Thursday May 5, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Waliotemwa uwaziri, u-DC waache kulalamika-Maaskofu

13th May 2012
Print
Comments
Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk. Thomas Laizer

Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk. Thomas Laizer, amewanyooshea kidole baadhi ya mawaziri na wakuu wa wilaya waliotemwa kwenye uteuzi mpya uliofanywa na Rais Dk. Jakaya Kikwete, kuwa waache kulalamika kwamba hawajatendewa haki kana kwamba hawajui taratibu za utendaji serikalini.

Badala yake waendelee kuutumikia umma wa Watanzania kwa nafasi nyingine walizonazo katika jamii, kwani mabadiliko hayo ni ya Kikatiba na Rais ana mamlaka ya kufanya hivyo pale anapoona kuna hitaji.

Dk. Laizer aliyasema hayo wakati akiwasilisha salamu za Dayosisi yake na kuvunja tanga mara baada ya kumalizika kwa mazishi ya Mzee Elitira Abraham Mengi (85), aliyezikwa kitongoji cha Kisereny kijiji cha Nkuu, Machame kata ya Machame Mashariki, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro na kuhudhuriwa na maelfu ya watu.

“Juzi Rais Kikwete amefanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri na Wakuu wa wilaya, wapo waliokuwepo wamerudi na wengine wameondolewa, kumekuwa na maneno mengi wengine wakidai hawajatendewa haki, wanaosema hivi hawajasoma taratibu za serikali, Katiba inampa nguvu Rais kufanya mabadiliko wakati wowote, tuache kulalamika, mshukuru Mungu na uungane na wanajamii kujenga Taifa” alisema

Naye, Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Martin Shao, alisema aliwataka mawaziri ambao hawajafanikiwa kupewa nafasi hizo kujipa moyo, kwani Tanzania inajengwa na wote wenye moyo kwa kufanya kazi kwa bidii na kuutumikia umma popote walipo kwani nafasi hizo ni za kupokezana na sasa wameshika wengine.

Katika mahubiri yake kwenye ibada ya kumuombea Marehemu Elitira Mengi, Askofu wa Dayosisi ya Pare, Charles Mjema, alisema kila mtu ayatafakari maisha anayoishi humu duniani kama ni yenye kumpendeza Mungu au kumchukiza kwa kuwa mwenye kudhulumu mali ya umma, mkandamizaji wa haki za wengine, migogoro isiyokwisha na mtababaishaji na mtesi wa kanisa la Mungu.

“Kwa sasa wapo wanaokufa kama hawajawahi kuishi na wapo wanaoishi kama hawatakufa, fikra zao hazijajijenga kuwa kuna maisha baada ya haya, wanafanya dhuluma, ufisadi, uonevu, wengi wananyimwa haki kuanzia ngazi ya familia hadi kitaifa… haijalishi umeishi kwa miaka mingapi bali umefanya nini cha kumpendeza Mungu katika maisha yako ya duniani”, alisema.

Aidha aliwataka viongozi wa kisiasa nchini kuishi na kufanya shughuli zao kama ndugu na kuacha kujengeana chuki na uadui ambao unahatarisha amani na utulivu wa nchi yetu.

Alisema hivi karibuni viongozi wa dini zote walikutanishwa katika semina ya pamoja ya kujadili amani ya nchi na kuweka mahusiano mazuri baina yao, ambapo viongozi hao walipaswa kukaa kwa umoja na kuwaunganisha waumini wao ili kuhakikisha amani ya nchi haviathiriki.

“Viongozi wa dini tunaelewa umuhimu wa tunu ya amani tuliyonayo na tunawajibika kuilinda na tunajua wazi wakristo wapende wasipende lazima waislamu wawepo na vivyo hivyo waislamu wapende wasipende lazima wakristo wawepo sasa ugomvi wa nini” alihoji Laizer

Alisema pamoja na kuwakutanisha viongozi wa dini, lakini viongozi wa kisiasa wamekuwa wakifanya tofauti na kwamba viongozi wa dini pekee hawawezi kuilinda amani ya nchi iwapo viongozi wa kisiasa hawataishi kama ndugu.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles