema.

Msako wa wavuvi haramu

Waziri anasema misako inayofanywa kupitia doria za majini na nchi kavu zinafaa, lakini si njia muafaka ya kupata suluhu endelevu ya kudhibiti uvuvi wa kutumia baruti.

“Wanaofanya doria ni binadamu wakiwasaka binadamu wenzao, sasa hapo yapo mambo katikati yake na ambayo yanaweza kukwamisha nia njema,” anasema.

Hivyo Waziri anashauri kufanyika kwa mpango wa utoaji elimu kuhusu madhara ya uvuvi huo, huku kukitolewa fursa mbadala za kukuza uchumi pasipo kushiriki uvuvi wa kutumia baruti.

Anasema hata samaki wanapokamatwa ufukweni na kuhusishwa na uvuvi wa kutumia baruti, ushahidi unakuwa mdogo kuishawishi mahakama kwa sababu hakuna vipimo vya kisayansi isipokuwa kutumia kigezo cha ‘samaki amelegea’.

Hifadhi za bahari

Serikali imejidhatiti kudhibiti uvuvi huo kwa kutumia njia tofauti, ikiwemo uanzishwaji wa Hifadhi ya Ghuba ya Mnazi na Maingilio ya Mto Ruvuma.

Redfrad Ngowo ni Kaimu Muhifadhi Mfawidhi wa hifadhi hiyo, anathibitisha kuwa uelimishaji na njia mbadala za kujipatia kipato na kukuza uchumi wa familia ni nyenzo muhimu katika kukabiliana na uvuvi wa kutumia baruti.

Anasema serikali kupitia taasisi mbalimbali mkoani Mtwara, imeshiriki kutoa elimu ya athari za uvuvi wa baruti na njia mbadala za kukuza kipato, huku ikiwashirikisha wananchi.

Ngowo anasema hatua hizo zilianza tangu kuanza kazi kwa hifadhi hiyo mwaka 2001, ikiwa ni mwaka mmoja tangu ilipotangazwa rasmi.

Hifadhi hiyo yenye kilomita za ukubwa 650, kati ya hizo, kilomita 430 zikiwa baharini na eneo la mikoko na 220 za nchi kavu, inahusika majukumu kadhaa, kubwa zaidi ikiwa ni kusimamia matumizi endelevu ya rasilimali za baharini.

Udhibiti hafifu

Ngowo anasema uvuvi wa kutumia baruti ni tatizo lililoshamiri nchini, ikilinganishwa na nchi jirani kama Msumbiji na Kenya.

Anasema baadhi ya raia wanaoshiriki uvuvi huo, wamekuwa wakikimbilia eneo la bahari lililopo nchini Msumbiji, ili kuwakwepa askari na maofisa wanaoshiriki doria.

“Wavuvi haramu wanapofanya uhalifu huo upande wa Tanzania, wanakimbilia Msumbiji kujificha, sasa hatuwezi kuwafuata kwa maana sheria za kimataifa hazituruhusu,” anasema.

Hata hivyo, Ngowo anasema kuna mazungumzo ya ushirikiano yanayofanywa kati ya Tanzania na Msumbuji ili kupata njia muafaka za kukabiliana na tatizo hilo.

Kwa upande mwingine, Ngowo anasema uanzishwaji wa miradi mbadala yenye lengo la kuiwezesha jamii ishiriki ipasavyo katika vita dhidi ya uvuvi haramu wa kutumia baruti umefanyika kwa maeneo ya hifadhi na yaliyoizunguka.

Anasema mafunzo ya miradi kama ufugaji samaki, ng’ombe, mbuzi, nyuki na kuku, hivyo kuyafanya maisha yao yasiwe tegemezi kwa bahari peke yake.

Ngowo anasema kumefanyika mafunzo na uratibu wa kuanzisha Benki za Jamii ya Vijijini maarufu kama Vicoba ambayo imewawezesha wananchi wanaoishi kwenye hifadhi hiyo kujihusisha na shughuli za nje ya uvuvi baharini.

Anasema fedha kwa ajili ya shughuli hizo zinatolewa na serikali na ufadhili wa nchi kadhaa za Ulaya.

Kwa hali hiyo, ni dhahiri kwamba uvuvi haramu wa kutumia baruti umeathiri na kupunguza fursa pana kwa wananchi wa Mtwara, huku ukihatarisha maisha ya uvuvi.

Umesababisha gharama na bei ya samaki kupanda, kupungua kwa idadi ya wavuvi na wachuuzi wa samaki.

Pamoja na changamoto nyingine zilizopo, kuna haja ya kuwepo jitihada za dhahiri zitakazoshirikisha jamii na wadau wengine kukabiliana na kuliangamiza tatizo la uvuvi haramu wa kutumia baruti.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles