



Wafanyakazi wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), wameeleza jinsi ufisadi na mipango mibovu inavyolimaliza shirika hilo kwa kununua vifaa nje na majengo kukaliwa bila kulipwa kodi.
Baadhi ya wafanyakazi hao walisema mikataba tata pia imesababisha shirika kununua umeme wa takribani bilioni 100 kila mwezi na wawekezaji kuweka vitega uchumi bila kulipa kodi kuwa ni miongoni mwa mambo yanayoliua shirika hilo.
NIPASHE Jumamosi wiki hii ilipata nafasi ya kuhojiana na baadhi yao jijini Dar es Salaam(waomba majina yasitajwe gazetini), kuhusu mambo wanayotaka Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kuyaangalia ili kuiokoa Tanesco na mzigo wa gharama kubwa za uendeshaji, walitaka serikali kuachana na utaratibu wa kifisadi wa ununuzi wa vifaa na mitambo kutoka nje.
Pia kulirudishia shirika hilo kampuni ya Mbeya Wood Poles, kuhakikisha majengo ya Tanesco yanalipiwa kodi, kuanzisha miradi ya nishati jadidi na kuwataka wawekezaji kulipa kodi .
Mahojiano hayo yalimshirikisha pia Mwenyekiti wa Kamati ya Majadiliano ya Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Viwanda na Biashara (TUICO ) Tanesco, Abdul Mkama, ambaye alifafanua na kuchambua hoja za wafanyakazi.
UNUNUZI WA VIFAA NA MITAMBO KUTOKA NG'AMBO
Watumishi hao walisema Tanesco inaagiza transfoma, nyaya na nguzo kutoka ng’ambo wakati bidhaa hizo zinapatikana hapa nchini , hivyo kumuomba Profesa Muhongo awasiliane na bodi ya zabuni na bodi ya wakurugenzi ya Tanesco kubadilisha utaratibu huo waliouita wa kifisadi ili kuokoa mapato.
Akifafanua , Mkama , alisema vifaa na mitambo hiyo inazalishwa hapa nchini hakuna sababu ya kuagiza nje vifaa ambavyo mara nyingi vina viwango duni.
“Transfoma zinazalishwa Arusha, nyaya kuna kiwanda cha East Africa Cables tunafikiri hakuna sababu ya kuvinunua nje , tunaomba Waziri alione hili.”
Kadhalika aliikumbusha Serikali kuondoa kodi kwenye vifaa, mitambo na mafuta yanayotumika kuzalisha umeme ili kupunguza gharama za uendeshaji.
KIWANDA CHA NGUZO MBEYA
Wafanyakazi waliomba serikali iwarudishie kiwanda cha kuzalisha nguzo cha Mbeya Wood Pole ambacho Serikali ya Awamu ya tatu ilikibinafsisha kwa mwekezaji binafsi hatua inayoifanya Tanesco kukosa nguzo ambazo ni muhimu kwenye kusambaza umeme.
Akitoa ufafanuzi wa suala hilo, Mkama alisema Mbeya Wood Poles ilikuwa ikipanda miti, kukata nguzo na kuziweka madawa na kwamba kiwanda kilizalisha nguzo za kutosha zilizodumu kwa miaka 20 hadi 30 .
Lakini baada ya kubinafsishwa shirika halina nguzo za kutosha tena hivyo kulazimika kuzinunua kwa bei kubwa kutoka kwa mwekezaji huyo huku zikiwa hazina viwango vinavyokubalika.
Alisema nguzo hizo zina uhai mfupi aghalabu hudumu kwa miaka mitano hivyo kuiongezea Tanesco mzigo wa kubadili nguzo kila mara na kulaumiwa na wateja mara kwa mara.
MAJENGO YA TANESCO
Wafanyakazi hao walisema wanamtaka Profesa Muhongo, ahakikishe kuwa jengo la Tanesco ambalo limegeuzwa kuwa makao makuu ya Wizara ya Nishati na Madini liwe linalipiwa kodi ili kuliongezea shirika mapato.
Wafanyakazi waliilaumu Serikali kwa kuchukua jengo lao na kukaliwa bure.
Aidha walimuomba waziri kuwarudishia nyumba yao iliyoko Upanga ambayo inatumiwa na hospitali ya Tumaini kwani wakilikodisha litawaongezea mapato.
Mkama alisema kuwa Tanesco ilijenga hospitali hiyo lakini hatua yao ilipingwa na serikali ya Awamu ya Tatu na nyumba hiyo ikaanza kutumiwa na hospitali hiyo ya Tumaini, lakini sasa shirika linalihitaji hivyo Waziri awasaidie lirudishwe kwao.
MIRADI YA NISHATI JADIDI (renewable energy).
Katika majadiliano, hayo wafanyakazi walitaka Profesa Muhongo atenge fedha na kutekeleza miradi ya uzalishaji umeme kutoka vyanzo mbadala ikiwemo, mkaa wa mawe, jua na upepo. Walisema licha ya Tanesco kuwa na nia ya kuongeza wateja 100,000 kila mwaka, chanzo cha umeme kinabaki kuwa mafuta na gesi pekee hali inayokwamisha malengo yao.
Walitaka utafiti wa umeme wa upepo kutoka Same na Singida ukamilike, uzalishaji uanze, na pia chanzo cha nishati ya jua nacho kipewe kipaumbele kwa Wizara kutoa fedha za utekelezaji badala ya kutoa litany ya ahadi.
TANESCO KUNUNUA UMEME KWA BILIONI 86 KILA MWEZI
Akizungumzia mikataba ya umeme, Mkama alisema mikataba iliyofungwa baina na serikali na makampuni ya umeme inaigharimu Tanesco Sh. bilioni 86 kwa mwezi jambo ambalo ni kitanzi shingoni mwa shirika hilo linalokusanya bilioni 56 tu kwa mwezi.
Mkama alisema shirika linazilipa fedha za kigeni zinazofikia bilioni 86 kampuni za Symbion, IPTL, Songas na PAN African Energy Tanzania (PAT).
Wafanyakazi walimtaka Waziri kushauri na kushirikiana nao katika kuongeza mapato ya TANESCO ili kuipunguzia mzigo mkubwa shirika linaoubeba kila mwezi.
WAWEKEZAJI KULIPA KODI YA PANGO
Wafanyakazi hao waliwalaumu wawekezaji wakubwa wa miradi ya umeme ambao licha ya kuwekeza nchini na kuuza umeme kwa gharama kubwa tena kwa fedha za kigeni hawalipi kodi na wanatumia ardhi ya Tanesco kuweka mitambo na vifaa vyao.
“Hivi inakuwaje hata maskini wa mwisho analipa kodi ya ardhi kupitia kiwanja chake iweje wawekezaji hawa wanatumia ardhi ya Tanesco (Tanzania) bure bila kulipa gharama ya pango/kodi…. Waanze kulipa kodi waongeze kipato chetu” alisema mfanyakazi wa idara ya miliki (estate).
Jitihada za kuwasiliana na Waziri Muhongo juu ya kutekeleza ushauri wa Tanesco zinaendelea. Hata hivyo kiongozi huyo yuko nje ya nchi kikazi.
Wiki mbili zilizopita Muhongo alizuru Tanesco na kupewa majina na mambo yanayodaiwa kulikwamisha shirika hilo kutoa huduma ya umeme endelevu.