Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

TBL yasaidia uchaguzi Yanga

5th July 2012
Print
Comments
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah

Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) jana iliikabidhi Yanga hundi ya Sh. milioni 20 kwa ajili ya kusaidia gharama za uchaguzi wa klabu hiyo utakaofanyika Julai 15 kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

Wanajangwani wanafanya uchaguzi huo mdogo baada ya waliokuwa viongozi wake, akiwemo mwenyekiti Lloyd Nchunga, kutangaza kujiuzulu na kufanya idadi ya viongozi waliobaki madarakani kuwa ndogo kiasi cha kutoruhusiwa kufanya maamuzi yoyote kama katiba ya klabu hiyo inavyoelekeza.

Akizungumza jana, kaimu meneja wa bia ya Kilimanjaro, Oscar Shelukindo, alisema lengo la kusaidia gharama za mkutano huo ni kutaka kuona Yanga ikipata viongozi bora ambao wataendeleza mchezo wa soka nchini.

Shelukindo alisema kuwa wanaamini kuwa viongozi watakaochaguliwa watahakikisha wanaongoza kwa kufuata katiba na kuepusha migogoro ambayo inatokana na viongozi wasiofuata maadili.

"Tunaamini viongozi watakaopatikana watahakikisha wanafuatilia na kuzingatia yale yaliomo kwenye mkataba kama tulivyokubaliana," alisema Shelukindo.

Katibu Mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa, alisema wanaishukuru TBL kwa kuwapa fedha hizo na wanaahidi kwamba watafanya uchaguzi wa haki ili kupata viongozi watakaoisaidia klabu hiyo.

Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah, aliwataka wanachama wa Yanga kuhakikisha watazingatia utawala bora kwa kuhakikisha demokrasia inakuwepo kwenye kupata viongozi.

Osiah alisema pia haipendezi kuona fedha za wadhamini zinatumika kusimamia uchaguzi mdogo badala ya kuwepo mkutano mkuu ambao utawapa nafasi wanachama kujua taarifa za utendaji na kujadili maendeleo ya klabu yao.

Aliitaka pia TBL isirudi nyuma na iendelee kusaidia maendeleo ya soka hapa nchini.

TBL ni wadhamini wa klabu za Simba na Yanga na ahadi ya kusaidia gharama za mkutano mkuu zilitolewa na kampuni hiyo katika mkutano mkuu wa mwaka wa Simba uliofanyika mwaka jana.

BUNAMWAYA


Yanga watatua dimbani Jumapili kujipima nguvu na timu ya Bunawaya kutoka Uganda kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maandalizi yao kabla ya kushiriki michuano ya Kombe la Kagame itakayoanza Julai 14.

Akizungumza na NIPASHE jana, Afisa Habari wa Yanga,  Louis Sendeu, alisema kuwa kama watafikia makubaliano, kocha wao mpya, Tom Santiefe atakuwepo uwanjani kushuhudia mechi hiyo, pamoja na kocha msaidizi Fred Felix Minziro.



SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment